Monday, January 26, 2015

HALMASHAURI YA MJI KUJENGA SOKO NA STENDI VYA KISASA

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha inatarajia kuanza mradi mkubwa wa ujenzi wa Soko la kisasa pamoja na Stendi utakaogharimu kiasi zaidi ya shilingi bilioni 20 kuanzia Februari mwaka huu.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Adhu Mkomambo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi na kusema kuwa taratibu za mwisho zinakamilika kuanza ujenzi huo.
Mkomambo alisema kuwa ujenzi huo wa soko na setndi vitakuwa mkombozi kwa wananchi wa Kibaha na mkoa mzima wa Pwani kutokana na kukosa vitu hivyo kwa muda mrefu.
“Pale kuna soko na stendi lakini havina hadhi ya Mji hivyo kupitia benki ya uwekezaji (TIB) tutajenga vitu hivi kwa lengo la kuboresha mji na kuleta maendeleo kwa wananchi wa wilaya ya Kibaha,” alisema Mkomambo.
Aidha alisema kuwa vitu hivyo ni moja ya vyanzo vya mapato ya Halmashauri hivyo ujenzi wake utazingatia ubora na viwango ili kuwa na hadhi kwani soko lililopo halina ubora kulingana na mji wa Kibaha
“Mbali ya miradi hiyo ambayo itaanza kwa pamoja pia Halmashauri itaendelea na miradi yake ya ujenzi wa barabara na uboreshaji wa sekta mbalimbali za jamii ili huduma ziweze kuwa bora,” alisema Mkomambo.
Alibainisha kuwa wataendeleza ushirikiano kati ya Halmashauri yake wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuendelea kuuboresha mji huo unaoelekea kuwa Manispaa.
Mwisho.  




  

No comments:

Post a Comment