Na John Gagarini, Mafinga
HOSPITALI ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa inahitaji kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa vya upasuaji kwenye wodi ya wazazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Mafinga Dk Innocent Mhagama alisema kuwa fedha hizo ni pamoja na ukarabati wa chumba cha upasuaji kwenye wodi hiyo.
Dk Mhagama alisema kuwa jengo hilo la wodi ya wazazi limekamilika na linatumika lakini halina huduma ya upasuaji kwa wanawake wajawazito.
Alisema kuwa wanafanya mipango mbalimbali kwa ajili ya kupata fedha hizo ili kutoa huduma bora za idi ya hapo kwani matatizo yote yatakuwa yakitatuliwa ndani ya jengo hilo pasipo kumhamisha mgonjwa.
“Wodi hii iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 320 imekamilika tangu mwaka jana na inatoa huduma zote isipokuwa upasuaji ambapo kwa sasa tunatafuta fedha hizo ili kuwe na huduma hiyo,” alisema Dk Mhagama.
Alisema kuwa kukamilika kwa wodi hiyo kumepunguza tatizo la akinamama kutopata huduma bora lakini sasa huduma zimeboreka.
“Wodi ya awali ilikuwa na uwezo wa kuzalisha akinamama wawili au watatu lakini kwa sasa wanazalisha akinamama nane kwa wakati mmoja ambapo inauwezo wa kulaza akinamama 60 toka 20 kwa wakati mmoja ambapo wanaojifungua kwa siku ni kati ya 18 na 20 na wanaofanyiwa operesheni kwa siku ni kati ya wanne hadi sita,” alisema Dk Mhagama.
Moja akinamama wanaotumia wodi hiyo Blandina Mpyanga alisem akuwa wanaishukuru serikali na wadau mbalimbali waliofanikisha ujenzi huo.
Mpyanga alisema kuwa kwa kipindi cha nyuma wakinamama wajawazito walikuwa wakilala wanne kwenye kitanda kimoja lakini kwa sasa kila mgonjwa na kitanda chake.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
KATIKA kukabiliana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi wa kike kupata ujauzito pamoja na kuozwa katika umri mdogo Jimbo la Mufindi Kaskazini wilayani Mufindi mkoani Iringa imewekwa mikakati ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi kwa shule za sekondari.
Akizungumza na waandishi wa habari mbunge wa Jimbo hilo ambaye anatetea kiti hicho Mahmoud Mgimwa alisema kuwa ujenzi huo ni kwa ajili ya shule zote za kata na zingine ili kukabiliana na changamoto hizo.
Mgimwa ambaye ni Naibu waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa hadi sasa shule ya sekondari ya Isalavanu tayari imekamilika huku ile ya Kibengu ikiwa ujenzi unaendelea.
“Hii ni moja ya mikakati ambayo nimeiweka kama kipaumbele cha utekelezaji wa ilani ya chama ambapo nimechangia hosteli hizo bati 170 na vifaa mbalimbali katika kukamilisha ujenzi huo,” alisema Mgimwa.
Alisema kuwa endapo kila kata itakuwa na hosteli ni dhahiri tatizo la mimba na wanafunzi kuozwa wakiwa bado wanafunzi litapungua au kwisha kabisa.
“Unajua wanafunzi wa kike wanachangamoto kubwa kwani baadhi ya watu wamekuwa wakiwarubuni kutokana na mazingira wanayoishi hasa kutokana na umbali wa shule wanazosoma lakini wakijengewa mabweni itawasaidia,” alisema Mgimwa.
Mmoja ya wakazi wa Mji wa Mfainga Anna Karoli alisema kuwa mpango huo ni mzuri na utasaidia kuwanusuru wanafunzi wanaopewa mimba na kuozwa.
Karoli alisema wanafunzi wa kike wakikaa shule itawasaidia kujiepusha na vishawishi mbalimbali mara watokapo au kwenda shule.
Moja ya wanafunzi wa kike Anita Michael ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya JJ Mungai alisema kuwa mpango huo ni mzuri na utawasadia wanafunzi wa kike kukabiliana na changamoto hizo.
Anita alisema kuwa baadhi ya changamoto wanazozipata ni kurubuniwa na baadhi ya watu wakiwemo madereva wa bodaboda ambao wamekuwa wakiwadanganya kwa kuwapa lifti wakati wakwenda shule.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
WATUMISHI wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kuacha kujihusisha na mambo ya siasa ili kutozorotesha utoaji huduma kwenye sehemu zao za kazi.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shaib Nnunduma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Mafinga na kusema kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Nnunduma alisema kuwa kama mtumishi anataka kujihusisha na sisa kuna taratibu ambazo anatakiwa afuate lakini si kufanya siasa akiwa kazini.
“Kufanya siasa ofisini ni kosa kisheria na mtumishi ambaye anafanya hivyo ni kinyume cha sheria za kazi hivyo hawapaswi kufanya hivyo kwani ni kukwamisha utendaji kazi,” alisema Nnunduma.
Alisema kuwa endapo mtumishi anabainika kujihusisha na siasa kazini sheria inambana na anaweza kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
“Kila mtu kuna chama anachokipenda lakini huwezi kuonyesha itikadi zako za chama ofisini kwani kuna baadhi ya watu utawabagua kutokana na vyama vyao hivyo hilo ni kosa kisheria,” alisema Nnunduma.
Aidha alisema kuwa ataandaa mkutano na watumishi wote wa Halmashauri ili kuwajulisha kujiepusha na siasa kazini ambapo wakuu wa shule za sekondari alishaongea nao juu ya kujiepusha na siasa shuleni.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment