Na John Gagarini, Mafinga
KUTOKANA na Utekelezaji wa Ilani kikamilifu chama cha mapinduzi kinatarajia kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao kwenye nafasi zote za Urais Ubunge na Udiwani
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kimeweka mikakati ya kupata ushindi wa kishindo kwa wagombea wake kwenye nafasi tatu za Urais Wabunge na Madiwani kutokana na utekelezaji wa ilani ya chama.
Hayo yalisemwa na mjini Mafinga na katibu wa CCM wilaya ya Mfundi Jimson Mhagama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa ushindi wa chama unatokana na ilani kutekelezwa kwa asilimia 95.
Mhagama alisema kuwa wilaya hiyo ina majimbo matatu ya Mufindi Kaskazini ambalo linaongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmoud Mgimwa, Mufindi Kusini linaongozwa na Menrad Kigora na Mafinga Mjini litakalowaniwa na Cosatu Chumi pamoja na kata 36 vyote vikiwa chini ya CCM hivyo wana uhakika wa kuendelea kuyaongoza maeneo hayo.
“Sisi hatuna wasiwasi tunaendelea kuweka mikakati ya suhindi lakini ushindi wetu utatokana na utekelezaji wa ilani ya chama juu ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali za huduma za jamii ambazo zimeboreka kutokana na uongozi mzuri wa viongozi wa chama,” alisema Mhagama.
Alisema kuwa mfano kwenye huduma za jamii ujenzi wa baadhi ya barabara kwa kiwango cha lami na changarawe zinazofanya kupitika kwa kipindi chote cha mwaka, uboreshaji wa huduma za afya kwenye Hospitali ya Mafinga na ujenzi wa zahanati kwenye vijiji, uanzishwaji wa vikundi vya ujasiriamali, huduma za taasisi za fedha na ujenzi wa shule za sekondari, uanzishwaji wa vyuo mbalimbali.
Aidha alisema kuwa CCM itaendelea kusimamia ilani yake kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanapatikana ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ambao wamekiamini chama kutokana na kuongoza kwa manufaa ya jamii.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mafinga
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa amemwagia sifa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmoud Mgimwa kutokana na uchapakazi wake kwenye wizara pamoja na kuhamasisha maendeleo kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini analoliongoza.
Akihutubia wakazi wa mji wa Mafinga wakati wa mkutano wake wa kampeni Lowassa alisema kuwa mbunge huyo ni mchapakazi na amefanya mabadiliko makubwa kwenye Jimbo hilo na kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii.
Lowassa alisema kuwa Mgimwa ni moja ya viongozi wazuri ambao wanawajibika vizuri katika maeneo ambayo wamepewa kuwajibika lakini angekuwa kwenye chama kama CHADEMA angefanya vizuri zaidi.
“Mgimwa namfahamu ni muwajibikaji mzuri katika maeneo ambayo anayaongoza lakini angekuwa upinzani angefanya vizuri zaidi kwani wapinzani wanafanya kazi sana na wana uwezo wa kuleta maendeleo,” alisema Lowassa.
Kwa upande wake katibu wa CCM wilaya ya Mufindi Jimson Mhagama akizungumzia juu ya kauli ya Lowassa alisema kuwa Mgimwa ni zao la CCM ambalo limeandaliwa kwani ndiyo kazi yao kutengeneza viongozi bora.
Mhagama alisema kuwa kiongozi bora anatoka CCM na kazi ya wapinzani ni kuchukua watu ambao uwezo wao umeshakuwa mdogo hivyo kushindwa kuwajibika hali ambayo haitawaletea maendeleo wananchi.
Aliwataka wananchi kuiunga mkono CCM na kuachana na vyama vya upinzani ambavyo havina sera za kuwaletea maendeleo wananchi badala yake ni kuwagawa na kuendeleza malumbano ambayo hayana faida kwa wananchi.
Naye mkazi wa Mafinga Edina Peter alisema kuwa wao wanataka kiongozi ambaye atawasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi na Mgimwa ni moja ya viongozi bora ambao wanajali maslahi ya wananchi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment