Thursday, March 24, 2016

WAWILI WASHIKILIWA KWA UTAPELI WAWILI WAKIMBIA

Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutaka kumtapeli mtu mmoja kiasi cha shilingi milioni tatu kwa kumuuzia madini aina ya Almasi ambayo ni bandia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa watu hao ambao walikuwa wanne wengine wawili walifanikiwa kukimbia walikamatwa baada ya kutaka kukimbia kutokana na mlalamikaji kupiga kelele ya kuomba msaada.
Mushongi alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi eneo la CCM Mkoani wilayani Kibaha majira ya saa 3:30 asubuhi baada ya mlalamikaji kutoka kuchukua fedha kwenye benki ya NMB Tawi la Kibaha.
“Mlalamikaji mara baada ya kuchukua fedha alikutana na watuhumiwa hao ambapo waliongea naye na kumwambia kuwa wanauza madini aina ya Almasi ambapo walikubalina na akawakabidhi fedha hizo,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa watuhumiwa hao wakiwa kwenye gari aina ya Primio lenye namba za usajili T 668 DFY walianza kuondoka lakini mlalamikaji akagundua kuwa madini yale si halisi na kuanza kupiga kelele za wezi kuomba msaada ndipo waendesha pikipiki walipoanza kuwafukuza na baadaye polisi nao wakatokea na kuwakamata.
“Watuhumiwa hao baada ya kuona wamezingirwa walikimbia hata hivyo wawili walikamatwa na wengine wawili walifanikiwa kutokomea kusiko julikana nab ado tunaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine ili kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema Mushongi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwantumu Juma maarufau kama Hawa, Fidelis Buberwa au Finas Barongo ambao wanashikiliwa kutokana na tukio hilo ambapo gari hilo linashikiliwa.
Kufuatia tukio hilo kamanda aliwataka wananchi kutokubali kuuziwa madini mikononi badala yake waende sehemu husika ambazo ziko rasmi kwa ajili ya uuzaji wa madini ili kuepukana na watu kama hao.
Mwisho

MMOJA AFA 10 WALAZWA KIPINDUPINDU

Na John Gagarini, Kibaha
MTU mmoja amefariki dunia wilayani Kibaha mkoani Pwani kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu huku wengine 10  wakiwa wanaugua ugonjwa huo kwenye hospitali mbalimbali wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha Ofisa afya wa mkoa wa Pwani Simon Malulu alisema kuwa ugonjwa huo uligundulika Aprili 17 mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Ruvu wilayani Kibaha.
Malulu alisema kuwa ugonjwa huo uliwakumba wanafunzi 21 wa shule hiyo ambapo awali waliona kuwa ni mchafuko wa matumbo kwani wanafunzi hao walikuwa wakiharisha.
“Baada ya kuona hali imezidi kuwa mbaya kwa wanafunzi walimu waliwapeleka wanafunzi kwenye Zahanati ya Kijiji cha hicho cha Ruvu Station na kuchukua sampuli ya kinyesi kwa wanafunzi tisa ambapo mmoja aligundulika kuwa na ugonjwa huo,” alisema Malulu.
Alisema kuwa baada ya kubaini hilo ilibidi mkuu wa wilaya aifunge shule hiyo ili kuwaepusha wanafunzi zaidi kuambukizwa ugonjwa huo ambapo wanafunzi waliokumbwa na ugonjwa huo wengi walikuwa ni wanafunzi wakike ambao wako bweni.
“Hadi sasa kwenye Zahanati ya Ruvu kuna wagonjwa wanne, Zahanati ya Dutumi watatu na Mlandizi wako watatu ambao wanendelea kupatiwa matibabu ya ugonjwa huo,” alisema Malulu.
Aidha alisema kuwa chanzo cha kuenea ugonjwa huo ni kinyesi ambacho kinatokana na watu wengi kujisaidia kwenye Mto Ruvu ambapo maji yake wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Ruvu Station.
“Tumechukua hatua za kufungua kambi kwenye maeneo yote yenye ugonjwa ikiwa ni pamoja na Ruvu Station, Dutumi na Mlandizi pia kuwaptia dawa ya kusafishia maji ili kutibu maji hayo ambayo wananchi wamekuwa wakiyatumia bila ya kuyachemsha,” alisema Malulu.
Aliongeza kuwa wananchi wanatakiwa kutumia vyoo pia wanatoa elimu ya jisni ya kujikinga na ugonjwa huo na kufanya ukaguzi  wa taasisi za umma, shule, nyumba za watumishi kuzuia upikwaji wa vyakula na uuzaji wa vinywaji na kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Ugonjwa huo mwaka jana Agosti ulitokea mkoani Pwani na kuisha Desemba ambapo 293 waliambukizwa huku 98 walibainika kuwa na ugonjwa huo huku watu watatu walipoteza maisha.
Mwisho.

Saturday, March 19, 2016

SHULE YAKABILIWA NA UHABA WA WALIMU INA WALIMU WAWILI TU

Na John Gagarini, Bagamoyo
MAZINGIRA magumu yanayokikabili Kijiji cha Kitame Kata ya makurunge wilayani bagamoyo mkoani Pwani yamesababisha walimu walimu wawili wanaofundisha shule hiyo kufundisha kwa siku 90 kwa mwaka mzima.   
Kutokana na shule hiyo kuwa kwenye mazingira magumu walimu wengi wamekuwa hawako tayari kufundisha shule hiyo yenye wanafunzi 51 wa kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ambayo ni idadi ndogo kutokana na mazingira hayo.
Akizungumza mbele ya Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa, moja ya wakazi wa Kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Adam Rashid alisema kuwa moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na kutokuwa na usafiri wa uhakika kutokana na ubovu wa miundombinu.
“Usafiri wa kutokana Kijijini hapa hadi makao makuu ya wilaya ni kilometa 54 kwa njia ya barabara na usafiri wake ni pikipiki na gharama yake ni kiasi cha shilingi 50,000 huku ule wa kutumia njia ya bahari mitumbwi gharama yake ni kiasi cha shilingi 60,000 kwenda na kurudi,”  alisema Rashid.
Alisema gharama hizo ni kubwa sana ajambo ambalo linawafanya walimu washindwe kwenda kufundisha kutokana na mazingira hayo ambapo walimu hao wawili wamekuwa wakipokezana kufundisha madarasa hayo.
“Wanafunzi wanafundishwa siku chache kutokana na walimu hao wakati mwingine kutofika kabisa shuleni hali ambayo inawakatisha tamaa wanafunzi na kusababisha kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo,” alisema Rashid.
Aidha aliiomba serikali kusaidia kupatikana kwa walimu ili kukabiliana na hali ya wanafunzi hao kukosa masomo na kusababisha elimu kuwa duni hali ambayo itatoa matokeo mabaya kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Makurunge Kabile Paulo alisema kuwa walimu wengi wanashindwa kwenda kufundisha shuleni hapo kutokana na mazingira magumu kwani hakuna huduma muhimu za jamii hivyo kushindwa kukaa huko.
Paulo alisema kuwa baadhi ya huduma ambazo hazipo ni pamoja na huduma ya afya kwani hakuna zahanati na huduma nyingine muhimu ambazo huwabidi kuzifuata Bagamoyo au maeneo mengine jambo ambalo limekuwa likiwagharimu.
Naye mbunge wa Jimbo hilo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa kweli hiyo ni changamoto ambayo inawakabili wakazi na walimu hao lakini kwa kushirikiana na diwani wa kata hiyo watahakikisha wanaitatua.
Dk Kawambwa alisema kuwa Halmashauri itafanya mgao wa walimu na ataiomba itoe kipaumbele kwa shule hiyo kwa kuwapatia walimu ili waweze kwenda huko na kuongeza nguvu ya ufundishaji kwenye shule hiyo ambayo iko pembezoni na kuwataka vijana waliosoma vyuo vya ualimu na ni wenyeji wa kata hiyo kujitolea kwenda kufundisha kama njia mbadala ya upungufu huo wa walimu.
Mwisho.  
  

VIJANA KUENDESHA MRADI WA SAMAKI MTAA WA KIBONDENI

Na John Gagarini, Kibaha
MTAA wa Kibondeni Kata ya Mkuza wilayani Kibaha utawapatia mafunzo ya ufugaji wa samaki vijana 40 wa mtaa huo ili waendeshe mradi wa ufugaji wa samaki kwenye bwawa la mtaa ambalo limerudishwa baada ya kuuzwa kimakosa kwa mtu binafsi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Hamis Mwarizo alisema kuwa vijana hao watapewa mafunzo hayo kutoka ofisi ya kata ili vijana waweze kujua namna ya kufuga samaki.
Mwarizo alisema kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa vijana ambao watakuwa wameunda vikundi ambavyo vitaendesha mradi huo ambao utatoa ajira kwa vijana hao na watakuwa wakipeana zamu ya kusimamia.
“Lengo la mradi huo ni kuongeza ajira kwa vijana ambapo asilimia 70 ya mapato yatakwenda kwenye kikundi na asilimia 30 yatakwenda kwenye mtaa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii ya mtaa wetu,” alisema Mwarizo.
Alisema kuwa kwa sasa tayari vijana 16 wameshapatikana kwa ajili ya kuanzisha kikundi cha mwanzo na wengine wanaendelea kujiandikisha na baadaye kikundi hicho kitasajiliwa ili kitambulike kisheria baada ya mradi huo kupitishwa ana wananchi kwenye mkutano mkuu wa mtaa.
“Kundi la kwanza litaendesha kwa kipindi cha miaka 10 na baadaye litapewa kundi lingine kwa ajili ya kuendeleza mradi huo ambao mbali ya kuwapatia vijana ajira pia utaipatia jamii ya eneo hilo na maeneo jirani lishe kwa ajili ya kuboresha afya,” alisema Mwarizo.
Katika hatua nyingine alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na taratibu za kulipima eneo la bwawa hilo ili kujua mipaka yake halisi ambapo maji yake baada ya kupimwa yalibainika kuwa hayafai kwa kunywa kwani yana viluilui ambavyo vinaweza kusababisha maradhi ya ugonjwa wa tumbo hivyo yatatumika kwa ajili ya kulimia bustani pamoja na kufulia.
Mwisho.


WAFANYABIASHARA WA NAFAKA WAIOMBA HALMASHAURI KUWAONDOLEA USHURU

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wa jumla na rejareja wa mazao ya nafaka kwenye soko la maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba Halmashauri ya Mji huo kuondoa ushuru wa shilingi 1,000 kwa gunia la kilogramu 100 la nafaka linaloingia sokoni hapo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha katibu wa umoja wa wauzaji wa mazao ya nafaka sokoni hapo Ramadhan Maulid alisema kuwa sheria hiyo ya utozaji wa ushuru wa shilingi 1,000 kwa gunia la la nafaka lenye uzito wa kilogramu 100 ina kinzana na sheria mama ambayo inataka ushuru ukatwe mara moja tu.
Maulid alisema kuwa wao wanaponunua nafaka hizo huko mikoani wanatozwa ushuru wa shilingi kati ya 2,000 hadi 5,000 kutegemeana na Halmashauri hivyo wanashangaa kutozwa tena mara wanapofikisha mzigo sokoni hapo.
“Kututoza ushuru tena ni sawa na kuwatoza ushuru mara mbili kwani hata sheria ndogo hiyo iliyowekwa na Halmashauri haikuwashirikisha wao kama watekelezaji wa sheria hiyo ambayo ilipitishwa mwaka 2007 na kutakiwa kuanza kutumika mwaka 2008 lakini haikuwahi kutumika licha ya kwamba kwa miaka ya nyuma ilikuwa ikitumika,” alisema Maulid.
Alisema kuwa waliletewa taarifa ya kutakiwa kulipa ushuru huo hivi karibuni lakini walijaribu kuonana na viongoizi wa halmashauri bila ya mafanikio ili kuzungumzia suala hilo ambalo kwao ni moja ya ushuru ambao ni kero.
“Mbali ya kutakiwa kulipia kiasi hicho pia gharama nyingine ni pamoja na kulipia Kizimba kiasi cha shilingi 9,000, Ardhi 3,000 na mlinzi 6,000 ambazo hulipa kila mwezi hivyo malipo hayo ni sawa na kuwaongezea mzigo wa ushuru,” alisema Maulid.
Aidha alisema kuwa kwa sasa wanawasiliana na wanasheria ili kutoa tafsiri ya sheria hizo mbili kati ya sheria mama na sheria ndogo ya Halmashauri ambapo inaonekana kama zinakinzana na kuleta mkanganyiko kwao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa soko hilo Ally Gonzi alisema kuwa tangu walipoletewa sheria hiyo ndogo ambayo ilipitishwa kwenye baraza la madiwani walijaribu kufanya vikao mbalimbali na Halmashauri ili kuangalia namna ya kupunguza ushuru huo lakini ilishindikana ambapo Halmashauri iliwaambia kuwa kama wanataka uondolewe basi wafuate taratibu.
Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Gladdys Dyamvunye alisema kuwa wafanyabiashara hao wanapaswa kulipa ushuru huo kwani uko kisheria na tayari vyombo vya sheria vimetoa siku 14 kwa wafanyabiashara hao kulipa na endapo hawatalipa watashitakiwa.
Mwisho.


RAS PWANI KUFUNGUA MAFUNZO YA MPIRA WA WAVU

Na John Gagarini, Kibaha
KATIBU Tawala (RAS) Mkoa wa Pwani Mgeni Baruani anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya walimu wa mchezo wa wavu Volleyball yatakayoanza Machi 24 hadi Aprili Mosi mwaka huu kwenye viwanja vya shule ya Msingi Kibaha.
Akizungumza na waandishi wa habari katibu wa chama cha mchezo huo mkoani Pwani (COREVA) Lonjin Mzava alisema kuwa wanatarajia mafunzo hayo yatawahusisha walimu wa mchezo huo kwa shule za msingi walimu wanne , sekondari walimu wanne , vyuo pamoja na wadau wengine wanaopenda kujifunza mchezo huo.  
Mzava alisema kuwa washiriki watatoka wilaya zote za mkoa wa Pwani ambapo kwa walimu tayari barua za kuomba ushiriki wao zimepelekwa kwa wakurugenzi wa Halmashauri ili kuwpaatia ruhusa ya kushiriki mafunzo hayo.
“Wanafunzi wa mchezo huo watajifunza masomo ya darasani pamoja nay a vitendo ili kuwajengea uwezo wa kuujua mchezo huo hata watakapokwenda kuwafundisha wengine wawe na maarifa ya kutosha na mafunzo haya yameandaliwa kwa pamoja na chama cha mchezo huo nchini (TAVA) alisema Mzava.
Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa ujuzi wa kutosha walimu wa mchezo huo ili waweze kujua sheria na namna mchezo unavyochezwa na kuusimamia kama sheria za mchezo huo zinavyoonyesha na kupitishwa na chama cha mchezo huo cha kimataifa FIVB.
“Hadi sasa walimu kutoka Hlamashauri za Bagamoyo, Mkuranga, Rufiji na Kibaha Mji tayari wamethibitisha kushiriki mafunzo hayo na waliobaki wanapaswa kuthibitisha kabla ya tarehe 22 Machi ili waweze kuwekewa utaratibu wa kushiriki mafunzo hayo,” alisema Mzava.
Aidha alisema kuwa walimu watakaofanya vizuri kwenye mafunzo hayo watapata nafasi ya kushiriki mafunzo ya Kimataifa ya Beach yatakayofanyika Aprili mwaka huu Jijini Dar es Salaam hivyo itasaidia kuutangaza mkoa kupitia mchezo huo.
“Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kudhamini mafunzo haya kwani hata wakitoa maji au kitu chochote itasaidia kupunguza gharama za kuendesha mafunzo hayo kwani hadi sasa hakuna wadhamini waliojitokeza kuzamini mafunzo hayo,” alisema Mzava.
Alibainisha kuwa matarajio ni kuzalisha walimu wengi wa mchezo huo hasa mashuleni na itasaidia kupunguza gharama za kuwalipa walimu toka nje hawa wakati wa mashindano ya Umoja wa Shule za Msingi na Utamaduni Tanzania( UMITASHUMTA) na Umoja wa Shule za Sekondari na Sanaa Tanzania (UMISSETA).

Mwisho. 

Monday, March 14, 2016

CHUO CHA KILIMO NA MIFUGO CHAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA ZANA ZA KILIMO

Na John Gagarini, Bagamoyo
CHUO cha Kilimo na Mifugo Kaole wilayani Bagamoyo kinachomilikiwa na Jumuiya ya wazazi Tanzania kinakabiliwa na upungufu wa madawa ya kujifunzia kwenye maabara pamoja na zana za kujifunzia hali ambayo inasababisha wanachuo kushindwa kujifunza kikamilifu.
Hayo yalisemwa Bagamoyo na Rais wa Chuo hicho Abas Kasusumo wakati wa ziara iliyofanywa na Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo ambao walitembelewa na Jumuiya hiyo wilaya ya Temeke kuangalia shughuli zinazofanywa na Jumuiya hiyo.
Kasusumo alisema kuwa changamoto hizo zinawasababisha washindwe kujifunza ipasavyo hali ambayo inawafanya wawe katika wakati mgumu kuelewa masomo yao.
“Tunaomba tusaidiwe vifaa vya kujifunzia kama vile matrekta ambayo hapa yapo lakini hayafanyi kazi hivyo tunaiomba serikali na Jumuiya ambayo ndiyo wamiliki wa chuo chetu ili tupate vifaa vya kujifunzia,” alisema Kasusumo.
Alisema kuwa kutokana na chuo hichi kuwa cha mifugo pia kuna changamoto ya ukosefu wa madawa mbalimbali kwa ajili ya kujifunzia masomo yetu kwani wakitoka hapo watategemewa kufanya kazi kutokana na walivyojifunza.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa chuo hicho Carthert Liwa alisema kuwa changamoto nyingine ni umeme ambapo wanatumia mita ya Luku ambayo haiwezi kumudu matumizi makubwa.
Liwa alisema kuwa changamoto zimekuwa nyingi kwani chuo hicho kimeanza upya baada ya kutokea matatizo hivyo wadau wanaombwa kujitokeza kukisaidia ili kiweze kutoa mafunzo kwa viwango vinavyotakiwa.
Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo ambao ndiyo wamiliki wa chuo hicho Abdul Sharif alisema kuwa watahakikisha wanshirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha kinatoa mafunzo kwa ubora.
Sharif alisema kuwa changamoto zilizotajwa ni za kweli na Jumuiya kwa kushirikiana na makao makuu watazifanyia kazi changamoto hizo ili elimu bora iweze kupatikana chuoni hapo. Chuo hicho kina wanafunzi 36 lakini uwezo wake ni wanachuo 600 ambapo hali hiyo ilitokana na kuchelewa kuandikisha wanachuo.
Mwisho.