Na John Gagarini, Chalinze
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk John
Magufuli emesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha mji wa
Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani unakuwa moja ya miji ya kisasa na wa
uwekezaji ambapo utakuwa na barabara za juu Fly Over.
Aidha ujenzi huo ambao utakuwa wa barabara sita hadi jijini
Dar es Salaam utagharimu kiasi cha shilingi trilioni 2.3 na Chalinze itakuwa
kiunganishi cha njia hizo kwenda mikoa ya Kasakazini na mikoa ya Kati ambapo
tayari wataalamu wa upembuzi wa ujenzio huo wamelipwa kiaisi cha shilingi billion
7.7.
Aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni kwenye Jimbo la
Chalinze mkoani humo ambapo alisema kuwa atahakikisha mji huo unakuwa wa kisasa
na huduma zote muhimu zinapatikana hapo na kuwa mji mbadala wa Dar es Salaam.
Dk Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi na Miundombinu alisema
kuwa mji huo utakuwa kituo kikubwa cha uwekezaji hapa nchini kwani faida
nyingine iliyopo ni kugunduliwa gesi eneo la Ruvu hivyo kufanya uchumi wa mji
huo kuwa juu na wananchi wataboresha maisha yao na kuwa na maisha bora.
“Msiuze kiholela maeneo yenu kwani baadhi ya watu wanauza
maeneo kwa bei ndogo lakini watakao nunua watakuja kuuza kwa bei kubwa hivyo
huu ni moja ya miji itakayokuwa ya kisasa hapa nchini na sasa maisha bora
yanakuja na sitawaangusha naomba mnipigie kura nyingi za kutosha ili niweze
kuwa Rais,” alisema Dk Magufuli.
Alisema kuwa kuhusu changamoto ya maji kwenye mji huo alisema
kuwa atahakikisha suala hilo linakwisha ambapo aliipongeza awamu ya tatu na nne
ambazo zimejitahidi angalau maji yanapatikana kwani mji huo ulikuwa na tatizo
kubwa la maji.
Katika hatua nyingine amesema anashangazwa na baadhi ya
wanasiasa kusema kuwa fedha zilizokuwa zijenge bandari ya Tanga zimepelekwa
Bagamoyo kisa ni wilaya anayotoka Rais Dk Jakaya Kikwete.
“Kauli kama hizo ni za uchonganishi kwani kila eneo
limetengewa fedha zake kwa ajili ya ujenzi wa Bandari kuanzia Tanga, Mtwara na
Mwanza kote kutajengwa bandari hizo na Bagamoyo ni uwekezaji wa watu binafsi
hivyo hakuna sababu ya kuwachonganisha watu kwa maneno ya uongo,” alisema Dk
Magufuli.
Alibainisha kuwa hizo ni hoja hafifu na hazina msingi wowote
zaidi ya kuleta uchonganishi kwani wanapaswa kutangaza sera zao na si kuongopa
hali ambayo inajenga chuki baina ya wananchi wa eneo fulani na eneo jingine.
Alisisitiza kuwa endapo atapata
ridhaa ya kuongoza atahakikisha ushuru mdogomdogo unaondolewa ili kuwaondolea
kero wananchi ambao wanataka kujiongezea kipato kutokana na shughuli zao za
ujasiriamali.
Kwa upande wake mgombea Ubunge wa
Jimbo hilo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alimshukuru Dk Magufuli kwa mipango
hiyo na kusema kuwa changamoto iliyopo ni ujenzi wa kituo cha afya kikub wa ili
kukabiliana na uwingi wa wagonjwa pamoja na majeruhi kwenye kituo cha afya chya
Chalinze.
Ridhiwani alisema kuwa changamoto
nyingine ni maji ambayo licha ya kupatikana bado kuna baadhi ya maeneo hayapati
maji hasa kwenye makmao makuu ya vitongoji ambapo kwa makao makuu ya vijiji
yote yanapata maji kwa asilimia 94 ambapo Dk Magufuli alisema atashughulikia
changamoto hizo endapo atachaguliwa kuwa Rais.
Mwisho
No comments:
Post a Comment