Friday, January 23, 2015

ASKARI ALIYEUAWA AAGWA

Na John Gagarini, Kibaha
KONSTEBO wa Polisi aliyeuwawa na majambazi waliovamia kituo cha Polisi cha Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani Judith Timoth (32) juzi aliagwa mjini Kibaha na mamia ya watu wakiwemo askari wenzake aliowahi kufanya nao kazi kabla ya kuhamia Rufiji.
Mwili huo uliagwa kwenye hospitali ya Polisi mkoa na kuongozwa na ofisa wa jeshi hilo Thabita Makaranga, kwa safari ya kuelekea mkoani Mbeya kwa ajili ya mazishi  na kuliibua simanzi kubwa kwa watu waliohudhuria tukio hilo na kuvuta hisia na vilio kutoka kwa waombolezaji.
Akiongoza kwenye ibaada ya kumwaga marehemu mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Maili Moja alikokuwa akisali kabla ya kuhamia wilayani Rufiji, Josephine Urio alisema kuwa watu wanapaswa kujiandaa kwa kusali muda wote kwani hawajui siku wala wakati watatwaliwa.
“Wanadamu wanapaswa kuacha roho za mauaji kama hao waliofanya mauaji hayo kwani hawako salama kama wanavofikiri Mungu atawapa pigo kama walivyotoa roho za watu wasiokuwa na hatia na watu wenye uovu waache njia hizo,” alisema Urio.
Akisoma wasifu wa marehemu moja ya wafanyakazi wenzake Robert Munisi alisema kuwa jeshi hilo litapambana na watu wote waliohusika na tukio hilo na kuliomba kanisa lilisaidie polisi kukabiliana na wahalifu hao na watasimamia amri kumi za Mungu.
Munisi alisema marehemu alizaliwa mkoani Mbeya na kupata elimu ya Msingi na Sekondari na kupata mafunzo ya sheria mkoani Mbeya kisha kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Polisi huko Moshi kuanzia Oktoba 30 mwaka 2004 na kuhitimu Fabruari 25 mwaka 2005 pia alipata mafunzo mbalimbali yakiwemo ya Upelelezi.
Aidha amesema marehemu kabla ya umauti alikuwa akisoma masomo ya Sociology mwaka wa pili Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ameacha mtoto mmoja wa kiume aitwaye Bryan.Marehemu alivamiwa juzi akiwa kazini na mwenzake majira ya saa 8 usiku na kushambuliwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi waliokuwa na silaha na kufariki dunia yeye na mwenzake Koplo Edger Milinga.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAZAZI wa shule ya Msingi Juhudi kata ya Visiga wilayani Kibaha wameulalamikia uongozi wa shule hiyo kwa kuwarudisha watoto wao wanaojiunga darasa la kwanza kwa kushindwa kulipa kiasi cha shilingi 15,000 kwa ajili ya kuwaandikisha.
Moja ya wazazi hao Mabeka Mabeka akizungumza kwenye kikao cha wazazi alisema kuwa wanashangazwa na taratibu za kuwatoza kiasi hicho licha ya kuwa serikali imekataza michango hiyo na kusababisha wazazi kuwa kwenye wakati mgumu kupata fedha hizo.
Mabeka alisema kuwa wanaushangaa uongozi wa shule hiyo kwa  kuwaandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza kwa kututoza fedha hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwani serikali ilitamka kuondoa michango kwa wanafunzi wanaoanza ili kuondoa kero kwa wazazi.
“Michango hii ni kikwazo kwa wazazi kuwapeleka watoto shule huku serikali ikitaka watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule waandikishwe ili waweze kupata elimu ya msingi,” alisema Mabeka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Theobad Rwegalulila alikiri kuwepo kwa jambo hilo na kusema kuwa limekuwa changamoto kubwa kwa wazazi ambao wamekuwa wakilalamika kupinga malipo hayo ili watoto waweze kupata fursa ya kujiunga na darasa la kwanza.
Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo Hawa Mgogolo alikiri kuwepo kwa michango hiyo na kusema kuwa walikubaliana na wazazi kwenye kikao cha wazazi mwaka 2012 lakini anashangaa wazazi hao kuanza kulalamika wakati wao wenyewe walikubali mchango huo.
Mgololo alisema kuwa ni kweli walikuwa wakiwatoza fedha hizo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na fedha hizo zinatumika kununulia vitu mbalimbali kama vile chaki, madaftari ya maendeleo na vifaa mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi hao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SHULE ya Msingi ya Maili Moja iliyopo wilayani Kibaha inakabiliwa na ubovu wa madarasa ambayo yanaweza kuanguka wakati wowote hali ambayo inahatarisha usalama wa wanafunzi na walimu kwenye shule hiyo.
Kutokana na ubovu huo madarasa matano kati ya 11 ndiyo yanayotumika ambapo wanafunzi wanasoma zaidi ya wanafunzi 150 hadi 200 kwenye darasa moja.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikoa cha dharura cha wazazi kuzungumzia ubovu wa madarasa hayo, mwalimu mkuu wa shule hiyo Reginald Fanuel alisema kuwa madarasa hayo yamebomoka vibaya.
“Madarasa hayo yako kwenye hali mbaya na wakati wowote yanaweza kuanguka na kusababisha maafa kwa wanafunzi na walimu endapo hazitachukuliwa hatua za haraka za kunusuru hali hiyo ambayo sasa imefikia hatu mbaya,” alisema Fanuel.
Fanuel alisema kuwa kutokana na hali hiyo wanaomba msaada wa kusaidiwa ujenzi ili kunusuru hali hiyo ambayo ni hatari kwa wanafunzi na walimu wanaotumia madarasa hayo pia mlundikano kwenye madarasa mazima ni mkubwa sana.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya shule Said Chitenje alisema kuwa tatizo hilo lilianza muda mrefu ambapo wamekuwa wakiakabiliana na hali hiyo kwa kuchangisha michango wazazi lakini michango imekuwa ikisusua.
“Kweli hali ni mbaya na kutokanana hali kuzidi kuwa mbaya tumekubaliana na wazazi kuwa kila mzazi ambaye ana mwanafunzi shuleni hapa atoe kiasi cha shilingi 5,000 kwa ajili ya kufanya ujenzi wa madarasa hayo,” alisema Chitenje.
Naye diwani wa kata ya Maili Moja Andrew Lugano alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya ujenzi wa madarasa hayo yaliyoharibika ili kuwanusuru wanafunzi hao.
Lugano alisema kuwa wazazi hao waliomba wakutane na mkurugenzi wa halmashauri ya Mji ili wazungumzie suala hilo na namna ya kuwez akukabiliana na tatizo hilo na kuwaomba watu na wafadhilimbalimbali kujitokeza kusaidia ujenzi wa majengo hayo.

Mwisho.  

No comments:

Post a Comment