Friday, October 2, 2015

MGOMBEA UDIWANI AHAIDI KUTOA ASILIMIA 50 YA POSHO KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MGOMBEA Udiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Kawawa Jimbo la Kibaha Vijijini Otto Kanyonyi amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo atatoa asilimia 50 ya posho zake atakazokuwa anapata kwenye vikao vya madiwani  kwa ajili ya kuchangia shughuli za maendeleo kwenye kata hiyo.
Kanyonyi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Mlandizi Kibaha juu ya mikakati yake ya kuwaletea maendeleo wakazi wa kata hiyo endapo atashinda kwenye nafasi ya udiwani kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema kuwa moja ya mkakati wake ambao ataupa kipaumbele ni ujenzi wa zahanati katika kata hiyo ili kuwapatia huduma wananchi badala ya kupata huduma hizo kwenye kata za jirani.
“Endapo nitafanikiwa kuwa diwnai wa kata yetu ya Kawawa nitahakikisha natoa asilimia 50 ya posho nitakayokuwa npata naitoa kwa ajili ya shughuli za maendeleo hasa zile huduma za jamii ikiwa ni pamoja na afya, elimu na maji,” alisema Kanyonyi.
Aidha alisema kuwa ameamua kujitolea posho hizo kutokana na kuwa na uchungu wa maendeleo na kuona kuwa moja ya njia za kuleta maendeleo ni kuchagia kwa hali na mali.
“Fedha hizo nataka zilete maendeleo katika kata yangu kwani ili kufanikisha mambo kiongozi lazima uonyeshe njia kwa wale unaowangoza hivyo na mimi nataka niwe kiongozi wa mfano ili niache kumbukumbu kuwa nilihamasisha maendeleo,” alisema Kanyonyi.
Alibainisha kuwa wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo moja ya njia za kuwahamasisha kujiletea maendeleo ni pamoja na kuchangia shughuli za maendeleo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani umetoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwenyekiti wa tawi la Ubena Zomozi Kido Antoni (65) kufariki dunia wakati wa mkutano wa kampeni wa diwani wa kata ya Ubena Jimbo la Chalinze.
Mwenyekiti huyo wa tawi alifariki Septemba 30 majira ya saa 7 mchana wakati wakiwa kwenye shamrashamra ya kuwahamasisha wananchi kujiandaa kwa kucheza huku wakimsubiri mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia CCM Nicholaus Muyuwa kwa ajili ya mkutano wa kampeni.
Akitoa salamu za pole katibu wa UWT wilaya ya Bagamoyo Mwatabu Hussein alisema kuwa wameupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa kwani marehemu alikuwa kwenye harakati za kukipigania chama wakati huu wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.
Hussein alisema kuwa familia pamoja na chama vimepata pigo kubwa la kuondokewa na kiongozi wao na kumwomba Mungu aipe nguvu katika kipindi hichi bkigumu cha majonzi.
“Tunawapa pole familia pamoja na chama kwa kuondokewa na mpendwa wao kwani alikuwa kwenye harakati za kuhakikisha chama kinapata ushindi kwenye uchaaguzi wa wagombea wa chama kuanzia Rais, Mbunge na Diwani,” alisema Hussein.
Kwa upande wake mgombea huyo wa udiwani Muyuwa alisema kuwa kifo amekipokea kwa masikitiko makubwa kwani marehemu alikuwa mtu muhimu sana ndani ya chama na amekufa wakati akipambana kuhakikisha ushindi unapatikana.
Muyuwa alisema kuwa marehemu alikuwa mzima kabisa na alikuwa kifurahi na wenzake na kutoa hamasa kwa wananchama  na wasio wanachama juu ya kukipigia kura ili kiweze kushinda kwenye uchaguzi m kuu ujao.
Alisema kuwa marehemu alianguka ghafla wakati wakimsubiri yeye aweze kufika kwa ajili ya kuhutubia kwenye mkutano wa kampeni na baada ya kuanguka walimpeleka kwenye zahanati ya Ubena Estate na alifariki wakatia kipatiwa matibabu.
Naye mgombea Ubunge kwenye Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alifika nyumbani kwa marehemu na kutoa salamu za pole kwani wakati tukio hilo linatokea mgombea huyo alikuwa kwenye mkutano wa kampeni katika kata hiyo kwenye Kijiji cha Mdaula.
Taarifa toka kwa daktari mfawidhi wa zahanati hiyo zilisema kuwa alikufa kutokana na presha na upungufu wa damu, marehemu alizikwa juzi kwenye makaburi ya Ubena na ameacha watoto watano.
Mwisho.
Na John Gagarini, Bagamoyo
MGOMBEA ubunge jimbo la Bagamoyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dk Shukuru Kawambwa, amesema endapo atachaguliwa kuongoza Jimbo hilo atahakikisha zahanati ya Yombo inapandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya ili kupanua huduma za kiafya.
Sambamba na kupandishwa hadhi kwa zahanati hiyo pia Dk Kawambwa  atahakikisha kunakuwa na gari la kubeba wagonjwa wanaopata rufaa kwenda hospitali kubwa  tofauti na ilivyo sasa.
Dk Kawambwa aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Yombo wakati wa mkutano wa kampeni na kusema kuwa vipaumbele vyake ni kuhakikisha huduma muhimu za jamii zinapatikana kwa uhakika.
“Mara zahanati hii ikipandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya huduma zitaboreka ikiwa ni pamoja na kuwa na wataalamu wa kutosha na huduma nyingi zitatolewa hapa hivyo itapunguza kutumia muda mwingi kufuata huduma mbali,” alisema Dk Kawambwa.
Aidha alisema kuwa pia kipaumbele kingine ni kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa ujenzi wa barabara kutoka Makofia-Yombo hadi Mlandizi-Mzenga kwa kiwango cha lami Dk ambapo kwa sasa upembuzi yakinifu umeshafanyika na kilichobakia ni tathmini ya watakaolipwa fidia ambako itapita barabara pamoja na hatua nyingine ili kupisha mpango huo.
“Utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo kuwa kwa kiwango cha lami upo katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 na ukamilikaji wake utafungua fursa nyingi za kiuchumi hivyo kuleta maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi,” alisema Dk Kawambwa.
Katika hatua nyingine alisema kuwa atahakikisha wakazi wa kata ya Yombo na maeneo ambayo hayajafikiwa umeme kuwa atashirikiana na tanesco kupitia mradi wa wakala wa umeme vijijini (REA) kuondoa tatizo hilo ndani ya miaka mitano ijayo.
"Nitahakikisha nasimamia mipango yote,na ilani ya chama changu ili niweze kupunguza makali ya kero zinazowakabili wana Bagamoyo ikiwemo kwenye afya,maji,nishati ya umeme ,elimu na miundombinu"alisema Dk.Kawambwa.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Yombo jimbo la Bagamoyo, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mohamed Usinga,aliwaahidi wakazi wanaoishi katika vijiji vinavyounda kata hiyo kuwa atahakikisha anamalizia kazi ya kusambaza maji, umeme na kituo cha afya kilichopo katani humo.
Alieleza kuwa pindi wakazi hao wakimpatia ridhaa ya kushika nafasi hiyo atapambana ili kumalizia kazi ambayo ilikuwa imeanzwa na mtangulizi wake Ubwa Idd Mazongera ambaye kwa sasa ametangulia mbele za haki.
Awali akiwanadi wagombea hao,meneja kampeni jimbo la Bagamoyo,AbdulSharif alisema wananchi jimboni hapo wasifanye makosa kuchagua wapinzani bali wawachague wagombea kupitia CCM.

Mwisho

No comments:

Post a Comment