Wednesday, October 14, 2015

RIDHIWANI AMWAGIA SIFA DK MAGUFULI

Na John Gagarini, Chalinze
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John Magufuli amepongezwa kwa kuuachia mkoa wa Pwani hususani wilaya ya Bagamoyo miradi mikubwa ambayo itakapokamilika itasaidia kuinua kipato cha wakazi wa mkoa huo.
Miradi hiyo ambayo inatoka kwenye Wizara Ujenzi na Miundombinu aliyokuwa akioongoza Dk Magufuli kabla ya kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea Urais kwenye kinyanganyiro kitakachofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Pongezi hizo zimetolewa na mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia chama hicho Ridhiwani Kikwete, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Kijiji cha Miono wilayani Bagamoyo na kusema kuwa mgombea huyo kila mkoa ameupatia miradi ambayo itachochea maendeleo.
Ridhiwani alisema kuwa Dk Magufuli ni kiongozi ambaye anastahili kuongoza nchi hii kwani wakati akiwa waziri alihakikisha kila mkoa unatumia rasilimali zake viuzuri ili kujiletea maendeleo hali ambayo imesababisha nchi kupiga hatua.
“Sisi wakazi wa wilaya ya Bagamoyo tunamshukuru kwani ametuachia miradi mikubwa ikiwa ni pamoja na ule wa Barabara ya Afrika Mashariki itakayoanzia Bagamoyo,  Makuruge,  Saadani hadi mkoa wa Tanga hadi Mombasa nchini Kenya,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa mradi mwingine ni ule wa Bandari ambayo itakuwa ni kubwa ambao utaanza wakati wowote kuanzia sasa kwani mipango tayari imekamilika huku mradi wa barabara tatu zitakazoanzia Jijini Dar es Salaam hadi mkoani Morogoro pia mzaini wa kisasa uliopo Vigwaza ambao tayari unafanya kazi.
“Mradi mwingine ni ule wa upanuzi wa Daraja la Mto Wami ili kupunguza ajali zinazotokea kwenye daraja hilo ambapo kwa sasa magari hayawezi kupishana, hakika miradi hii ni mikubwa na itafungua fursa za maendeleo kwa kukuza uchumi wao kutumia fursa zilizopo na zitakazokuwepo kwenye miradi hiyo,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema Dk Magufuli ni kiongozi ambaye hana kashfa yoyote na ameonyesha kuwa anafaa kuliongoza Taifa la Tanzania kutokana na uchapa kazi wake pamoja na uadilifu aliokuwa nao ukilinganisha na viongozi wengine wanaowania nafasi hiyo.
Aliwataka watanzania kumchagua kwa kumpiga kura nyingi za kishindo ili awe Rais wa awamu ya tano na anaamini kuwa uwezo wa kuongoza nchi anao akiwa chini ya CCM ambao kwa wakati huu imechagua viongozi wenye sifa na wanaopendwa na wananchi.

Mwisho.
 Meneja kampeni wa Jimbo la Chalinze Alhaj Amiri Mkangata kushoto akimtambulisha mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Ridhiwani Kikwete kwenye Kijiji cha Kikwazu wilayani Bagamoyo

Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ridhiwani Kikwete akizindua  huku akiwa amekaa kwenye kigoda tawi la vijana wa Boda boda kwenye Kijiji cha Pongwemnazi 


Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ridhiwani Kikwete akizindua tawi kwa kupandisha bendera kwenye moja ya matawi wakati wa kampeni kuwania kiti hicho.

 Mgombea Udiwani kata ya Kimange kwa tiketi ya CCM Husein Hadingoka akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Kikwazu wakati wa mkutano wa kampeni

 Mama Mwenye ulemavu ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja akiwa kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea wa CCM Ridhiwani Kikwete kwenye Kijiji cha Pongwemnazi kata ya Kimange.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa CCM Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kwenye kijiji cha pongwekiona kata kimange wilayani bagamoyo 

 wananchi wa kijiji cha pongwekiona wakiwa wanamsikiliza mgombea ubunge jimbo la chalinze ridhiwani kikwete hayupo pichani wakati wa mkutano wa kampeni

 Mwigizaji aitwaye Puto akitoa burudani kwa wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Pongwemnazi kata ya Kimange wilayani Bagamoyo

 Mwimbaji Sam wa Ukweli akiimba na moja ya wananchi kwenye mkutano wa kampeni wa CCM kwenye kijiji cha Pongwemnazi 

 Wagombea Ridhiwani Kikwete kushoto akicheza na mgombea Udiwani kata ya Kimange Hussein Hadingoka wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kwenye kijiji cha Pongwekiona

 Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Ridhiwani Kikwete kushoto akimkabidhi ilani mgombea udiwani wa kata ya Kimange Hussein Hadingoka wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kwenye Kijiji cha Pongwekiona

 Mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kupitia CCM akimkabidhi ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020, diwani wa Viti maalumu Nuru Mpwimbwi wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kata ya kimange kwenye Kijiji cha Pongwekiona 

 Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akimkabidhi moja ya wanachama wapya kwenye Kijiji cha Pongwekiona

No comments:

Post a Comment