Na John Gagarini, Kibaha
WANASIASIA nchini wametakiwa kuwa na hofu ya Mungu na kuacha kutumia
lugha za kusema kuwa watamwaga damu wakati wa kipindi cha uchaguzi.
Hayo yalisemwa na Mchungaji wa kanisa la Gosheni Inland Church lililopo
kitongoji cha Chamakweza wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Jackson Bukelebe,
wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya awali kituo cha kuhudumia
watoto wa wafugaji inayomilikiwa na kanisa hilo.
Mch Bukelebe alisema wao kama kanisa wanataka uchaguzi wa amani na
utulivu na hawataki wanasiasa watakaotuvunjia hali ya amani iliyopo na
kutuletea vurugu kwani hao hawafai na hawastahili kuwa viongozi na wanapaswa
kutumia lugha za ustaarabu na siyo zile zitakazosababisha uvunjifu wa amani
ambayo imedumu kwa kipindi kirefu tangu nchi imepata uhuru,
“Viongozi hawa wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu na si kuwa na roho ya
uharibifu na wakiwa na hofu ya Mungu watakuwa na upendo wa kuwapenda wengine na
wataachana na mambo binafsi bali wataangalia mambo ya watu kwa ujumla,” alisema
Mch Bukelebe.
Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye harambee hiyo mwenyekiti wa
CHADEMA Jimbo la Chalinze Mathayo Torongey alisema kuwa muda wa siasa umekishwa
kinachotakiwa ni kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika ili kuwaondolea
wananchi changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Kuhusu uchangiaji wa fedha kwa ajili ya elimu ni muhimu lakini
kuna baadhi ya jamii ya wafugaji inaona kama elimu siyo jambo la muhimu hivyo
kuwa wagumu kuchangia maendeleo ya elimu,” alisema Torongey.
Torongey ambaye alikuwa mgombe kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Chalinze aliwataka wanajamii ya kifugaji kutokuwa wagumu kuchangia elimu na
kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wao wakike badala yake wawapleke shule.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi moja ya wanafunzi wanaosoma
kwenye shule hiyo Amina Simbilwa alisema kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya
kukosa elimu kutokana na baadhi ya wazazi wao kuhamahama kutafuta malisho.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2014 kwa lengo la kuwapatia elimu ya
awali watoto hao kwani iliyopo iko mbali na wao ambao Kijiji chao ni cha
Wafugaji na ina jumla ya wanafunzi 72.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment