Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la polisi mkoani Pwani,linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watu waliohusika kufanya mauaji ya askari wawili wa jeshi hilo pamoja na kuiba silaha mbalimbali kwenye kituo cha polisi Ikwiriri,wilayani Rufiji .
Pia limekanusha uvumi wa kuwa siku ya tukio hilo kuliwa na askari wengine ambao walikimbia kwa lengo la kujihami baada suala ambalo si la ukweli.
Kamanda wa polisi mkoani humo kamishna msaidizi mwandamizi Ulrich Matei alisema kuwa hakuna hadi sasa hakuna mtu aliyekamtwa na msako unafanywa usiku na mchana ili kuhakikisha wanawapata wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Aidha Matei aliitaka jamii kuacha tabia ya kuvumisha mambo yasiyo ya ukweli ama kuibua hoja zisizokuwa za ukweli baada ya matukio mbalimbali kutokea na badala yake anaetaka ukweli anatakiwa kuuliza kwa wahusika ili kupata taarifa za ukweli na si vinginevyo.
Wakati huo huo Mkuu wa wilaya ya rufiji Nurdin Babu amesema emesikitishwa na mauaji ya polisi wawili kwenye kituo cha ikwiriri wilayani humo juzi.
Akizungumza na gazeti hili Babu alisema kuwa tukio hilo ni la kusikitsha na halistahili kuungwa mkono na jamii iliyostaarabika.
"Inasikitisha sana na jambo hili ni ukatili na tunalilaani kwa nguvu zote na tutahakikisha tunawasaka watu waliohusika na tukio hili," alisema Babu.
Babu alisema kuwa wanaendelea kufuatilia na kufanya misako kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ili kubaini waliohusika na tukio hilo la kikatili.
"Kuwaua watu wanaolinda usalama wa raia ni jambo la kusikitisha kwani linakatisha tamaa sana," alisema Babu.
Babu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alisema kuwa wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kuhakilisha watu hao wanatiwa mikononi mwa vyombo vya sheria na jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi kubaini watu waliohusika na tukio hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment