Na John Gagarini, Kibaha
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibaha
Mjini mkoani Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Silvestry Koka ameunga
mkono mpango wa kukipatia kila kijiji hapa nchini shilingi milioni 50 za
uwezeshaji wajasiriamali kwa kuahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 700 kwa
Jimbo hilo kwenye mpango huo.
Alitoa ahadi hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni kwenye Jimbo
hilo zilizofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja Kibaha mbele ya Mgombea
Mwenza wa CCM Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi na kusema kuwa mpango
huo ni mzuri na unapaswa kuungwa mkono na wadau wa maendeleo.
Koka ambaye alikuwa Mbunge wa
Jimbo hilo anatetea kiti chake alisema kuwa tangu achaguliwe amekuwa
akiwawezesha wajasiriamali wa Jimbo lote la Kibaha kwa kuwapatia fedha za
kuwezesha vikundi vyao pamoja na mafunzo.
“Nimefurahishwa na mapango huo
ambao ndiyo ilikuwa ajenda yangu ya kutaka wajasirimali waweze kuendeleza
shughuli zao hivyo naipongeza serikali kwa kuona kuwa kuna haja ya kutoa fedha
kwa ajili kuongeza pato la wananchi,” alisema Koka.
Alisema kuwa katika muda wake wa
Ubunge miaka mitano iliyopita alitoa zaidi ya shilingi zaidi ya milioni 500 kwa
wajasiriamali pamoja na kuwapatia elimu ya ujasirimali kupitia vikundi
alivyohamasisha kuanzishwa.
“Nitatoa fedha hizo kwa kuiunga
mkono serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo la Kibaha Mjini ambao
wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kuendeshea
shughuli zao,” alisema Koka.
Naye Mgombea Mwenza Samia Suluhu
alisema kuwa mpango huo utawezesha wajasiriamali kukuza mitaji yao na serikali itasimamia ipasavyo fedha hizo ili
zisiweze kutumika vibaya ili ziweze kuleta manufaa kwa wananchi.
Samia alisema kuwa wenyeviti wa
Vijiji ambao watazinyemelea fedha hizo kwa manufaa yao binafsi wajiandae kwani
wale watakaozitumia kinyume cha taratibu watachukuliwa hatua kali ikiwa ni
pamoja na kuwashtaki. Pia fedha kwa akinamama na vijana asilimia 10 kwenye
halmashauri atasimamia na kuhakikisha zinatolewa kama taratibu zinavyoonyesha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment