Tuesday, September 22, 2015

KAMPENI ZAENDELEA JIMBO LA CHALINZE

Na John Gagarini, Mandela
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi Ridhiwani Kikwete amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo atahakikisha zahanati inajengwa kwenye Kijiji cha Kibaoni ili kuwaondolea adha wananchi wa kijiji hicho.
Aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kijijini hapo kata ya Mandela na kusema kuwa ilani ya chama anasema kila kijiji lazima kiwe na zahanati huku kila kata ikitakiwa kuwa na kituo cha afya ili kurahishisha upatikanaji wa huduma za afya karibu.
Ridhiwani alisema kuwa hicho kitakuwa moja ya vipaumbele vyake ambavyo atahakikisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ujenzi huo unakamilika na wanakijiji wanapata huduma za afya karibu tofauti na sasa ambapo huwalazimu kwenda kijiji jirani cha Mandela.
“Ilani ya chama inasema kuwa kila kijiji lazima kiwe na zahanati hivyo endapo nikichaguliwa kwenye nafasi hii ya ubunge kwa kushirikiana na wananchi hivyo nitahakikisha zahanati inajengwa ili huduma zipatikane karibu,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa hata kata ya Mandela haina Kituo cha afya ambapo kata hiyo ni mpya ambayo imezaliwa kutoka kata ya Miono na kutaka ujenzi wa kituo hicho cha afya kujengwa kwenye kijiji hicho.
“Katika kipindi cha uongozi wangu wa mwaka mmoja na miezi miwili tumeweza kukarabati zahanati 24 huku nane zikiwa zimejengwa pia tumeweza kufanikisha kujngwa nyumba za waganga pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba na dawa,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya vijiji kukosa zahanati hata hivyo mikakati ni kuhakikisha zinajengwa ambapo mipango inaendelea kwa kushirikiana na wananchi.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa kata ya Mandela Madaraka Mbode alisema kuwa tayari kata imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati kwenye kijiji cha Kibaoni.
Mbode alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo utafanikiwa endapo wananchi watawachagua wgombea kutoka CCM lakini endapo wakiwachagua viongozi wa vyama vya upinzani hawataweza kupata maendeleo.
Naye mkazi wa Kibaoni Ally Athuman alisema kuwa changamoto kubwa inayowakumba wananchi kwenye zahanati wanazokwenda kupata matibabu ni ukosefu wa dawa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mandela
MGOMBEA Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mandela wilaya ya Bagamoyo Madaraka Mbode amemwomba mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kusimamia ujengwaji wa tenki kubwa la maji ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji.
Mbode aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Lupungwi wakati wa mkutano wa kampeni za Ubunge nakusema kuwa Ridhiwani ndiye aliyeanzisha mchakato wa ujengwaji wa matenki kwenye baadhi ya vijiji.
Alisema kuwa awamu ya pili imevifanya vijiji vingi kwenye Jimbo hilo kuwa na maji lakini baadhi bado havijapata huduma hiyo ambapo awamu ya tatu ya mradi wa maji utavifikia vijiji na vitngoji ambavyo havikubahatika kupata maji.
“Wananchi nawaombeni mchagueni Ridhiwani kwani anauwezo wa kutufanikishia kupata maji ambapo kwa sasa maji yanatoka lakini endapo kunatokea tatizo kwenye mtambo maji hayapatikani ndiyo maana ujenzi wa matenki makubwa unaanza ili kuhakikisha maji yanapatikana muda wote,” alisema Mbode.
Aidha alisema kuwa anaomba na yeye achaguliwe kwenye nafasi ya udiwani ili ashirikiane na mbunge huyo kuwaletea maendeleo ambapo kwa sasa kijiji hicho kimewekewa nguzo kwa ajili ya kuwasambaziwa umeme.
Naye Ridhiwani Kikwete alisema kuwa tayari tathmini imeshaanza kufanywa ambapo wataalamu wameshachukua udongo kwa ajili ya kupima kabla ya kujenga tenki hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mengi.
Ridhiwani alisema kuwa awamu hii ya tatu ya mradi wa maji wa wami chalinze utavifikia vijiji na vitongoji vyote sambamba na ujengaji wa matenki makubwa kwa ajili ya kuhifadhia maji.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mandela
BAADHI ya waangalizi wa uchaguzi wamesema kuwa Tanzania imeweka historia kwa kuwa na waangalizi wengi kwenye uchaguzi wa mwaka huu hali ambayo itafanya uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Hayo yalisemwa jana na mwangalizi wa ndani kutoka (TEMCO) Renatus Mkinga kwenye kijiji cha Lupungwi kata ya Mandela wilayani Bagamoyo wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete.
Mkinga alisema kuwa kwa waangalizi wa ndani ni zaidi ya 6,000 huku wale wa kutoka nje wakiwa ni 600 ambao ni wengi na haijawahi kutokea katika chaguzi zilizopita.
“Sisi hatuna vyama tunachokifanya ni kuangalia ,mwenendo mzima wa uchaguzi kuanzia hatua ya kampeni hadi utakapofanyika uchaguzi Oktoba 25 mwaka huu,” alisema Mkinga.
Alisema kuwa kazi ya wasimamizi ni kuangalia mienendo ya uchaguzi katika kampeni na anaamini kuwa utakuwa huru na haki kwani hadi sasa kampeni zinaendele vizuri.
“Tunahudhuria kwenye mikutano ya vyama mbalimbali ili kuangalia wanapiga kampeni vipi na kuangalia wananchi wanajitokeza vipi kusikiliza sera za vyama husika,” alisema Mkinga.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za vyama mbalimbali ili waweze kuangalia ni mgombea gani ambaye anawafaa ili mwisho wa siku waweze kumchagua kiongozi bora na si bora kiongozi.
Mwisho.
   

        

Monday, September 21, 2015

SITA WAFA WANNE WAJERUHIWA

 Na John Gagarini, Mkuranga
WATU sita wamepoteza maisha na wanne kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria kugongana uso kwa uso na basi kubwa la kampuni ya Ibra.
Ajali hiyo ilitokea jana katika kijiji cha Njopeka wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Jafari Ibrahim alithibisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa katika ajali hiyo watu sita amekufa na wanne kujeruhiwa.
Ibrahim alisema basi hilo kubwa  lenye namba za usajili T 195 DCE aina ya YU TONG likiendeshwa na Alex Peter (46) liligongangana na gari ndogo iliyokua ikitokea Jaribu kuelekea Mbagala jijini Dar Es Salam lenye namba za  usajili T 782 DC.
Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo kuwa ni dereva wa Basi la Ibra kuendesha zaidi kulia na hivyo kukutana uso kwa uso na kusababisha ajali hiyo.
Aidha alisema baada ya ajali hiyo wamelazimika kuweka askari katika eneo hilo, huku wakiwataka madereva kuwa makini na sheria za barabarani.
Ibrahim aliwasihi wananchi kutoa taarifa kwa Askari wa Usalama barabarani kwa namba zilizopo kwenye mabasi pindi wanapobaini kukiukwa kwa sheria za barabarani kabla ajali haijatokea.
Mwisho.

WENGI WAMUAGA MTOTO WA ALIKUWA KIONGOZI WA WAFUGAJI, RAIS DK JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Na John Gagarini, Lugoba
WAGOMBEA wanaowania nafasi za uongozi hapa nchini wametakiwa kukubali matokeo mara uchaguzi utakapofanyika Oktoba 25 mwaka huu kwani kuna maisha mengine baada ya uchaguzi  kuendelea kufanya kampeni zao huku wakiendelea kuhubiri na kulinda amani iliyopo kwani wana nafasi kubwa ya kuwashawishi wafuasi wao wasifanye vurugu au kufanya vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa amani.
Pia wagombea watakaoshindwa kwenye uchaguzi mkuu wakubali matokeo kwani kwenye washindani lazima kuwe na washindwa ili kuondoa hali ya mafarakano kwani kwa wale watakaoshindwa wasipokubali matokeo wanaweza kuleta uvunjifu wa amani.
Hayo yalisemwa juzi Kijiji cha Maviayangombe kata ya Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na Askofu mkuu wa Dayosisi ya Morogoro ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jacob Mameo Ole Paulo wa Dayosisi ya Morogoro wakati wa mazishi ya mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa wafugaji Laban Moreto, Karokya Moreto (33) ambaye alikuwa mwanajeshi wa kikosi cha 04/691 cha Mtwara.
Askofu Ole Paulo alisema kuwa wagombea hao wanauwezo wa kudumisha amani kwa kuhubiri au kuingiza nchi kwenye machafuko endapo watayatumia vibaya majukwaa wakati wa kipindi hichi cha kampeni za uchaguzi.
“Wanapaswa kuhubiri amani na kuacha kutumia maneno yatakayo haribu amani ya nchi iliyopo ambayo imedumu kwa kipindi kirefu tangu nchi ilipopata uhuru miaka zaidi ya 50 hivyo itakuwa ajabu ivunjwe kisa kuwania uongozi tu,” alisema Askofu Ole Paulo.
Aidha alisema kuwa vyama vya siasa vinapaswa kupingana kwa hoja na kwa malumbano ambayo hayana maana bali yanaweza kuleta mitafaruku isiyokuwa ya lazima hasa kwa wale wanaoshindwa kwani wanapaswa kukubali matokeo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa amesikitishwa na kifo cha marehemu ambaye alikuwa ni ndugu kwani wamekuwa wakiishi kama familia moja na walikuwa na ushirikiano mkubwa baina ya familia zao.
Ridhiwani alisema kuwa kifo hicho ni pigo kwa familia hiyo pia kwa Taifa kwani alikuwa ni mtumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na alikuwa mtaalamu wa rada hivyo pengo lake haliwezi kuzibika kikubwa ni kumwombea marehemu.
Kufuatia msiba huo Rais Dk Jakaya Kikwete alituma salamu za pole kwa familia hiyo kupitia kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete na kusema kuwa anatoa pole na Mungu awape nguvu katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo na yuko pamoja nao.
Alisema kuwa Rais alishindwa kuhudhuria msiba huo kwani kwa sasa yuko nje ya nchi lakini pindi atakaporudi ataitembelea familia hiyo kwa ajili ya kuifariji kufuatia kifo cha mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa kabila wafugaji
Naye mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mathayo Torongei alisema ili amani iendelee kuwepo ni vema dola ikatenda haki badala ya kupendelea upande mmoja.
Marehemu alifariki kwa ajali baada ya gari alilokuwa akiendesha kupasuka tairi la mbele na kusababisha ajali iliyopelekea kifo chake siku ya Septemba 16 mwaka huu  huko Mtwara ameacha mke na watoto watatu.
Mwisho. 







Mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete kulia akifurahia jambo na mkuu wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Pololet Mgema wakati wa mazishi ya Karokya Moreto (33) mtoto wa alikuwa kiongozi wa wafugaji Laban Moreto huko Kijiji cha Maviyangombe kata ya Lugoba. 

 Baadhi ya Wazee wakiwa wamekaa kwenye msiba huo huko kijiji cha Maviyangombe Lugoba wilayani Bagamoyo. 

Kulia ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Morogoro  Jacob mameo Ole Paulo akiwa na mgombea Ubunge jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete. 

Kulia Ridhiwani Kikwete mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM akifuatiwa na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, mkuu wa wilaya ya Nachingwea Pololet Mgema na mgombea ubunge Jimbo hilo kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Matayo Torongei wakiwa kwenye msiba huo. 

 Askofu Jacob Mameo Ole Paulo akizungumza wakati wa msiba huo. 

Baadhi ya ndugu wa wakilia kuomboleza kifo cha ndugu yao. 

 baadhi ya ndugu wa wakilia kuomboleza kifo cha ndugu yao.

Akinamama ndugu wa karibu wa marehemu wakilia kuomboleza kifo hicho. 

Baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ wakiwa wamebeba jeneza lilokuwa na mwili wa marehemu kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi. 

Baadhi ya waombolezaji wakiaga mwili wa marehemu kabla ya mazishi  

Sehemu ya waombolezaji wa msiba huo. 

Sunday, September 13, 2015

MBUNGE KUTOA M 700 KUSAIDIA WAJASIRIAMALI

Na John Gagarini, Kibaha
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Silvestry Koka ameunga mkono mpango wa kukipatia kila kijiji hapa nchini shilingi milioni 50 za uwezeshaji wajasiriamali kwa kuahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 700 kwa Jimbo hilo kwenye mpango huo.
Alitoa ahadi hiyo  wakati wa uzinduzi wa kampeni kwenye Jimbo hilo zilizofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja Kibaha mbele ya Mgombea Mwenza wa CCM Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi na kusema kuwa mpango huo ni mzuri na unapaswa kuungwa mkono na wadau wa maendeleo.
Koka ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo anatetea kiti chake alisema kuwa tangu achaguliwe amekuwa akiwawezesha wajasiriamali wa Jimbo lote la Kibaha kwa kuwapatia fedha za kuwezesha vikundi vyao pamoja na mafunzo.
“Nimefurahishwa na mapango huo ambao ndiyo ilikuwa ajenda yangu ya kutaka wajasirimali waweze kuendeleza shughuli zao hivyo naipongeza serikali kwa kuona kuwa kuna haja ya kutoa fedha kwa ajili kuongeza pato la wananchi,” alisema Koka.
Alisema kuwa katika muda wake wa Ubunge miaka mitano iliyopita alitoa zaidi ya shilingi zaidi ya milioni 500 kwa wajasiriamali pamoja na kuwapatia elimu ya ujasirimali kupitia vikundi alivyohamasisha kuanzishwa.
“Nitatoa fedha hizo kwa kuiunga mkono serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo la Kibaha Mjini ambao wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao,” alisema Koka.
Naye Mgombea Mwenza Samia Suluhu alisema kuwa mpango huo utawezesha wajasiriamali kukuza mitaji yao na  serikali itasimamia ipasavyo fedha hizo ili zisiweze kutumika vibaya ili ziweze kuleta manufaa kwa wananchi.
Samia alisema kuwa wenyeviti wa Vijiji ambao watazinyemelea fedha hizo kwa manufaa yao binafsi wajiandae kwani wale watakaozitumia kinyume cha taratibu watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwashtaki. Pia fedha kwa akinamama na vijana asilimia 10 kwenye halmashauri atasimamia na kuhakikisha zinatolewa kama taratibu zinavyoonyesha.

Mwisho.  

Sunday, September 6, 2015

BAKWATA WAASA UCHAGUZI MKUU

Na John Gagarini, Kibaha
KAIMU Mufti Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Abubakari Zuberi amesema kuwa wanasiasa wanaokosa nafasi za uongozi wasiwe chanzo cha kuvunja amani ya nchi katika kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa maombi maalumu ya kuombea amani ya nchi yailiyoandaliwa na BAKWATA mkoa wa Pwani na kuwashirikisha viongozi na waumini wa kiislamu wa mkoa huo pamoja na waumini wa dini mbalimbali.
Mufti Zuberi alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi walioshindwa na watakaoshindwa kwenye kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa wanaonesha viashiria vya kutaka kuvunja amani iliyopo kutokana na kutokubali kushindwa.
“Kwa sasa tunaona viashiria mbalimbali vya kutaka kuvunja amani ya nchi     kutoka kwa baadhi ya wanasiasa hapa nchini na kutokana na hali hiyo tumeona ni vema tukafanya maombi haya kwa ajili ya kumwomba Mungu atunusuru na hali hiyo ili isije ikajitokeza,” alisema Mufti Zuberi.
Alisema kuwa Tanzania ni kama chumvi ya amani ambayo ikitumika vizuri itaongeza ladha lakini ikitumika vibaya itaharibu kila kitu hivyo ni vema Watanzania wakaendelea kuilinda amani iliyopo kwa sasa kwani baadhi ya majirani zetu wameathiriwa na vita na wanakimbilia kwetu.
“Tumwombe Mungu aendelee kutudumishia amani iliyopo kwa muda mrefu na tusikubali kuivunja amani yetu kwa tama ya baadhi ya watu wenye uroho wa madaraka kwani endapo amani itavunjika tutakuwa hatuna pa kukimbilia kwani majirani zetu wanakuja kwetu je sisi tutaenda wapi endapo amani itatoweka,” alisema Mufti Zuberi.
Kwa  upande wake mkuu wa Wilaya ya Kibaha Halima Kihemba ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani alisema kuwa tayari serikali imeweka mazingira ya uchaguzi kufanyika kwa njia ya amani na utulivu.
Kihemba alisema kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuhakikisha amani inaendelea kudumu na kuwataka wawaelekeze waumini wao kufuta taratibu zilizopangwa katika kushiriki uchaguzi na wale wote waliojiandikisha watapiga kura na watakaokwenda kinyume cha sheria hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Naye Kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Abbas Mtupa alisema kuwa tayari wametoa maagizo kwa Maimamu na Masheikh wa misikiti yote kufanya maombi maalumu kila Ijumaa kuiombea amani ya nchi ili uchaguzi uwe wa amani.
Mtupa alisema kuwa maombi hayo maalumu ya kumwomba Mungu kwa wale wenye nia mbaya ya kuleta vurugu washindwe na maombi hayo yatakuwa endelevu hadi uchaguzi mkuu utakapoisha ili hali ya amani iendelee kudumu.
Mwisho.

  

     
 









Picha 1914 Kadhi wa mkoa wa Pwani Abbas Mtupa akizungumza kwenye maombi maalumu kuliombea taifa amani lilofanyika kwenye viwanja vya Bwawani Maili Moja Kibaha.

1918 Baadhi ya wakinamama waliohudhuria maombi maalumu ya kuliombea Taifa kuwa na amani katika uchaguzi mkuu wakiewasikiliza viongozi wao
1922 Mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba akihutubia kwenye maombi maalumu ya kuombea amani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
1923 Sheikh Mtonda akiongea kwenye maombi maalumu kuliombea Taifa kuwa na amani kwenye kipindi cha uchaguzi.
1925 Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Pwani Said Lipambila akiwahutubia waumini wa Kiislamu waliohudhuria maombi maalumu kuiombea nchi kuwa na amani kipindi cha uchaguzi
1933 Kaimu Mufti mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Abubakari Zuberi akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria maombi maalumu kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani Kibaha
1936 Baadhi ya wamini wa dini ya Kiislamu wakiwasikiliza viongozi wao wakati wa maombi ya kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani maili Moja Kibaha
1940 baadhi ya waumini wakisikiliza viongozi wao wakati wa maombi maalumu ya kuliombea Taifa
1947 Kaimu Mufti Mkuu Abubakari Zuberi kulia akizungumza na Kadhi wa mkoa wa Pwani Abbas Mtupa wakati wa maombi maalumu ya kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja Kibaha


Wednesday, September 2, 2015

WATAKA MABADILIKO YA SHERIA ZA MIRATHI

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI kupitia vyombo vya kutunga sheria likiwemo Bunge vimetakiwa kubadilisha sheria za mirathi ili wanawake na watoto waweze kupata haki zao mara baba anapofariki dunia.
Hayo yalisemwa na baadhi ya madaktari na wauguzi wa Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, wakati wa mafunzo juu ya kukabiliana na kansa ya kizazi na matiti pamoja na unyanyasaji wa jinsia mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Wanawake Tanzania.
Moja ya washiriki wa mafunzo hayo Mganga wa Kituo cha Afya Mlandizi  Amilen Sam alisema kuwa familia nyingi mara baba anapofariki dunia wanawake wamekuwa hawapati mali yoyote licha ya kuwa wao walihusika katika upatikanaji wa mali hizo.
“Kutokana na sheria  nyingi za mirathi kupitwa na wakati vyombo vya kutunga sheria likiwemo Bunge lazima zibadili sheria hizo ambazo hazimpi nafasi ya kurithi mali ambazo mama kahusika kuzichuma na marehemu mume wake,” alisema Dk Sam.
Kwa upande wake Dk Pascalina Kamba wa Kituo cha Afya Disunyala alisema kuwa baadhi ya mila na desturi nazo ni chanzo cha tatizo hilo kutokana na kutoruhusu mwanamke kuongea lolote juu ya mali walizochuma na mume.
Dk Kamba alisema kutokana na sheria hizo kutungwa miaka ya nyuma ni dhahiri zimepitwa na wakati na hazipaswi kuendelezwa ili mwanamke na mtoto waweze kupata haki zao ikiwa ni matunda ya ndoa na si kuwanufaisha ndugu wa mume ambao hawajui mali hizo zimepatikana vipi.
Kwa upande wake mratibu kutoka mtandao huo wa maendeleo kwa wanawake Tanzania Gaudence Msuaya alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa nafasi walengwa kujadili unyanyasaji uliopo ndani ya jamii pia kuchukua hatua mara waonapo dalili mbaya zinazohusiana na magonjwa ya Kansa ya matiti na shingo ya uzazi.
Msuya alisema kuwa lengo lingine ni kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi hao ili watoe elimu hiyo kwa jamii pamoja na wteja wao wagonjwa ambao wanawapatia huduma ya matibabu kwenye maeneo yao ya kazi.
Mwisho.
  

SHULE YAFUNGWA BAADA YA MWANAFUNZI KUFA KWA KIPINDUPINDU

Na John Gagarini, Kibaha

KUFUATIA kifo cha mwanafunzi wa wa darasa la tatu Shule ya Msingi Maendeleo wilayani Kibaha mkoani Pwani kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu serikali imeifunga shule hiyo kwa muda usiofahamika ili kuwanusuru wanafunzi na ugonjwa huo.

Aidha imepiga marufuku mikusanyiko yote sherehe, misiba, minada ya hadhara na wafanyabiashara ndogondogo wa vyakula kuuza biashara mashuleni, biashara za matunda na vyakula kwenye maeneo ya wazi ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.

Akitoa ufafanuzi juu ya ugonjwa huo kuthibitika kuingia katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na mkoa wa Pwani mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa mwanafunzi mwingine anaugua ugonjwa huo hali iliyosababisha serikali wilayani Kibaha kuifunga shule hiyo kwa muda ili kuchukua tahadhari na kuhofia ugonjwa huo usienee kwa wengine.

“Tunasikitika kutokana na kifo cha mwanafunzi huyo na tumeona ili kunusuru wanafunzi wengine kuambukizwa tumeifunga shule hiyo na kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula kwenye maeneo ya wazi ikiwemo stendi ya Maili Moja ambapo biashara ya chakula hufanyika nyakati za usiku,” alisema Kihemba.

Kihemba alisema kuwa waliamua kuchukua hatua hizo za dharura ili kupunguza kuenea ugonjwa huo ambao na wafanyabiashara waache tabia ya baadhi ya wananchi ya kutiririsha maji machafu kwenye mitaro na mifereji ya barabarani.

“Nawaomba wananchi kuzingatia maagizo hayo na kuzingatia kanuni za usafi ili kuepuka ugonjwa huo ambao endapo hatua za haraka hazijachukuliwa husababisha kifo,” alisema Kihemba.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya hiyo amekemea vitendo cha baadhi ya wananchi kwenda kupatiwa matibabu kwenye hospitali za mitaani hali inayosababisha kushindwa kupona ama kugundulika kwa ugonjwa huo hatimaye kusababisha vifo.

“Kwa sasa tayari tumeshachukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuagiza madawa ya kutokomeza ugonjwa huo wa kipindupindu katika mamlaka husika na wanafunzi wa shule ya msingi maendeleo wamepatiwa dawa wote na wanafunzi wote wa shule hiyo wamepatiwa dawa,” alisema Kihemba.

Aidha alisema Idara ya afya mkoani humo imetenga maeneo ya kuwalaza baadhi ya wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo kwa ajili ya kuwapatia vipimo maalumu na kuwaanzishia  tiba mahususi ya ugonjwa huo.
  
“Kuanzia tarehe 24 Agosti mwaka huu wilaya ya Kibaha imepokea wagonjwa wenye dalili za ugonjwa wa kipindupindu wapatao 11 katika kituo cha afya Mlandizi na Mkoani, ambapo wawili kati yao waligundulika kuwa na ugonjwa huo na mmoja ambae ni mwanafunzi alifariki dunia kabla ya matibabu.

Alibainisha kuwa wagonjwa waliopokelewa walikuwa ni kutoka maeneo ya Maili Moja, Muheza, Tangini na Makuruge wilaya ya Kisarawe, Msigani na Mpiji Majohe wilaya ya Kinondoni, Visiga na Magindu Kibaha vijiji , Ruvu Darajani Bagamoyo ambapo kati yao watatu ndio waliogundulika kuwa na ugonjwa huo baada ya kufanyiwa vipimo .

Mwisho