Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA kifo cha mwanafunzi wa wa darasa la tatu Shule ya Msingi Maendeleo wilayani Kibaha mkoani Pwani kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu serikali imeifunga shule hiyo kwa muda usiofahamika ili kuwanusuru wanafunzi na ugonjwa huo.
Aidha imepiga marufuku mikusanyiko yote sherehe, misiba, minada ya hadhara na wafanyabiashara ndogondogo wa vyakula kuuza biashara mashuleni, biashara za matunda na vyakula kwenye maeneo ya wazi ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.
Akitoa ufafanuzi juu ya ugonjwa huo kuthibitika kuingia katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na mkoa wa Pwani mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa mwanafunzi mwingine anaugua ugonjwa huo hali iliyosababisha serikali wilayani Kibaha kuifunga shule hiyo kwa muda ili kuchukua tahadhari na kuhofia ugonjwa huo usienee kwa wengine.
“Tunasikitika kutokana na kifo cha mwanafunzi huyo na tumeona ili kunusuru wanafunzi wengine kuambukizwa tumeifunga shule hiyo na kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula kwenye maeneo ya wazi ikiwemo stendi ya Maili Moja ambapo biashara ya chakula hufanyika nyakati za usiku,” alisema Kihemba.
Kihemba alisema kuwa waliamua kuchukua hatua hizo za dharura ili kupunguza kuenea ugonjwa huo ambao na wafanyabiashara waache tabia ya baadhi ya wananchi ya kutiririsha maji machafu kwenye mitaro na mifereji ya barabarani.
“Nawaomba wananchi kuzingatia maagizo hayo na kuzingatia kanuni za usafi ili kuepuka ugonjwa huo ambao endapo hatua za haraka hazijachukuliwa husababisha kifo,” alisema Kihemba.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya hiyo amekemea vitendo cha baadhi ya wananchi kwenda kupatiwa matibabu kwenye hospitali za mitaani hali inayosababisha kushindwa kupona ama kugundulika kwa ugonjwa huo hatimaye kusababisha vifo.
“Kwa sasa tayari tumeshachukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuagiza madawa ya kutokomeza ugonjwa huo wa kipindupindu katika mamlaka husika na wanafunzi wa shule ya msingi maendeleo wamepatiwa dawa wote na wanafunzi wote wa shule hiyo wamepatiwa dawa,” alisema Kihemba.
Aidha alisema Idara ya afya mkoani humo imetenga maeneo ya kuwalaza baadhi ya wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo kwa ajili ya kuwapatia vipimo maalumu na kuwaanzishia tiba mahususi ya ugonjwa huo.
“Kuanzia tarehe 24 Agosti mwaka huu wilaya ya Kibaha imepokea wagonjwa wenye dalili za ugonjwa wa kipindupindu wapatao 11 katika kituo cha afya Mlandizi na Mkoani, ambapo wawili kati yao waligundulika kuwa na ugonjwa huo na mmoja ambae ni mwanafunzi alifariki dunia kabla ya matibabu.
Alibainisha kuwa wagonjwa waliopokelewa walikuwa ni kutoka maeneo ya Maili Moja, Muheza, Tangini na Makuruge wilaya ya Kisarawe, Msigani na Mpiji Majohe wilaya ya Kinondoni, Visiga na Magindu Kibaha vijiji , Ruvu Darajani Bagamoyo ambapo kati yao watatu ndio waliogundulika kuwa na ugonjwa huo baada ya kufanyiwa vipimo .
Mwisho
No comments:
Post a Comment