Na John Gagarini, Chalinze
WAKAZI wa Kijiji cha Kwaruhombo Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo
wametoa kilio chao kwa kuomba viongozi watakaochaguliwa kwenye uchaguzi mkuu
kuwaondolea changamoto ya kutozwa kiasi cha shilingi 100,000 kwa ajili ya
mafuta ya kuweka kwenye gari la wagonjwa wanaopata rufaa toka kwenye kituo cha
afya cha Kwaruhombo.
Akizungumza Kijijini hapo mara baada ya mkutano wa kampeni wa
mgombea ubunge jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, Ally Rashid alisema kuwa hali hiyo
inawapa wakati mgumu kutokana na hali halisi ya kipato chao kidogo.
Rashid alisema kuwa changamoto hiyo ni kubwa kwani wao kupata
fedha hizo mzigo mkubwa ikizingatiwa maisha ya Kijijini ni magumu na hawana
vyanzo vikubwa vya mapato zaidi ya kilimo ambacho nacho kimekuwa si cha uhakika
kutokana na mvua kutokuwa za uhakika.
“Tunaomba viongozi watakaochaguliwa wahakikishe wanashughulikia
kero hii kwani kwa sasa ni muda mrefu na tumekuwa tukilalamika lakini hakuna
hatua zinazochukuliwa pia tunaomba Halmashauri itenge bajeti kwa ajili ya
mafuta ya gari hilo la wagonjwa,” alisema Rashid.
Naye mgombea Udiwani wa kata ya Kwaruhombo ramadhan mahamba
alisema kuwa kero hiyo ni kubwa kwa wanakijiji na kumwomba mgombea huyo wa
ubunge kuhakikisha nawasemea huko halmashauri ili gari hilo liwe na bajeti ya
mafuta.
Mahamba alisema kuwa mbali ya kero hiyo ya wananchi kutakiwa
kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuwekea mafuta ya kuwasafirisha
wagonjwa wanapopata rufaa kwenda hospitali kubwa pia kuna tatizo la upungufu wa
wahuduma wa afya.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kero hiyo
ameisikia na mara atakapochaguliwa atahakikisha anashinikiza kutenga fedha za
mafuta kwa ajili ya vituo vya afya ili kuwaondolea mzigo wananchi.
Ridhiwani alisema kuwa utaratibu umewekwa na Halmashauri wa
bajeti ya mafuta ya magari hayo hivyo akichaguliwa hiyo ni moja ya vitu
atakavyovifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha mafuta yanapatikana kwenye gari
hilo.
Mwisho.
NA John Gagarini, Chalinze
KIJIJI ch Kwaruhombo Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo
kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hali inayowafanya wakazi wake
kuchota maji ya visima vya kienyeji ambavyo viko chini ya ardhi huku vingine
vikiwa na urefu wa futi 12.
Mbali ya visima hivyo kuwa na urefu mkubwa ambapo huwabidi
wachotaji wengi wao wakiwa ni wakinamama kushuka kwa kutumia ngazi pia kumekuwa
na foleni kubw ahali ambayo inawafanya wakeshe wakisubiri maji ambayo yamekauka
kutokana na hali ya kiangazi.
Moja ya wanakijiji aliyejitambulisha kwa jina la Hadija
Yusufu alisema kuwa maji ni changamoto kubwa kwao kwani wamekuwa wakitumia muda
mrefu wa kusubiria maji hasa kipindi hichi cha kiangazi pia ni hatari kwa
maisha yao kutokana na urefu wa visima hivyo.
“Tunaiomba serikali kutusaidia kupatikana maji ili
kutuondolea adha hii kwani tumeletewa maji ambapo kuna vioski kwa ajili ya
kuchota maji lakini havitoi maji hatujui kuna tatizo gani linalosababisha maji
yasitoke hivyo tumebaki tunategemea maji ya visima hivyo vya kienyeji ambavyo
navyo ni hatari kweteu,” alisema Yusufu.
Kwa upande wake mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM Ramadhan
Mahamba alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anafuatilia suala hilo
ili maji yaweze kupatikana kwa kutatua changamoto iliyopo ili maji yapatikane
na kuwaondolea kero wananchi.
Naye mgombe ubunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete alisema
kuwa tatizo la ukosefu wa maji ni kutokana na miundombinu iliyowekwa kuwa ya
zamani hivyo kushindwa kuhimili kasi ya maji na kupasuka.
Ridhiwani alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha
miundombinu mipya ambayo ni mabomba inapatikana ili kuondoa kero hiyo
inayowanyima usingizi wananchi hao ambao hicho ni kilio chao kikubwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment