Na John Gagarini, Kibaha
MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani Zakia Meghji
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za (CCM) kutimiza miaka 38 zitakazofanyika
Kata ya Visiga wilayani Kibaha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha
katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa sherehe hizo
zitaadhimishwa kwa shughuli mbalimbali za kuimarisha chama ambazo tayari
zilishaanza tangu Januari 26 kwenye kata ya Mkuza.
Mdimu alisema kuwa Meghji ambaye ni Mbunge na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu (MNEC) atahitimisha sherehe hizo Februari Mosi kwenye kata hiyo
ambayo imepewa upendeleo kutokana na chama hicho kuchukua mitaa yote saba
kwenye uchaguzi wa wenyeviti wa Mitaa uliofanyika hivi karibuni.
“Wakati wa sherehe hizi kutakuwa na shughuli mbalimbali kama
vile kukagua uhai wa chama ngazi ya mashina, matawi, kata wilaya pamoja na
uhakiki wa daftari la uanachama ili kuwa na takwimu sahihi za wanachama,” alisema
Mdimu.
Aidha alisema kuwa kazi nyingine ni kufanya mikutano ya
kuhamasisha wanachama kujitokeza kujiandikisha katika daftarai la wapiga kura
msisitizo ukiwa ni kwa wananchi wote wenye sifa kujiandikisha upya hata wale
wenye vitambulisho vya kupiga kura miaka iliyopita.
“Tunatarajia Halmashauri kuu za kata zitafanyika kwenye kata hizo
za Kibaha Mjini ambazo ni 14 ambapo wajumbe wa mkoa watasambaa kwenye kata hizo
kabla ya mkutano mkubwa wa hadhara wa kuhitimisha sherehe hizo ambapo Meghji
ndiye atakayefunga akiwa ndiyo mgeni rasmi,” alisema Mdimu.
Aliwataka wanaccm kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kwenda
kumsikiliza mlezi wa chama siku hiyo ili waweze kuimarisha chama katika maeneo
yao pia kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kuhakikisha chama kinapata
ushindi mkubwa wa kishindo huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisema Umoja ni Ushindi
(Katiba Yetu, Taifa Letu).
Mwisho.
No comments:
Post a Comment