Na John Gagarini, Mkange
WANANCHI wa Kijiji cha Gongo kata ya Mkange wilayani Bagamoyo
wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ambapo huweka foleni ya kuchota
maji kwenye kisima kilichopo kijijini hapo baada ya wiki mbili.
Kutokana na usosefu huo wa maji wananchi hao wamekuwa
wakinunua maji ya bomba ndoo ya lita 20 kati ya shilingi 1,000 na shilingi
1,500 maji ambayo huuzwa kwenye magari au pikipiki hivyo kuwafanya wajikute
hawapati maendeleo kutokana na gharama kubwa kuzitumia kununulia maji.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa
kampeni wa mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete,
kwenye kata ya Mkange mwananchi wa Kijiji hicho Hungilo Nyoka alisema kuwa maji
yamewafanya washindwe kupata maendeleo.
Nyoka alisema kila kaya inatakiwa ichote madumu manne ili
angalau kila mmoja apate baada ya hapo maji hukatika ambapo inatakiwa mtu
asubirie tena na mzunguko huo hufanya foleni ya mtu mmoja kufikiwa tena baada
ya wiki mbili kwani hapa kuna wananchi 1,690.
Alisema changamoto kubwa kwao ni maji ambayo yamekuwa
yakiwafanya washindwe kufanya shughuli za maendeleo ipasavyo kwani hata
wakipata fedha kutokana na shughuli zao fedha zote huishia kununulia maji.
“Tunawaomba wahusika kutuangalia kwa jicho la huruma maji
kwetu ni kikwazo cha kupata maendeleo kwani hata ukipata fedha kiasi gani zote
zinaishia kwenye maji hivyo tunaomba tuchimbiwe kisima kwani kilichopo maji ni
kidogo sana yanatoka kila baada ya saa moja yanakatika,” alisema Nyoka.
Aidha alisema kuwa maji wanayokunywa ni ya bomba lakini
yanatoka vijiji jirani vya Matipwili ambako kuna umbali wa kilomita 11 na
kijiji cha Mkange kilomita tisa na alisema kuwa chanzo cha maji ya kisima
kutotoka ipasavyo ni kwamba waliochimba kisima hawakuchimba hadi kuuukuta
mwamba ambapo chini ya mwamba ndiyo kuna maji mengi.
“Tunaomba wadau wa masula ya maendeleo kutusaidia kuweza
kupata maji kwani tunashindwa hata kujiletea maendeleo kutokana ukosefu wa maji
na wkati mwingine watoto hushindwa kwenda shule endapo maji yanakuwa ya shida
kwani hawawezi kwenda wachafua kwani mimi kwa siku hutumia madumu matatu hadi
matano kwa siku,” alisema Nyoka.
Kwa upande wake mgombea udiwani kupitia CCM Injinia Juma Mgweno
alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa sana lakini atahakikisha maji yanapatikana
kwa kuita wadau mbalimbali ili waweze kuwachimbia kisima.
Naye mgombea wa Ubunge kupitia CCM Ridhiwani Kikwete alisema
kuwa visima viwili vilivypo kijiji hapo havitoi maji ambapo kimoja kinahitaji
pampu ambayo imeharibika atahakikisha inapatikana mpya ili kuwaondolea kero
wananchi wa kijiji hicho.
Ridhiwani alisema kuwa mbali ya kuhakikisha pampu mpya
inapatikana pia kuna mradi mwingine wa mjai toka Matipwili na ule wa Wami
Chalinze atahakikisha maji yanafika kwani mradi huo utavifikia vijiji na
vitongoji ambavyo havikupata maji katika awamu mbili zilizopita vitafikiwa na
awamu hii.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mkange
KIJIJI cha Gongo kata ya Mkange wilaya ya bagamoyo mkoa wa
Pwani kinakabiliwa na ukosefu wa mizani ya kuwapimia watoto wenye umri chini ya
miaka mitano hali inayowafanya akinamama kuwapimia watoto wao mzani wa kijiji
cha jirani cha Matipwili.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho
wakati wa mikutano ya kampeni ya CCM ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Chalinze
Ridhiwnai Kikwete, moja ya akinamama Mwajuma Juma alisema kuwa hutugemea mizani
ya majirani zao ili kupata huduma hiyo.
Juma alisema kuwa kama ujuavyo kiafya watoto wenye umri wa
chini ya miaka mitano hubidi wahudhurie kliniki kila baada ya mwezi ambapo
huchunguzwa afya yake na moja ya jambo muhimu ni kupima uzito kwenye zahanati
ya kijiji.
“Tatizo lililopo kwenye zahanati yetu ni ukosefu wa mizani
ambapo hutubidi tukaazime kwa majirani zetu kijiji cha jirani hivyo kusababisha
msongamano mkubwa inapofikia siku ya kwenda kliniki tunaomba tusaidiwe
upatikanaji wa mizani kwa ajili ya kurahisisha huduma hiyo ambayo ni muhimu kwa
watoto,” alisema Juma.
Alisema kuwa kijiji kinalazimika kutoa kisia cha shilingi
10,000 kwa jili ya kumlipa mhudumu wa afya wa Kijiji hicho cha Matipwili ambaye
ndiyo hutoa huduma hiyo ya kuwapima uzito watoto hao wanapokwenda kliniki.
“Tunaomba tusaidiwe kifaa hicho kwani akinamama wanajitihada
kubwa ya kuwapeleka watoto wao kliniki lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa
mizani ya kuwapimia ambapo siku unapokuja siku hiyo inabidi kazi nyingine
zisifanyike kwa ajili ya kusubiria foleni kwa ajili ya kuwapima watoto uzito,”
alisema Juma.
Kwa upande wake mgombea Udiwani kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi CCM, Injinia Juma Mgweno alisma kipaumbele chake cha kwanza endapo
atachaguliwa ni kuhakikisha huduma za afya hasa za mama na mtoto zsinaboreshwa.
Mgweno alisema kuwa akichaguliwa atahakikisha kuwa huduma
bora zinapatikana ili akinamama na watoto waweze kuwa na afya bora kwa kupata
huduma muhimu za kiafya kwani bila ya afya bora mama hatoweza kuihudumia
familia yake.
Naye Mgombe Ubunge wa CCM Ridhiwani Kikwete alisema kuwa
chnagamoto ya vifaa tiba pamoja na wahudumu katika zahanati ya kijiji
iliyojengwa na Mkapa Foundation anaijua lakini mkakati wake ni kuhakikisha kuwa
wahudumu wa afya wanakuwepo pamoja na mganga ili huduma bora ziwepo.
Ridhiwani alisema kuwa atahakikisha wagnga watatu wanaletwa
kwenye zahanati hiyo ili kukabiliana na upungufu wa wahudumu wa afya katika
zahanati hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mkange
MGOMBEA Ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi( CCM)
Ridhiwani Kikwete amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo hilo
atahakikisha ujenzi wa shule ya Msingi Kwamakulu unakamilika ili kuwaondolea
adha wanafunzi kusoma shule ya kitongoji jirani cha Manda.
Aliyasema hayo jana kwenye Kitongoji cha Kwamakulu kata ya Mkange wilayani Bagamoyo
wakati wa mkutano wake wa kampeni kuomba ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo kwa
kipindi cha miaka mitano ijayo kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Ridhiwani alisema kuwa atahakikisha ujenzi huo unafanyika
ambapo kwa sasa wanafunzi wanaotoka kitongoji hicho husomea shule ya Msingi
Manda kwenye kitongoji cha jirani kwa kutembea muda wa masaa mawili hadi kufika
shuleni hali inayosababisha wengine kushindwa kusoma kutokana na umbali.
“Namshukuru Mungu kunijalia mimi nimesoma kiasi fulani lakini
hali kama hii ya kitongoji kukosa shule ya msingi ni jambo ambalo
halinifurahishi hata kidogo lakini naomba mnipe ridhaa ya kuwa kiongozi wenu
ili niweze kufanya kazi hii ya kuhakikisha shule ya msingi inapatikana hapa ili
watoto wafaidi shule,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa elimu ni haki ya msingi ya mtoto lakini pia
anapaswa aipate katika mazingira mazuri siyo kugeuka tena mateso kwani umbali
wa masaa mawili kwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni tatizo kubwa.
“Tumeanza na ujenzi wa darasa la awali ambapo nilitoa mifuko
100 ya simenti nashukuru naona angalau kimepatikana chumba kimoja cha darasa na
choo pamoja na nyumba ya mwalimu nitahakikisha ujenzi huu unakamilika na
baadaye tutaendelea na ujenzi wa madarasa mengine ili kupata shule hapa badala
kwenda Manda,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa CCM Injinia Juma Mgweno
alisema kuwa kwa kutumia elimu yake akishirikiana na mgombea ubunge
watahakikisha kwa pamoja shule inajengwa na inakamilika ili watoto waondokane
na adha ya kusoma mbali.
Mgweno alisema kata hiyo inakabiliwa na baadhi ya changamoto
ikiwa ni pamoja na ukosefu wa shule kutokana na baadhi ya vitongoji kujigawa
kutoka kwenye vijiji hivyo atahakikisha ujenzi wa shule na nyumba za walimu
inakuwa kipaumbele chake.
Naye mwananchi wa Kijiji hicho Siyawezi Juma alisema kuwa
ujenzi wa shule ya Msingi utasaidia kuwapunguzia adha watoto wao kwenda kusoma
umbali mrefu ambapo husababisha wengine kukata tama na kuacha shule kutokana na
umbali.
Juma alisema kujengwa kwa shule kitongojini hapo itakuwa ni
mkombozi wa watoto wao katika suala la elimu ambayo ni muhimu kwa watoto kwani
endapo wataikosa itawasababishia kuwa nyuma kielimu na kuhsindwa kujiendeleza
kimaisha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment