Na John Gagarini, Chalinze
WANAFUNZI wawili wa kidato cha tatu waliokuwa wakisoma shule ya sekondari Msata wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambao mwanzoni mwa mwaka jana walilamikiwa na wanafunzi wenzao kuwa wanajihusisha na vitendo vya ushirikina shuleni hapo hali iliyosababisha washindwe kuendelea na masomo wako katika hatari ya kukatishwa masomo kufuatia taarifa kuwa mmoja kaozeshwa kwa mwanaume na mwingine yuko kwenye mipango ya kuolewa.
Wanafunzi hao ambao wanatoka kijiji cha Mkoko kata ya Msata wilayani humo wanadaiwa kuwa wako kwenye hatua hizo baada ya wazazi wao na walezi kushindwa kuwafanyia uhamisho kwenda shule nyingine baada ya wanafunzi wenzao kuwakataa kutokana na madai hayo ya ushirikina.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi moja ya wakazi wa kijiji hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake kutajwa alisema kuwa mwanafunzi wa kwanza (17) anaishi na mwanaume baada ya baba yake kumwoza.
Alisema kuwa baba wa mwanafunzi huyo Damian Joseph alifikia hatua hiyo baada ya mwanae kugoma kuendelea kusoma kwenye shule hiyo na kutaka ahamishiwe shule nyingine kutokana na wenzake kumtuhumu kuwa ni mshirikina.
Baba wa mwanafunzi huyo Joseph alipoulizwa juu ya suala hilo alikanusha na kusema kuwa hajamwoza mwanaye na hana mpango wa kumwozesha kwa kuwa bado ni mwanafunzi ila tatizo lilikuwa ni uhamisho na kufiwa na mkewe.
Akielezea juu ya tatizo la mwanae alisema kuwa mwanawe alikuwa ni mnyonge na kukata tamaa ya kusoma kutokana na wanafunzi wenzake kumtuhumu kuwa ni mchaawi na anawaloga wanafunzi wenzake yeye na mwenzake ambao wanatoka Kijiji kimoja hivyo walishindwa kwenda shule na yeye alikataa kurudi shuleni vinginevyo ahamishiwe shule nyingine.
Joseph alisema kuwa jambo lililomfanya ashindwe kumhamisha mwanae ni kutokana na msiba wa mkewe uliomfanya achanganyikiwe hivyo kusimamisha taratibu za kumhamisha shule hata hivyo amesema kuwa atahakikisha mwanae anawekwenda shule.
Kwa upande wa mwanafunzi (17) ambaye alidaiwa yuko kwenye mchakato wa kutolewa mahari na mwanaume kaka wa mwanafunzi huyo Ramadhan Ndege alikanusha taarifa hizo na kusema kuwa mdogo wake yuko kwa bibi yake mzaa mama ambapo kwa sasa anazaidi ya miezi sita hajaenda shule kutokana na kuwa na matatizo ya mapepo.
Ndege alisema kuwa si kweli kuwa mdogo wake yuko kwenye mpango wa kuozeshwa ila yuko kwa bibi yake akipatiwa matibabu ambapo akienda shule hali inakuwa mbaya kutokana na mapepo kumsumbua.
“Changamoto nyingine ni kukosa fedha kwa ajili ya kumfanyia uhamisho kiasi cha shilingi 250,000 ambazo ni gharama zote kuanzia ufuatiliaji pamoja na sare, vitabu na vifaa vinavyotakiwa kwenye shule anayokwenda ya Changarikwa ambayo ni jirani na kijiji hicho,” alisema Ndege.
Alisema kuwa tatizo kubwa linalowasumbua ni ukosefu wa fedha kwani kipato chao ni kidogo na hawawezi kupata fedha hizo kwa mara moja na msaada ni mdogo kwani wazazi wao walishafariki nakuomba kama kuna wafadhili wanaoweza kuwasaidia wajitokeze ili kuwasaidia kumpeleka shule ndugu yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Hamis Buzoza alisema kuwa mambo hayo yalikuwa yakifanywa kifamilia zaidi lakini masuala hayo hayajapelekwa ofisini kwake ila aliwataka wazazi wa familia hizo kutofanya hivyo kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment