Wednesday, September 2, 2015

WATAKA MABADILIKO YA SHERIA ZA MIRATHI

Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI kupitia vyombo vya kutunga sheria likiwemo Bunge vimetakiwa kubadilisha sheria za mirathi ili wanawake na watoto waweze kupata haki zao mara baba anapofariki dunia.
Hayo yalisemwa na baadhi ya madaktari na wauguzi wa Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, wakati wa mafunzo juu ya kukabiliana na kansa ya kizazi na matiti pamoja na unyanyasaji wa jinsia mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Wanawake Tanzania.
Moja ya washiriki wa mafunzo hayo Mganga wa Kituo cha Afya Mlandizi  Amilen Sam alisema kuwa familia nyingi mara baba anapofariki dunia wanawake wamekuwa hawapati mali yoyote licha ya kuwa wao walihusika katika upatikanaji wa mali hizo.
“Kutokana na sheria  nyingi za mirathi kupitwa na wakati vyombo vya kutunga sheria likiwemo Bunge lazima zibadili sheria hizo ambazo hazimpi nafasi ya kurithi mali ambazo mama kahusika kuzichuma na marehemu mume wake,” alisema Dk Sam.
Kwa upande wake Dk Pascalina Kamba wa Kituo cha Afya Disunyala alisema kuwa baadhi ya mila na desturi nazo ni chanzo cha tatizo hilo kutokana na kutoruhusu mwanamke kuongea lolote juu ya mali walizochuma na mume.
Dk Kamba alisema kutokana na sheria hizo kutungwa miaka ya nyuma ni dhahiri zimepitwa na wakati na hazipaswi kuendelezwa ili mwanamke na mtoto waweze kupata haki zao ikiwa ni matunda ya ndoa na si kuwanufaisha ndugu wa mume ambao hawajui mali hizo zimepatikana vipi.
Kwa upande wake mratibu kutoka mtandao huo wa maendeleo kwa wanawake Tanzania Gaudence Msuaya alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa nafasi walengwa kujadili unyanyasaji uliopo ndani ya jamii pia kuchukua hatua mara waonapo dalili mbaya zinazohusiana na magonjwa ya Kansa ya matiti na shingo ya uzazi.
Msuya alisema kuwa lengo lingine ni kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi hao ili watoe elimu hiyo kwa jamii pamoja na wteja wao wagonjwa ambao wanawapatia huduma ya matibabu kwenye maeneo yao ya kazi.
Mwisho.
  

No comments:

Post a Comment