Wednesday, January 7, 2015

WAKAZI CHALINZE WALALAMIKA UKOSEFU WA DAWA KITUO CHA AFYA

Na John Gagarini, Chalinze
WAKAZI wa Chalinze Mjini wameiomba Wizara ya Afya kuangalia upya mgawanyo wa dawa kwenye kituo cha Afya cha Chalinze kwani dawa zinazopelekwa kituoni hapo hazikidhi mahitaji.
Wagonjwa wengi wanaokwenda kuhudumiwa kituoni hapo licha ya kuandikiwa dawa hazipatikani na hutakiwa kununua kwenye maduka ya dawa.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ambaye yuko kwenye ziara ya kukagua masuala ya maendeleo, moja ya wakazi wa Chalinze kitongoji cha Bwiringu aliyejitambulisha kwa jina la Athuman Rashid alisema huduma ya dawa hakuna kabisa.
“Kila ukienda kupata huduma kwenye kituo cha afya Chalinze utahudumiwa vizuri lakini dawa ni mtihani kwani utaambiwa dawa hakuna nenda kanunue kwenye maduka ya dawa,” alisema Rashid.
Rashid alisema kuwa mgawanyo wa dawa kwenye kituo hicho ni mdogo licha ya kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa wengi lakini kinakuwa na upungufu mkubwa wa dawa.
“Ombi letu sisi kwa Wizara ya Afya ni kuangalia namna gani ya kukiwezesha kituo hichi kuwa na mgao mkubwa wa dawa kwani suala la dawa ni tataizo kubwa sana na linatuathiri kwani maduka ya madawa yanauza kwa bei za juu,” alisema Rashid.
Naye Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ni kweli changamoto hiyo ni kubwa sana kwenye kituo hicho na ni vema kituo hicho kikaangaliwa upya.
“Wagonjwa wamekuwa wakilalamika sana juu ya upatikanaji wa dawa kwani kituo hichi kinapewa dawa sawa na vituo vingine vya afya ambavyo havina wagonjwa wengi,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema tayari wameshaongea na Wizara hiyo na stoo ya madawa MSD juu ya kuomba kuongezewa mgao wa dawa kutokana na ukubwa wa kituo kwani mahitaji ni makubwa sana.

Mwisho.    w

No comments:

Post a Comment