RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete amesema kuwa mara atakapostaafu nafasi hiyo Novemba 5 mwaka huu anatarajia kuanzisha taasisi ya maendeleo kwa Afrika na Dunia.
Aidha alisema kuwa atarudi Kijijini kwake Msoga Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo mbali ya kuanzisha taasisi hiyo ya maendeleo pia ataendeleza ufugaji na kilimo cha mananasi.
Dk Kikwete aliyasema hayo jana katika Kijiji cha Msoga mara baada ya kupiga kura yake kwenye uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais, Mbunge na Diwani na kusema kuwa amefurahi sana kuona watu wanapiga kura bila ya usumbufu wowote.
Dk Kikwete alisema kuwa mara baada ya kustaafu na baada ya Rais mpya kuapishwa Desemba 5 atajihusisha na masuala hayo kwani hawezi kukaa tu hivi bila ya kuwa na jambo la kufanya kwani ataendelea kuwa na nguvu.
“Natarajia kuwa mfugaji kwani nina shamba la mifugo pia kuwa mkulima wa mananasi huko Kijiji cha Kiwangwa na ninafurahi kupiga kura kwani nimetumia haki yangu na nanishukuru hadi sasa hatujasikia kama kuna tatizo lolote,” alisema Dk Kikwete.
“Nawaomba wananchi wajitokeze kupiga kura na ningependa na vituo vingine viwe na utulivu kama hichi cha hapa na watu washiriki uchaguzi ili baadaye wasije wakahoji kuwa hata fulani kachaguliwa wakati wao hawakupiga kura kumchagua kiongozi ambaye wanamtaka wao,” alisema Dk Kikwete.
Juu ya uchaguzi wa mwaka huu alisema kuwa chaguzi zote zinakuwa na upinzani mkali na anaomba hali ya amani iendelee hivi ili iwe nchi ya mfano kwa kufanya uchaguzi bila ya kuwa na vurugu.
Kwa Upande wake mgombea wa Ubunge wa (CCM) Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa anashukuru kwani hadi sasa zoezi hilo la upigaji kura linaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote na anaamini kuwa uchaguzi utakwenda vizuri.
Ridhiwani ambaye naye alipiga kura kwenye kituo cha Kijiji cha Msoga alisema kuwa kuna changamoto ndogondogo zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu hawakuona majina yao licha ya kuwa walikuwa na vitambulisho vya kupigia kura huko maeneo ya Miono.
Naye mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mathayo Torongey alisema kuwa amepita kwenye vituo vingi hajaona tatizo lakini kuna baadhi ya maeoneo mawakala wao walitishwa.
Torongey alisema kuwa mawakala hao walitishwa kwenye kituo cha Kijiji cha Msoga lakini baada ya makubaliano waliweka mawakala wengine na wakaendelea na zoezi la kusimamia kwenye vituo walivyopangiwa.
Aidha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa hadi mchana kulikuwa hakuna tatizo lililoripotiwa licha ya kuwa baadhi ya maeneo watu walikuwa na hofu kwamba zoezi litaenda taratibu lakini hali hiyo iliondoka na utaratibu kwenda vizuri.
Ndikilo alisema kuwa eneo la Vigwaza kulikuwa na hofu ya upungufu wa karatasi kutokana na idadi kubwa ya watu lakini hali hiyo iliwekwa sawa na mambo yanakwenda vizuri na wameweka ulinzi wa kutosha.
Alibainisha kuwa suala la kukaa mita 200 kwa ajili ya kulinda kura halipo kwani sheria imeelekeza vizuri juu ya watu mara baada ya kupiga kura wanaondoka na hakuna mtu aliyebaki kulinda kura kwani wameondoka na kuendelea na shughuli zao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment