Tuesday, October 6, 2015

DIWANIA AHIDI KUNUA GARI LA WAGONJWA

Na John Gagarini, Chalinze
MGOMBEA Udiwani kata ya Vigwaza Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Muhsin Bharwan amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa atanunua gari la kubeba wagonjwandani ya kipindi cha miezi sita kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa wanaopata rufaa kwenda hospitali kubwa.
Aliyasema hayo kwenya mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete kwenye Kijiji cha Buyuni kwenye kata hiyo na kusema kuwa gari hilo litatumika kwenye vijiji vya kata hiyo ya Vigwaza.
Bharwan alisema kuwa kutokana na kata hiyo kutokuwa na gari la wagonjwa wakazi  hao wamekuwa wakipata taabu kuwapeleka wagonjwa wao wanaopata rufaa kwenda kwenye hospitali kubwa kama vile Tumbi au Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Endapo nitafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hii ya Udiwani ndani ya miezi sita nitahakikisha nimenunua gari la kubeba wagonjwa, tutamwomba mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupata msamaha wa kodi toka serikalini ili kufanikisha kupatikana gari hilo,” alisema Bharwan.
Alisema kuwa kwa kushirikiana na Wanakijiji hao atahakikisha ujenzi wa zahanati unakamilika ili waanze kupata huduma za afya kijijini hapo badala ya kupata huduma hiyo mbali kwani kwa sasa hakuna huduma hiyo kutokana na kukosa zahanati.
“Sera inasema kila Kijiji lazima kiwe na zahanati na kata inakuwa na kituo cha afya hivyo tutahakikisha tunatimiza hilo ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi,” alisema Bharwan.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni pmaoja na upatikanaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wahudumu wa afya wanapatikana.
Ridhiwani alisema kuwa pia upatikanaji wa madawa, vifaatiba, pamoja na ujenzi wa nyumba za wahudumu wa afya ili waishi kwenye vituo vyao vya kazi kwa lengo la kutoa huduma kwa urahisi.
Naye mkazi wa Kijiji hicho Pamilasi Sambana alisema kuwa huduma hizo za kiafya zikipatikana itawasaidia kukabiliana na matatizo yanayotokana na umbali wa upatikanaji wa huduma hizo.
Sambana alisema kuwa huduma za afya ni moja ya vilio vya wananchi na mara anapotokea mgonjwa inakuwa ni taabu sana hivyo wanawaomba wagombea hao kutimiza ahadi zao ili kuwapunguzia adha ya kupata huduma hizo.
Mwisho.

Na John Gagarini, Chalinze
UTUNGWAJI wa sheria ndogondogo kwenye Kijiji cha Malivundo kata ya Pera kwenye Jimbo la Chalinze kumesaidia kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambayo ilikuwa imekithiri katika Kijiji hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari moja ya wanakamati ya maridhiano baina ya wakulima na wafugaji ya Kijiji hicho Charles Antony alisema kuwa tangu kuundwa kamati hiyo miezi minne iliyopita migogoro imepungua kwa kiasi kikubwa.
Antony alisema kuwa mkutano wa Kijiji ulipitisha sheria ya kumtoza mfugaji gunia nane za mahindi kwa hekari moja  endapo ataingiza mifugo kwenye shamba la mkulima ambalo lina mazao na kwa shamba ambalo limeandaliwa halina mazao atatozwa kiasi cha shilingi 50,000 kwa hekari moja  na 40,000 kwa shamba ambalo limevunwa mazao.
“Sheria hii iliridhiwa na wakulima na wafugaji licha ya kuwa tatizo kubwa lipo kwa wafugaji ambao wamekuwa wakilisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima hali ambayo ilikuwa inasababisha migogoro ya mara kwa mara lakini toka sheria hii imepitishwa na Kijiji matatizo hayo yamepungua,” alisema Antony.
Alisema kuwa endapo mlalamikiwa anakataa kutekeleza agizo la kamati suala hilo linapelekwa ngazi ya kata ambako nao husisitiza mlalamikiwa kulipa faini hiyo mara baada ya kamati kupita kwenye eneo ambalo limefanyiwa uharibifu.
“Kamati hii inaundwa na watu 10 wakulima watano na wafugaji watano ambao huangalia ukubwa wa tatizo kisha hutoa maamuzi juu ya uharibifu uliofanywa lakini pia pande mbili zinazohusika nazo huruhusiwa kukaa na kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo,” alisema Antony.
Ashura Ramadhan alisema kuwa kwa sasa angalau mazao yao yanaweza kukua bila ya tatizo lolote tofauti na ilivyokuwa awali ilikuwa ni ugomvi mkubwa kati ya wakulima na wafugaji lakini kwa sasa angalau amani inapatikana kutokana na sheria hizo.
Kwa upande wake mgombea udiwani  kata ya Pera kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)Lekope Laini alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anatumia taaluma yake ya sheria kukabili migogoro ya wakulima na wafugaji pia kuwaunganisha ili waishi kama ndugu.
Naye mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM Ridhiwani Kikwete alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha mpango wa matumizi bora ya ardhi unawekewa mkazo ili kuwe na maeneo ya wakulima na wafugaji kupunguza migogoro hiyo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WAKINAMAMA wa Jamii ya wafugaji kwenye Kijiji cha Wafugaji cha Chamakweza wameiomba serikali kuwapatia matenki makubw aya kuhifadhia maziwa pamoja na soko la uhakika la kuuza maziwa yao.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete Anastazia Masaka alisema kuwa maziwa wanayozalisha ni mengi lakini hawana sehemu ya kuhifadhia pamoja na soko la uhakika.
Masaka alisema kuwa wanaiomba serikali kuwapatia matenki hayo ili waweze kuhifadhi maziwa yao ili yasiweze kuharibika wakati yakisubiri kusafirishwa au kuwasubiri wanunuzi wa maziwa hayo ambayo yanapatikana kwa wingi kwenye kijiji chao ambacho ni cha wafugaji.
“Maziwa ni mengi lakini tunataabika na soko pamoja na sehemu ya kuhifadhia hivyo tunaiomba serikali kupitia mgombea Ubunge kutusaidia kupata matenki ya kuhifadhia pamoja na soko la uhakika kwani soko likiwa kubwa vijana wetu watapata ajira kupitia maziwa,” alisema Masaka.
Alisema kuwa wakipata ufumbuzi wa masuala hayo basi itakuwa ni ufumbuzi wa changamoto wa namna ya kuhifadhi pamoja na soko la kuuza bidha hiyo ambayo inapendwa na watu kutokana na umuhimu wake kiafya.
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo atahakikisha soko pamoja na matenki hayo vinapatikana ili kuwaondolea adha ya kuhifadhi maziwa yao pamoja na soko.
Ridhiwani alisema kuwa kwa kupitia umoja wao wa wauzaji maziwa atahakikisha anawaletea wanunuzi wa maziwa pia wanawezeshwa kuptia fedha ambazo zitatolewa kwa kila Kijiji kiasi cha shilingi milioni 50.
Naye mgombea Udiwani Lekope Laini alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anakabiliana na changamoto za akinamama wa kifugaji ili nao waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao.
Mwisho.

Na John Gagarini, Bagamoyo

KATIKA kuhakikisha kurahisisha utendaji kazi hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani kimetoa pikipiki 12 kwa makatibu kata kwenye Jimbo la Bagamoyo ili kuwaondolea tatizo la usafiri wakati wakutimiza majukumu yao.


 Akikabidhi pikipiki hizo mwenyekiti wa CCM wilayani hapo Maskuzi alisema walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa usafiri kwa makatibu hao hivyo kushindwa kutekeleza kikamilifu shughuli za chama.

Maskuzi alisema kuwa lengo lingine ni kuwawezesha makatibu kata hao kuweza kusimamia majukumu yao kikamilifu pamoja na uhai wa chama na kurahisisha shughuli hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi.

“Utoaji wa pikipiki hizi zenye thamani ya  shilingi milioni 24 kwa makatibu wa kata ni muendelezo  ambapo awali kwenye awamu ya kwanza tulitoa pikipiki 15 katika Jimbo la Chalinze na sasa kumalizia na jimbo la Bagamoyo,” alisema Maskuzi.

Alisema kuwa kwasasa anaamini watendaji hao watafanya kazi zao pasipo usumbufu kwani tatizo kubwa lilikuwa ni ukosefu wa usafiri wa uhakika wakutembelea maeneo mbalimbali ya kazi.

“Pikipiki hizi tunazitoa sio kwa shughuli nyingine ila ni kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kichama kwa kutembelea matawi,kusimamia uhai wa chama na kutekeleza majukumu yatakayotakiwa kufuatilia wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu”alisema Masukuzi.

Kata zilizopatiwa pikipiki hizo ni pamoja na Mapinga, Kerege, Zinga, Kilomo, Yombo, Dunda, Magomeni, Kisutu na Nianjema, Makurunge na Fukayosi na pikipiki moja itakuwa kwa ajili ya mtendaji mkuu CCM wilayani hapo.
                            
Kwa upande wake katibu wa CCM kata ya Kisutu Buruhani Setebe alisema amepokea pikipiki na amekishukuru chama kwa kutambua changamoto yao hivyo atahakikisha anaitunza pikipiki hiyo.

Naye katibu wa CCM kata ya Mapinga ,Muhdin Mipango alisema awali walikuwa wakipata shida katika utendaji wa kazi zao ikiwa ni pamoja na kutembelea kwa miguu ama kukodi pikipiki ili kwenda kutembelea matawi.

                                          Mwisho.




No comments:

Post a Comment