Na John
Gagarini, Chalinze
WAKAZI
wa Kijiji cha Misani kata ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wameiomba
serikali kuibana kampuni Eco Energy kuwalipa fidia ya mali zao ili kupisha
upanuzi wa barabara ya kuelekea kwenye mradi wa umwagiliaji.
Wakizungumza
kwenye mkutano wa hadhara wa mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete ambapo wakazi wa Kijiji hicho walisema kuwa tathmini
ya upanuzi huo haukuwashirikisha wananchi na utaathiri mali zao.
Mkazi wa
Kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Ally Hemed alisema kuwa mradi huo
ambao ni wa kampuni hiyo ambapo imeweka alama za kupita barabara hiyo na kusema
kuwa hakutakuwa na fidia yoyote itakayotolewa kwa uharibifu wa mali zao.
“Wamekuja
hapa kijijini na kuweka alama za kuonyesha barabara itapita wapi ambapo katika
maeneo hayo kuna mali zetu zitaathiriwa ikiwa ni pamoja na nyumba, mazao ya
nanasi, miti na vitu vingine ambapo tumeambiwa kuwa hatutalipwa chochote jambo
ambalo tunaona kuwa hatutatendewa haki mara zoezi hilo litakapoanza,” alisema
Hemed.
Alisema
kuwa kutokana na kutolipwa wao hawako tayari kuruhusu greda la kuchonga
barabara kupita kwenye maeneo yao hadi watakapolipwa fidia za mali zao.
“Hatuna
tataizo na kuchongwa barabara yetu lakini tunachoomba tulipwe kwanza fidia
ndipo upanuzi ufanyike kama unavyoona mananasi yetu karibu yatakomaa na nyumba
zetu zinaonekana zipo kwenye eneo la upanuzi wao watulipe kwanza ndipo wafanye
upanuzi huo,” alisema Hemed.
Kwa upande
wake mgombea udiwani kata ya Kiwangwa Malota Kwaga alisema kuwa jambo hilo
limekuwa ni kero kubwa kwa wakazi hao hivyo ni vema suala lao likaangaliwa
kabla ya utekelezaji wake.
Kwaga alisema
kuwa wananchi wametoa malalamiko yao kwa wahusika lakini hawajaonesha nia ya
kutoa fidia kwa watu ambao wataathiriwa na zoezi hilo.
Naye
Ridhiwani alisema kuwa wahusika hao wanapswa kulipa fidia kabla ya kutekeleza
mradi huo kwani haipendezi watu kuharibiwa mali zao bila ya kulipwa fidia.
Ridhiwani
alisema kuwa tayari amewasiliana na wahusika na kuwaambia kuwa walipe kwanza
fidia kabla ya kuanza upanuzi huo wa barabara hiyo inayoelekea kwenye mradi
huo.
“Sheria haisemi hivyo lazima unapofanya suala
la maendeleo kwenye ardhi lazima ulipe fidia kwenye maeneo ambayo unayaendeleza,”
alisema Ridhiwani.
Aidha alisema
kuwa jambo hilo ni la maendeleo lakini pia liangalie haki za wananchi ambao
mali zao zitaathiriwa na maendeleo hayo hivyo kwa sasa hakutafanyika chochote
hadi malipo yatakapofanyika.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment