Sunday, February 22, 2015

JAMII ISIMAMIE UKIUKWAJI HAKI ZA WATOTO

Na John Gagarini, Kibaha
JAMII mkoani Pwani imetakiwa kusimamia malezi ya watoto wadogo na kuacha kuwafanyia vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikiwaletea athari kubwa katika makuzi yao.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mratibu wa mtandoa wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Watoto wadogo Tanzania (TECDEN) mkoa wa Pwani Feliciana Mmasi wakati wa mafunzo ya Sera ya Haki ya Mtoto Tanzania kwa walimu na walezi wa vituo vya watoto wadogo wilayani Kibaha.
Mmasi alisema kuwa baadhi ya watoto mkoani Pwani wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na ndugu wa karibu hata baadhi ya wazazi hasa wale wa kike.
“Kumekuwa na vitendo vingi vya ukatili ambavyo watoto wadogo wamekuwa wakifanyiwa huku baadhia ya jamii ikiviangalia na kuvifumbia macho hivyo kuendeleza unyanyasaji kwa watoto wadogo,” alisema Mmasi.
Aidha alisema kuwa baadhi ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto wadogo ni pamoja na ubakaji, vipigo, kuuwawa, kunyimwa chakula na vitendo ambavyo ni kinyume cha haki za binadamu.
“Utafiti uliofanyanyika mwaka 2010 kuhusu hali ya ukatili nchini umeonyesha kuwa watoto 6 kati ya 10 wamefanyiwa vitendo vya ukatili katika mikono ya ndugu na jamaa wa karibu huku mtoto mmoja kati ya wawili wamefanyiwa vitendo vya ukatili na walimu,” alisema Mmasi.
Kwa upande wake ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Joannes Bigirwamungu alisema kuwa wamekuwa wakiunda timu kwenye ngazi mbalimbali kwa ajili ya kupokea taarifa za vitendo vya ukatili na kuripoti kwenye vyombo vya sheria.
Bigirwamungu aliitaka jamii kutoa taarifa za baadhi ya watu wanaofanya vitendo vya ukatili kwa watoto ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika wa matukio hayo ambayo yanawanyima haki watoto.
Mwisho.

Monday, February 9, 2015

WAFUGAJI WASIOPELEKA WATOTO WA KIKE WALIOFAULU SEC KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

Na John Gagarini, Bagamoyo
WAZAZI wa watoto wa wafugaji  kwenye Kijiji cha wafugaji cha Chamakweza kata ya Pera wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametakiwa kuwapeleka shule watoto wao wakike waliofaulu kwenda kidato cha kwanza mwaka huu kwenye shule mbalimbali wilayani humo.
Hayo yalisemwa na mjumbe wa kamati ya wafugaji ya kata ya Pera, Yohana Kipojo, wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya awali ya Ekishomi inayomilikiwa na kanisa la Gosheni Inland lililopo kwenye kitongoji cha Chamakweza.
Kipojo alisema kuwa lengo la kuwahimiza wazazi hao kuwapeleka shule watoto wao wakike waliofaulu ni kuhakikisha wanapata elimu ya juu na kuachana na tabia ya kuwaoza huku wale wakiume wakipatiwa elimu.
“Tunatoa hadi Machi 30 endapo mfugaji yoyote kama hajampeleka shule mtoto wake wakike aliyefaulu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake hivyo lazima wahakikishe wanawapeleka ili wapate elimu,” alisema Kipojo.
Aidha alisema kuwa elimu ni haki kwa watoto wote na si watoto wa jinsia moja ambapo baadhi ya wazazi hawawapeleki watoto wakike shule na kuwapelendelea wakiume jambo ambalo linalosababisha watoto wakike kukosa elimu.
Kwa upande wake mlezi wa shule hiyo Rehema Ishengoma alisema kuwa kuwaoza watoto wadogo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu ambayo iko kikatiba.
Ishengoma amesema kuwa wanafunzi wakike wanaoozwa kwenye umri mdogo wanapata mateso makubwa hasa wakati wa kujifungua kwani miili yao bado haijawa na uwezo wa kujifungua na endapo mtoto wakike atapata elimu atajua haki zake na kuweza kuyatawala maisha yake.
Naye Mchungaji wa Kanisa hilo Jackson Bukelebe alisema kuwa lengo la kujenga shule hiyo ya awali ni kuwasogezea shule karibu watoto wawafugaji kwani shule zilizopo ziko mbali nao.
Mch Bukelebe alsema kuwa eneo hilo halina shule jambo ambalo linawafanya wanafunzi ambao ni wadogo kuwa na wakati mgumu kwenda shule ambapo kitongoji hicho hakuna shule.
Mwisho.  





Sunday, February 8, 2015

MKOA KUENDELEA KUSAIDIA MICHEZO

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesema kuwa mkoa utaweka mazingira mazuri kwa wanamichezo ili waweze kufanya vema kwenye michuano mbalimbali ya ndani na ile ya Kitaifa ili kuendeleza vipaji.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akipokea kombe la ushindi wa tatu kwa timu ya mpira wa Pete ya Ruvu JKT Mlandizi wilayani Kibaha ambayo ilishika nafasi hiyo kwenye mashindano ya Taifa yaliyofanyika mwaka jana.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa ofisi yake itahakikisha kuwa michezo ndani ya mkoa inasonga mbele kwa ili kuleta mafanikio kwenye sekta hiyo ambayo imekuwa ikiuletea sifa kubwa mkoa wa Pwani ambapo timu za soka za Ruvu Stars na Ruvu Shooting zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara zinatokea kwenye mkoa huo.
“Fedha ni changamoto kubwa kwenye sekta ya michezo lakini tutajitahidi kwa hali na mali kw akushirikiana na wadau wa michezo kuhakikisha timu zilizondani ya mkoa wetu zinafanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ya kimkoa na kitaifa ili kuendeleza sifa nzuri ya michezo iliyopo kwa sasa,” alisema Mhandisi Ndikilo.
 Aidha alisema kuwa licha ya mkoa kuwa na changamoto kubw aya ukosefu wa fedha lakini mkoa umekuwa ukipiga hatua kubwa na kuufanya kuweza kutamba kwenye nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na timu ya mpira wa soka la wanawake kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Taifa yaliyomaliziki hivi karibuni .
Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la michezo la mkoa ambaye ni katibu Tawala wa mkoa huo Mgeni Baruhani alisema kuwa kwa bahati mbaya hakuna fedha zinazotengwa kwa ajili ya michezo lakini ofisi ya mkoa imekuwa ikisaidia michezo kwa kuzichangia timu na vilabu vya mkoa ili vishiriki kwenye michuano mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha mpira wa Pete mkoani Pwani Fatuma Mgeni alisema kuwa timu hiyo kwa sasa iko kwenye maandalizi ya mashindano ya Afrika Mashariki itakayofanyika Zanzibar kuanzia mwezi Machi mwaka huu na kuwaomba wadau kujitokeza kuisaidi ili iweze kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

Mwisho.

WEKENI MFUKO WA KUSAIDIA WENYE UHITAJI

Na John Gagarini, Kibaha
VYAMA vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) wilayani Kibaha mkoani Pwani vimetakiwa kuweka mifuko kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye shida mbalimbali wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu na watoto waishio kwenye mazingira hatarishi.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) Kibaha Mjini Rugemalila Rutatina wakati wa kuwakabidhi  vifaa vya shule wanafunzi wa shule za msingi na  sekondari waishio kwenye mazingira hatarishi kwenye mtaa wa Kwa Mfipa wilayani humo vilivyotolewa na chama cha kuweka na kukopa cha Upendo cha mtaa huo.
Rutatina alisema kuwa ili jamii iweze kunufaika na vyma hivyo ni vema vikawa na mifuko hiyo ili kuwezesha makundi hayo ambayo hayana msaada wowote kutokana na hali zao.
“Ni vema vyama hivyo vikatenga fedha kidogo kwa ajili ya kuisaidia jamii kwani SACCOS zimeonekana kuwa ni msaada mkubwa kwa wanachama ambao wengi wao ni wajasiriamali kwa kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa kuwasaidia watu wenye shida ni ibaada ambayo inafanywa na mtu anayetoa hivyo Mungu humbariki na kumuongezea kwa kuwa amewajali wale wasio na uwezo kama vile wazee, wajane, yatima na  wenye ulemavu.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Kibaha Said Nangurukuta alisema kuwa chama hicho kimeonyesha mfano kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto waishio kwenye mazingira hatarishi hivyo kuwasaidia walezi wa watoto hao.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Faustina Kayombo alisema kuwa watoto wenye mahitaji maalumu wamekuwa wakiongezeka kila mara kutokana na utengano wa wazazi au mazingira magumu ya kwenye familia na kuwapatia vifaa hivyo chama hicho kimeisaidia serikali kubeba mzigo wa kuwasaidia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira hatarishi na kuwataka watu wenye uwezo kuwasaidia watoto kama hao.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mwajuma Teya alisema kuwa mbali ya chama chao kukopesha kimetenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanoishi kwenye mazingira magumu ambapo kimekuwa kikitoa vifaa mbalimbali pamoja na kuwalipia ada baadhi yawanafunzi.
Teya alisema kuwa mbali ya mafanikio hayo pia wanakabiliwa na changamoto ya udogo wa mtaji wao hali inayosababisha mzunguko wa kukopeshana kutokwenda kwa wakati, jumla ya wanafunzi 25 walipewa misaada hiyo na kinajumla ya wanachama 30 ambao ni wajasiriamali wanaojihusisha na ufumaji, ushonaji, ulimaji wa bustani, utengenezaji wa sabuni na kukopeshana na kilianzishwa mwaka 2012.
Mwisho. 

Tuesday, January 27, 2015

ZAKIA MEGHJI SHEREHE ZA CCM PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani Zakia Meghji anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za (CCM) kutimiza miaka 38 zitakazofanyika Kata ya Visiga wilayani Kibaha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa sherehe hizo zitaadhimishwa kwa shughuli mbalimbali za kuimarisha chama ambazo tayari zilishaanza tangu Januari 26 kwenye kata ya Mkuza.
Mdimu alisema kuwa Meghji ambaye ni Mbunge na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (MNEC) atahitimisha sherehe hizo Februari Mosi kwenye kata hiyo ambayo imepewa upendeleo kutokana na chama hicho kuchukua mitaa yote saba kwenye uchaguzi wa wenyeviti wa Mitaa uliofanyika hivi karibuni.
“Wakati wa sherehe hizi kutakuwa na shughuli mbalimbali kama vile kukagua uhai wa chama ngazi ya mashina, matawi, kata wilaya pamoja na uhakiki wa daftari la uanachama ili kuwa na takwimu sahihi za wanachama,” alisema Mdimu.
Aidha alisema kuwa kazi nyingine ni kufanya mikutano ya kuhamasisha wanachama kujitokeza kujiandikisha katika daftarai la wapiga kura msisitizo ukiwa ni kwa wananchi wote wenye sifa kujiandikisha upya hata wale wenye vitambulisho vya kupiga kura miaka iliyopita.
“Tunatarajia Halmashauri kuu za kata zitafanyika kwenye kata hizo za Kibaha Mjini ambazo ni 14 ambapo wajumbe wa mkoa watasambaa kwenye kata hizo kabla ya mkutano mkubwa wa hadhara wa kuhitimisha sherehe hizo ambapo Meghji ndiye atakayefunga akiwa ndiyo mgeni rasmi,” alisema Mdimu.
Aliwataka wanaccm kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kwenda kumsikiliza mlezi wa chama siku hiyo ili waweze kuimarisha chama katika maeneo yao pia kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kuhakikisha chama kinapata ushindi mkubwa wa kishindo huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisema Umoja ni Ushindi (Katiba Yetu, Taifa Letu).
Mwisho.

  

WANASIASA WASIMWAGE DAMU WAKATI WA UCHAGUZI

Na John Gagarini, Kibaha
WANASIASIA nchini wametakiwa kuwa na hofu ya Mungu na kuacha kutumia lugha za kusema kuwa watamwaga damu wakati wa kipindi cha uchaguzi.
Hayo yalisemwa na Mchungaji wa kanisa la Gosheni Inland Church lililopo kitongoji cha Chamakweza wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Jackson Bukelebe, wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya awali kituo cha kuhudumia watoto wa wafugaji inayomilikiwa na kanisa hilo.
Mch Bukelebe alisema wao kama kanisa wanataka uchaguzi wa amani na utulivu na hawataki wanasiasa watakaotuvunjia hali ya amani iliyopo na kutuletea vurugu kwani hao hawafai na hawastahili kuwa viongozi na wanapaswa kutumia lugha za ustaarabu na siyo zile zitakazosababisha uvunjifu wa amani ambayo imedumu kwa kipindi kirefu tangu nchi imepata uhuru,
“Viongozi hawa wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu na si kuwa na roho ya uharibifu na wakiwa na hofu ya Mungu watakuwa na upendo wa kuwapenda wengine na wataachana na mambo binafsi bali wataangalia mambo ya watu kwa ujumla,” alisema Mch Bukelebe.
Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye harambee hiyo mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Chalinze Mathayo Torongey alisema kuwa muda wa siasa umekishwa kinachotakiwa ni kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika ili kuwaondolea wananchi changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Kuhusu uchangiaji wa fedha kwa ajili ya elimu ni muhimu lakini kuna baadhi ya jamii ya wafugaji inaona kama elimu siyo jambo la muhimu hivyo kuwa wagumu kuchangia maendeleo ya elimu,” alisema Torongey.

Torongey ambaye alikuwa mgombe kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze aliwataka wanajamii ya kifugaji kutokuwa wagumu kuchangia elimu na kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wao wakike badala yake wawapleke shule.

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi moja ya wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo Amina Simbilwa alisema kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya kukosa elimu kutokana na baadhi ya wazazi wao kuhamahama kutafuta malisho.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2014 kwa lengo la kuwapatia elimu ya awali watoto hao kwani iliyopo iko mbali na wao ambao Kijiji chao ni cha Wafugaji na ina jumla ya wanafunzi 72.


Mwisho.   

Monday, January 26, 2015

MAJAMBAZI WALIOUA ASKARI BADO KUKAMATWA MSAKO WAENDELEA

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la polisi mkoani Pwani,linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watu waliohusika kufanya mauaji ya askari wawili wa jeshi hilo pamoja na kuiba silaha mbalimbali kwenye kituo cha polisi Ikwiriri,wilayani Rufiji .

Pia limekanusha uvumi wa kuwa siku ya tukio hilo kuliwa na askari wengine ambao walikimbia kwa lengo la kujihami baada suala ambalo si la ukweli. 

Kamanda wa polisi mkoani humo kamishna msaidizi mwandamizi Ulrich Matei alisema kuwa hakuna hadi sasa hakuna mtu aliyekamtwa na msako  unafanywa usiku na mchana ili kuhakikisha wanawapata wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

Aidha Matei aliitaka jamii kuacha tabia ya kuvumisha mambo yasiyo ya ukweli ama kuibua hoja zisizokuwa za ukweli baada ya matukio mbalimbali kutokea na badala yake anaetaka ukweli anatakiwa kuuliza kwa wahusika ili kupata taarifa za ukweli na si vinginevyo.

Wakati huo huo Mkuu wa wilaya ya rufiji Nurdin Babu amesema emesikitishwa na mauaji ya polisi wawili kwenye kituo cha ikwiriri wilayani humo juzi.
Akizungumza na gazeti hili Babu alisema kuwa tukio hilo ni la kusikitsha na halistahili kuungwa mkono na jamii iliyostaarabika.
"Inasikitisha sana na jambo hili ni ukatili na tunalilaani kwa nguvu zote na tutahakikisha tunawasaka watu waliohusika na tukio hili," alisema Babu.
Babu alisema kuwa wanaendelea kufuatilia na kufanya misako kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ili kubaini waliohusika na tukio hilo la kikatili.
"Kuwaua watu wanaolinda usalama wa raia ni jambo la kusikitisha kwani linakatisha tamaa sana," alisema Babu.
Babu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alisema kuwa wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kuhakilisha watu hao wanatiwa mikononi mwa vyombo vya sheria na jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi kubaini watu waliohusika na tukio hilo.
Mwisho.