Na John Gagarini, Kibaha
VYAMA vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) wilayani Kibaha mkoani Pwani vimetakiwa kuweka mifuko kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye shida mbalimbali wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu na watoto waishio kwenye mazingira hatarishi.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) Kibaha Mjini Rugemalila Rutatina wakati wa kuwakabidhi vifaa vya shule wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waishio kwenye mazingira hatarishi kwenye mtaa wa Kwa Mfipa wilayani humo vilivyotolewa na chama cha kuweka na kukopa cha Upendo cha mtaa huo.
Rutatina alisema kuwa ili jamii iweze kunufaika na vyma hivyo ni vema vikawa na mifuko hiyo ili kuwezesha makundi hayo ambayo hayana msaada wowote kutokana na hali zao.
“Ni vema vyama hivyo vikatenga fedha kidogo kwa ajili ya kuisaidia jamii kwani SACCOS zimeonekana kuwa ni msaada mkubwa kwa wanachama ambao wengi wao ni wajasiriamali kwa kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa kuwasaidia watu wenye shida ni ibaada ambayo inafanywa na mtu anayetoa hivyo Mungu humbariki na kumuongezea kwa kuwa amewajali wale wasio na uwezo kama vile wazee, wajane, yatima na wenye ulemavu.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Kibaha Said Nangurukuta alisema kuwa chama hicho kimeonyesha mfano kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto waishio kwenye mazingira hatarishi hivyo kuwasaidia walezi wa watoto hao.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Faustina Kayombo alisema kuwa watoto wenye mahitaji maalumu wamekuwa wakiongezeka kila mara kutokana na utengano wa wazazi au mazingira magumu ya kwenye familia na kuwapatia vifaa hivyo chama hicho kimeisaidia serikali kubeba mzigo wa kuwasaidia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira hatarishi na kuwataka watu wenye uwezo kuwasaidia watoto kama hao.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mwajuma Teya alisema kuwa mbali ya chama chao kukopesha kimetenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanoishi kwenye mazingira magumu ambapo kimekuwa kikitoa vifaa mbalimbali pamoja na kuwalipia ada baadhi yawanafunzi.
Teya alisema kuwa mbali ya mafanikio hayo pia wanakabiliwa na changamoto ya udogo wa mtaji wao hali inayosababisha mzunguko wa kukopeshana kutokwenda kwa wakati, jumla ya wanafunzi 25 walipewa misaada hiyo na kinajumla ya wanachama 30 ambao ni wajasiriamali wanaojihusisha na ufumaji, ushonaji, ulimaji wa bustani, utengenezaji wa sabuni na kukopeshana na kilianzishwa mwaka 2012.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment