Na John Gagarini,
Ubena
MCHAKATO wa kuifanya
Chalinze kuwa mamlaka ya Mji Mdogo umekumbwa na changamoto kubwa baada ya
makundi mawili ya wakulima na wafugaji kupinga mpango huo.
Makundi hayo ambayo
ndiyo makubwa katika Jimbo la Chalinze yameonekana kutoupokea mpango huo kwa
madai kuwa utawasababisha kushindwa kufanya shughuli za ambazo ndizo
zinazowafanya waweze kuishi.
Changamoto za kupinga
mchakato huo zimebainika wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani
Kikwete kutembelea shughuli za maendeleo.
Akizungumzia changamoto
hizo Ridhiwani alisema Jimbo hilo lilitenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na
wakulima katika mpango bora wa matumizi ya ardhi ambapo kila kundi linakaa
kwenye eneo lake.
“Changamoto hizi
zinakuja kutokana na hali halisi kuwa endapo mamlaka hiyo itakubalika ina maana
kutakuwa na sheria ya kuzuia ufugaji wa mifugo pamoja na kuzuia kilimo huku
makundi hayo yakitegemea shughuli hizo kuendeshea maisha yao,” alisema
Ridhiwani.
Ridhiwani alitoa mfano
kwenye maeneo ya wafugaji ya Vijiji vya Chamakweza ambao wana mifugo zaidi ya
18,000, Lukenge wana mifugo zaidi ya 10,000 na Matuli mifugo zaidi ya 8,000.
“Wafugaji wamesema
kuwa endapo Mamlaka hiyo itapitishwa mifugo yao wataipeleka wapi na wao ufugaji
ndiyo maisha yao kwa ajili ya chakula pamoja na uchumi,” alisema Ridhiwani.
Alisema pia kwa
wakulima nao hawataruhusiwa kulima je wataishije wakati kilimo ndiyo shughuli
yao ya kuendeshea maisha yao ikiwa ni pamoja na uchumi wao na hawana kitu
kingine wanachoweza kukifanya.
“Changamoto hizi
katika kueleka Mji Mdogo zimekuwa ni kubwa na ukiangalia zina uzito hivyo
mchakato huu umesitishwa huku serikali ikiwa inaangalia namna bora ya kufanya
ili kutoathiri maisha ya wananchi,” alisema Ridhiwani.
Aliongeza hata hivyo
wananchi wanapaswa kujiandaa na mabadiliko kwani kila jambo lina wakati wake
ambapo mipango kama hiyo ina lengo la kuwasogezea huduma karibu wananchi.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Ubena
WANANCHI wa Kata ya
Ubena Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani wameuomba uongozi wa Gereza
la Ubena kuwaruhusu kulitumia eneo la pori la Mwidu kwenye barabara ya Morogoro
Chalinze ambalo limekuwa likitumiwa na majambazi kujificha kwa ajili ya kuteka
magari nyakati za usiku.
Ombi hilo lilitolewa
na diwani wa kata hiyo Mrisho Choka mbele ya Mbunge wa Jimbo la Chalinze
Ridhiwani Kikwete ambaye yuko kwenye ziara kutembelea Jimbo hilo kukagua
shughuli za maendeleo.
Choka alisema kuwa
kuwa pori hilo limekuwa likitumiwa na majambazi ambao hujificha kisha kutega
magogo barabarani na kusababisha ajali kisha kufanya uhalifu kwa kutumia silaha
mbalimbali.
“Eneo hili limekuwa
hatarishi kwa magari hasa nyakati za usiku ambapo kumekuwa na matukio mengi ya
utekwaji wa magari ambayo kabla ya kutekwa husababishiwa ajali kwa kuwekewa
magogo hivyo tunauomba uongozi wa gereza kuturuhusu tutumie eneo hilo ili
kuzuia vitendo hivyo,” alisema Choka.
Alisema kuwa endapo
wananchi watalitumia eneo hilo itasaidia kupunguza vitendo hivyo kwani kwa ambapo
kwa sasa majambazi hao wanafanya wanavyotaka kutokana na eneo hilo kuwa pori.
Aidha alisema kuwa wiki
iliyopita magari manne yalitekwa na katika kukabiliana na uhalifu katika eneo
hilo wamekuwa wakifanya doria na askari polisi lakini hata hivyo majambazi hao
wamekuwa wakiwategea na kutekeleza uhalifu.
Kwa upande wake
Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ombi lao atalipeleka kwenye vyombo husika ili
lifanyiwe kazi ili kuondokana na vitendo hivyo ambavyo vimekithiri katika eneo
hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment