Na John Gagarini, Kibaha
KAIMU Mufti Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
Abubakari Zuberi amesema kuwa wanasiasa wanaokosa nafasi za uongozi wasiwe
chanzo cha kuvunja amani ya nchi katika kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa maombi maalumu ya
kuombea amani ya nchi yailiyoandaliwa na BAKWATA mkoa wa Pwani na
kuwashirikisha viongozi na waumini wa kiislamu wa mkoa huo pamoja na waumini wa
dini mbalimbali.
Mufti Zuberi alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi
walioshindwa na watakaoshindwa kwenye kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa
wanaonesha viashiria vya kutaka kuvunja amani iliyopo kutokana na kutokubali
kushindwa.
“Kwa sasa tunaona viashiria mbalimbali vya kutaka kuvunja
amani ya nchi kutoka kwa baadhi ya wanasiasa hapa nchini
na kutokana na hali hiyo tumeona ni vema tukafanya maombi haya kwa ajili ya
kumwomba Mungu atunusuru na hali hiyo ili isije ikajitokeza,” alisema Mufti
Zuberi.
Alisema kuwa Tanzania ni kama chumvi ya amani ambayo
ikitumika vizuri itaongeza ladha lakini ikitumika vibaya itaharibu kila kitu hivyo
ni vema Watanzania wakaendelea kuilinda amani iliyopo kwa sasa kwani baadhi ya
majirani zetu wameathiriwa na vita na wanakimbilia kwetu.
“Tumwombe Mungu aendelee kutudumishia amani iliyopo kwa muda
mrefu na tusikubali kuivunja amani yetu kwa tama ya baadhi ya watu wenye uroho
wa madaraka kwani endapo amani itavunjika tutakuwa hatuna pa kukimbilia kwani
majirani zetu wanakuja kwetu je sisi tutaenda wapi endapo amani itatoweka,”
alisema Mufti Zuberi.
Kwa upande wake mkuu
wa Wilaya ya Kibaha Halima Kihemba ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani alisema
kuwa tayari serikali imeweka mazingira ya uchaguzi kufanyika kwa njia ya amani
na utulivu.
Kihemba alisema kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuhakikisha
amani inaendelea kudumu na kuwataka wawaelekeze waumini wao kufuta taratibu
zilizopangwa katika kushiriki uchaguzi na wale wote waliojiandikisha watapiga
kura na watakaokwenda kinyume cha sheria hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Naye Kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Abbas Mtupa alisema kuwa tayari
wametoa maagizo kwa Maimamu na Masheikh wa misikiti yote kufanya maombi maalumu
kila Ijumaa kuiombea amani ya nchi ili uchaguzi uwe wa amani.
Mtupa alisema kuwa maombi hayo maalumu ya kumwomba Mungu kwa
wale wenye nia mbaya ya kuleta vurugu washindwe na maombi hayo yatakuwa endelevu
hadi uchaguzi mkuu utakapoisha ili hali ya amani iendelee kudumu.
Mwisho.
1918 Baadhi
ya wakinamama waliohudhuria maombi maalumu ya kuliombea Taifa kuwa na amani
katika uchaguzi mkuu wakiewasikiliza viongozi wao
1922 Mkuu wa
wilaya ya Kibaha Halima Kihemba akihutubia kwenye maombi maalumu ya kuombea
amani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
1923 Sheikh
Mtonda akiongea kwenye maombi maalumu kuliombea Taifa kuwa na amani kwenye
kipindi cha uchaguzi.
1925 Sheikh
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Said Lipambila akiwahutubia waumini wa Kiislamu
waliohudhuria maombi maalumu kuiombea nchi kuwa na amani kipindi cha uchaguzi
1933 Kaimu
Mufti mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Abubakari Zuberi
akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria maombi maalumu kuliombea
Taifa kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja wilayani Kibaha
1936 Baadhi
ya wamini wa dini ya Kiislamu wakiwasikiliza viongozi wao wakati wa maombi ya
kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani maili Moja Kibaha
1940 baadhi
ya waumini wakisikiliza viongozi wao wakati wa maombi maalumu ya kuliombea
Taifa
1947 Kaimu
Mufti Mkuu Abubakari Zuberi kulia akizungumza na Kadhi wa mkoa wa Pwani Abbas
Mtupa wakati wa maombi maalumu ya kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Bwawani
Maili Moja Kibaha
No comments:
Post a Comment