Sunday, January 4, 2015

WANANCHI WAMLALAMIKIA MWEKEZAJI

Na John Gagarini, Chalinze
WAWEKEZAJI kwenye Kijiji cha Changarikwa wametakiwa kufuata taratibu za kisheria ili kuondoa migogoro baina yao na wananchi.
Hayo yalisemwa na mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho kwenye ziara yake ya maendeleo jimboni humo.
Ridhiwani alitoa ushauri huo kufuatia wananchi hao kulalamika dhidi ya moja ya wawekezaji kwenye kijiji hicho kuchukua eneo lenye ukubwa wa hekari 500 na kutotimiza ahadi za kuwasaidia kwenye huduma za kijamii.
Moja ya wananchi wa Kijiji hicho Bakary Hatibu alisema kuwa mwekezaji huyo wakati anaomba ardhi hiyo moja ya masharti waliyokubaliana naye ni kuwajengea shule, zahanati na trekta lakini sasa ni miaka 15 hakuna hata kimoja alichotekeleza.
“Tumekuwa tukipata tabu kwani wakati mwingine tnazuiwa kupita kwenye maeneo amabayo yanamilikiwa na mwekezaji,” alisema Hatibu.
Kwa upande wake Mbunge huyo alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi dhidi ya wawekezaji kujipatia maeneo pasipo kutimiza masharti ya maombi ya ardhi.
“Jambo la kushangaza ni mwekezaji kupewa hekari 500 na kijiji jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya ardhi namba 5 ya mwaka 1999 inayosema kuwa kijiji kinauwezo wa kumpa mwekezaji si zaidi ya hekari 50,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa kama wameona mwekezaji hafai kwani wao ndiyo waliompa ardhi wanauwezo wa kumnyanganya kwa kufuata taratibu za kisheria endapo wataona ameshindwa kutekeleza ahadi wakati anaomba ardhi.
“Mnauwezo wa kumuondolea umiliki endapo atakiuka masharti kwani huo ni mkataba na endapo atakiuka masharti unaweza kuvunjika na ardhi ikarudishwa kwa wanakijiji,” alisema Ridhiwani.
Alisema ni vema wawekezaji wakatekeleza tatatibu ili kuwa na ushirikiano na wananchi ambao wanatoa ardhi yao ili nao wanufaike nayo.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment