Saturday, September 26, 2015

KAMPENI CHALINZE





Na John Gagarini, Chalinze
HALMASHAURI ya wilaya ya Bagamoyo imeshauriwa kuisitisha mikata ya umiliki wa ardhi iliyochukuliwa na wawawkezaji ambao hawajaiendeleza ardhi hiyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 wairejeshe kwenye serikali za vijiji kwa ajili ya matumizi ya umma.
Hayo yalisemwa na mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete wakati wa mikutano ya hadhara ya kampeni kwenye Vijiji vya Makombe na Kinzagu kwenye kata ya Lugoba na kusema kuwa wamiliki hao kama wameshindwa kuiendeleza ardhi hiyo ni vema wakairudisha kwa wananchi.
Ridhiwani alisema kuwa inashangaza kuona kuwa wananchi kwenye vijiji hivyo wamekuwa wakihangaika kutafuta ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja na matumizi mengine lakini wanakosa maeneo ambayo yamehodhiwa na watu wachache.
“Kwa sasa ni vema halmashauri zikasitisha mikata ya umiliki wa ardhi hiyo kutokana na kushindwa kuiendeleza kwa kipindi cha miaka zaidi yha 10 ambapo sheria inataka mwekezaji kuiendeleza ardhi ndani ya kipindi cha miezi 32 na endapo atashindwa kuiendeleza anaweza kufutiwa umiliki,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa haipendezi kuona wananchi wanahangaika kutafuta maeneo huku baadhi ya watu wakiwa wamehodhi maeneo bila ya kuyaendeleza na kuacha yakiwa mapori ambayo yanahatarisha usalama wao.
“Ni vema maeneo hayo yakarejeshwa kwenye serikali za vijiji ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo kwani itakuwa ni sehemu ya kutoa ajira kwa wananchi hususani vijana,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo ya Lugoba ambaye amepita bila ya kupingwa Rehema Mwene alisema kuwa ni kweli maeneo hayo yalichukuliwa na wawekezaji muda mrefu lakini hayajaendelezwa.
Mwene alisema wananchi wa maeneo hayo hususani vijana hawana ajira lakini endapo ardhi hiyo itarejeshwa itasadia kujiajiri kupitia kilimo ambacho ni ajira ya uhakika lakini wanashindwa kujiajiri kupitia kilimo kutokana na kukosa maeneo kwa ajili ya kulima.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wa Kijiji cha Makombe wameomba uwekwe utaratibu wa malori yanayobeba kokoto kutoka kwenye machimbo ya kokoto yapimwe uzito ili yabebe uzito kutokana na uwezo wa barabara.
Sambamba na hilo wameomba kuwe na utaratibu wa magari hayo kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara ambazo zimekuwa zikiharibika vibaya kutokana na kupitishwa malori hayo ambayo yana  uzito mkubwa.
Ombi hilo lilitolewa na Rehema John alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa kampeni wa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete.
John alisema kuwa barabara hizo zimeharibika vibaya kutokana na magari ya kubebea kokoto ambayo ni mazito na hakuna utaratibu wa kuyapima uzito hali inayosababisha barabara kuharibika.
“Tunaiomba serikali kuweka utaratibu mzuri wa malori hayo yanayobeba kokoto kutoka kwenye machimbo  na kusababisha uharibifu wa barabara inayoelekea kwenye machimbo hayo na kutoka huko kwenda barabara kubwa ya lami,” alisema John.
Alisema kuwa kwa sasa barabara hizo zinazoelekea kwenye machimbo hayo ya kokoto zimeharibika vbaya kutokana na uzito kuwa mkubwa hivyo kushindwa kuhimili uzito.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Lugoba ambaye amepita bila ya kupingwa Rehema Mwene alisema kuwa atahakikisha maombi hayo anayapeleka sehemu husika ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani uharibifu ni mkubwa sana.
Mwene alisema kuwa barabara zinazoelekea kwenye machimbo hayo zote ni mbaya kutokana na kutofanyiwa ukarabati ambapo licha ya halmashauri kuzifanyia matengenezo lakini zinaharibika haraka kutokana na uzito mkubwa wa malori hayo.
Kwa upande wake mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kuna haja ya wanaotumia barabara hizo hasa wale wenye magari yanayobeba kukoto pamoja na wawekezaji kwenye machimbo hayo kufanya ukarabati wa barabara hizo.
Ridhiwani alisema kuwa wawekezaji wanapaswa kuboresha huduma mbalimbali ndani ya kijiji ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji wao na hivyo ni vema wakazikarabati barabara hizo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wakiwemo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wilayani Bagamoyo hususani wanawake wametakiwa wasikubali kurubuniwa na baadhi ya watu na kuuza shahada zao kwa matapeli kwa madai ya kuipunguzia kura kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa CCM Ridhiwani Kikwete kwenye kijiji cha Lunga kata ya Lugoba wilayani humo katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mwatabu Husein alisema kuwa wapinzani wao wameanza kununua kadi za wapiga kura ili kukipunguzia kura.
Hussein alisema kuwa kuna watu wanapita na kuwarubuni wananchi na wanachama wa CCM ili wawauzie kadi za mpiga kura ili kupunguza idadi ya wapiga kura kwani endapo mtu atakuwa hana kadi ya mpiga kura hatakuwa na haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo.
“Nawashauri wananchi na wana CCM kuwa makini na watu hao kwani wamekuwa wakitumia njia hiyo ya kuzinunua kadi hizo ili kutuathiri kupata ushindi wa kishindo hivyo mnapaswa kuwa macho hasa wakinamama msikubali kuyumbishwa,” alisema Hussein.
Alisema kuwa tayari wamewashika pabaya wapinzani wao ambao sasa wamenza kuweweseka na kufanya vitendo vinavyoashiria kushindwa na kuanza kutapatapa.
“Wapinzani wetu hawatuwezi wamenza kununua kadi za wapiga kura ili kutupunguzia ushindi wa kishindo lakini tayari wameshachelewa tutawashinda kwa kishindo kikubwa na mwisho wao utakuwa Oktoba 25 mwaka huu,”a lisema Hussein.
Aidha alisema kuwa wapinzani hali yao imekuwa mbaya kwani hawana uwezo wa kuishinda CCM ambayo imejipanga vizuri kwa mikakati yake ya ushindi na washindani wao tayari wameshakubali kushindwa sasa wanatafuta sababu ya kushindwa hata kabla uchaguzi haujafanyika.
Mwisho.








No comments:

Post a Comment