Na John Gagarini, Lugoba
WAGOMBEA wanaowania nafasi za uongozi
hapa nchini wametakiwa kukubali matokeo mara uchaguzi utakapofanyika Oktoba 25
mwaka huu kwani kuna maisha mengine baada ya uchaguzi kuendelea kufanya kampeni zao huku wakiendelea
kuhubiri na kulinda amani iliyopo kwani wana nafasi kubwa ya kuwashawishi
wafuasi wao wasifanye vurugu au kufanya vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa
amani.
Pia wagombea watakaoshindwa
kwenye uchaguzi mkuu wakubali matokeo kwani kwenye washindani lazima kuwe na
washindwa ili kuondoa hali ya mafarakano kwani kwa wale watakaoshindwa
wasipokubali matokeo wanaweza kuleta uvunjifu wa amani.
Hayo yalisemwa juzi Kijiji cha
Maviayangombe kata ya Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na Askofu mkuu wa
Dayosisi ya Morogoro ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jacob
Mameo Ole Paulo wa Dayosisi ya Morogoro wakati wa mazishi ya mtoto wa aliyekuwa
kiongozi wa wafugaji Laban Moreto, Karokya Moreto (33) ambaye alikuwa
mwanajeshi wa kikosi cha 04/691 cha Mtwara.
Askofu Ole Paulo alisema kuwa
wagombea hao wanauwezo wa kudumisha amani kwa kuhubiri au kuingiza nchi kwenye
machafuko endapo watayatumia vibaya majukwaa wakati wa kipindi hichi cha
kampeni za uchaguzi.
“Wanapaswa kuhubiri amani na
kuacha kutumia maneno yatakayo haribu amani ya nchi iliyopo ambayo imedumu kwa
kipindi kirefu tangu nchi ilipopata uhuru miaka zaidi ya 50 hivyo itakuwa ajabu
ivunjwe kisa kuwania uongozi tu,” alisema Askofu Ole Paulo.
Aidha alisema kuwa vyama vya
siasa vinapaswa kupingana kwa hoja na kwa malumbano ambayo hayana maana bali
yanaweza kuleta mitafaruku isiyokuwa ya lazima hasa kwa wale wanaoshindwa kwani
wanapaswa kukubali matokeo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo
la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa amesikitishwa na kifo cha marehemu
ambaye alikuwa ni ndugu kwani wamekuwa wakiishi kama familia moja na walikuwa
na ushirikiano mkubwa baina ya familia zao.
Ridhiwani alisema kuwa kifo hicho
ni pigo kwa familia hiyo pia kwa Taifa kwani alikuwa ni mtumishi wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) na alikuwa mtaalamu wa rada hivyo pengo lake haliwezi
kuzibika kikubwa ni kumwombea marehemu.
Kufuatia msiba huo Rais Dk Jakaya
Kikwete alituma salamu za pole kwa familia hiyo kupitia kwa Mbunge wa Jimbo la
Chalinze Ridhiwani Kikwete na kusema kuwa anatoa pole na Mungu awape nguvu
katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo na yuko pamoja nao.
Alisema kuwa Rais alishindwa
kuhudhuria msiba huo kwani kwa sasa yuko nje ya nchi lakini pindi atakaporudi
ataitembelea familia hiyo kwa ajili ya kuifariji kufuatia kifo cha mtoto wa
aliyekuwa kiongozi wa kabila wafugaji
Naye mgombea Ubunge Jimbo la
Chalinze kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mathayo Torongei
alisema ili amani iendelee kuwepo ni vema dola ikatenda haki badala ya
kupendelea upande mmoja.
Marehemu alifariki kwa ajali
baada ya gari alilokuwa akiendesha kupasuka tairi la mbele na kusababisha ajali
iliyopelekea kifo chake siku ya Septemba 16 mwaka huu huko Mtwara ameacha mke na watoto watatu.
Mwisho.
Baadhi ya Wazee wakiwa wamekaa kwenye msiba huo huko kijiji cha Maviyangombe Lugoba wilayani Bagamoyo. |
Kulia ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Morogoro Jacob mameo Ole Paulo akiwa na mgombea Ubunge jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete. |
Askofu Jacob Mameo Ole Paulo akizungumza wakati wa msiba huo. |
Baadhi ya ndugu wa wakilia kuomboleza kifo cha ndugu yao. |
baadhi ya ndugu wa wakilia kuomboleza kifo cha ndugu yao. |
Akinamama ndugu wa karibu wa marehemu wakilia kuomboleza kifo hicho. |
Baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ wakiwa wamebeba jeneza lilokuwa na mwili wa marehemu kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi. |
Baadhi ya waombolezaji wakiaga mwili wa marehemu kabla ya mazishi |
Sehemu ya waombolezaji wa msiba huo. |
No comments:
Post a Comment