Na John Gagarini, Mandela
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi
Ridhiwani Kikwete amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa kwenye nafasi
hiyo atahakikisha zahanati inajengwa kwenye Kijiji cha Kibaoni ili kuwaondolea
adha wananchi wa kijiji hicho.
Aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika
Kijijini hapo kata ya Mandela na kusema kuwa ilani ya chama anasema kila kijiji
lazima kiwe na zahanati huku kila kata ikitakiwa kuwa na kituo cha afya ili
kurahishisha upatikanaji wa huduma za afya karibu.
Ridhiwani alisema kuwa hicho kitakuwa moja ya vipaumbele
vyake ambavyo atahakikisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ujenzi huo
unakamilika na wanakijiji wanapata huduma za afya karibu tofauti na sasa ambapo
huwalazimu kwenda kijiji jirani cha Mandela.
“Ilani ya chama inasema kuwa kila kijiji lazima kiwe na
zahanati hivyo endapo nikichaguliwa kwenye nafasi hii ya ubunge kwa
kushirikiana na wananchi hivyo nitahakikisha zahanati inajengwa ili huduma
zipatikane karibu,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa hata kata ya Mandela haina Kituo cha afya ambapo
kata hiyo ni mpya ambayo imezaliwa kutoka kata ya Miono na kutaka ujenzi wa
kituo hicho cha afya kujengwa kwenye kijiji hicho.
“Katika kipindi cha uongozi wangu wa mwaka mmoja na miezi miwili
tumeweza kukarabati zahanati 24 huku nane zikiwa zimejengwa pia tumeweza
kufanikisha kujngwa nyumba za waganga pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba na
dawa,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya vijiji
kukosa zahanati hata hivyo mikakati ni kuhakikisha zinajengwa ambapo mipango
inaendelea kwa kushirikiana na wananchi.
Kwa upande wake mgombea udiwani wa kata ya Mandela Madaraka
Mbode alisema kuwa tayari kata imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 10 kwa
ajili ya ujenzi wa zahanati kwenye kijiji cha Kibaoni.
Mbode alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo utafanikiwa endapo
wananchi watawachagua wgombea kutoka CCM lakini endapo wakiwachagua viongozi wa
vyama vya upinzani hawataweza kupata maendeleo.
Naye mkazi wa Kibaoni Ally Athuman alisema kuwa changamoto
kubwa inayowakumba wananchi kwenye zahanati wanazokwenda kupata matibabu ni
ukosefu wa dawa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mandela
MGOMBEA Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya
Mandela wilaya ya Bagamoyo Madaraka Mbode amemwomba mgombea Ubunge Jimbo la
Chalinze Ridhiwani Kikwete kusimamia ujengwaji wa tenki kubwa la maji ili
kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji.
Mbode aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Lupungwi wakati wa
mkutano wa kampeni za Ubunge nakusema kuwa Ridhiwani ndiye aliyeanzisha
mchakato wa ujengwaji wa matenki kwenye baadhi ya vijiji.
Alisema kuwa awamu ya pili imevifanya vijiji vingi kwenye
Jimbo hilo kuwa na maji lakini baadhi bado havijapata huduma hiyo ambapo awamu
ya tatu ya mradi wa maji utavifikia vijiji na vitngoji ambavyo havikubahatika
kupata maji.
“Wananchi nawaombeni mchagueni Ridhiwani kwani anauwezo wa
kutufanikishia kupata maji ambapo kwa sasa maji yanatoka lakini endapo
kunatokea tatizo kwenye mtambo maji hayapatikani ndiyo maana ujenzi wa matenki
makubwa unaanza ili kuhakikisha maji yanapatikana muda wote,” alisema Mbode.
Aidha alisema kuwa anaomba na yeye achaguliwe kwenye nafasi
ya udiwani ili ashirikiane na mbunge huyo kuwaletea maendeleo ambapo kwa sasa
kijiji hicho kimewekewa nguzo kwa ajili ya kuwasambaziwa umeme.
Naye Ridhiwani Kikwete alisema kuwa tayari tathmini
imeshaanza kufanywa ambapo wataalamu wameshachukua udongo kwa ajili ya kupima
kabla ya kujenga tenki hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mengi.
Ridhiwani alisema kuwa awamu hii ya tatu ya mradi wa maji wa
wami chalinze utavifikia vijiji na vitongoji vyote sambamba na ujengaji wa
matenki makubwa kwa ajili ya kuhifadhia maji.
Mwisho.
Na John Gagarini, Mandela
BAADHI ya waangalizi wa uchaguzi wamesema kuwa Tanzania
imeweka historia kwa kuwa na waangalizi wengi kwenye uchaguzi wa mwaka huu hali
ambayo itafanya uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Hayo yalisemwa jana na mwangalizi wa ndani kutoka (TEMCO) Renatus
Mkinga kwenye kijiji cha Lupungwi kata ya Mandela wilayani Bagamoyo wakati wa
mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete.
Mkinga alisema kuwa kwa waangalizi wa ndani ni zaidi ya 6,000
huku wale wa kutoka nje wakiwa ni 600 ambao ni wengi na haijawahi kutokea
katika chaguzi zilizopita.
“Sisi hatuna vyama tunachokifanya ni kuangalia ,mwenendo
mzima wa uchaguzi kuanzia hatua ya kampeni hadi utakapofanyika uchaguzi Oktoba
25 mwaka huu,” alisema Mkinga.
Alisema kuwa kazi ya wasimamizi ni kuangalia mienendo ya
uchaguzi katika kampeni na anaamini kuwa utakuwa huru na haki kwani hadi sasa
kampeni zinaendele vizuri.
“Tunahudhuria kwenye mikutano ya vyama mbalimbali ili
kuangalia wanapiga kampeni vipi na kuangalia wananchi wanajitokeza vipi
kusikiliza sera za vyama husika,” alisema Mkinga.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za
vyama mbalimbali ili waweze kuangalia ni mgombea gani ambaye anawafaa ili
mwisho wa siku waweze kumchagua kiongozi bora na si bora kiongozi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment