Thursday, February 26, 2015

WAHARIRI NA HALI YA HEWA

Na John Gagarini, Kibaha
WAHARIRI hapa nchini wametakiwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa kuhakikisha vyombo vya habari vinatoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati kwa usahihi na kwa lugha rahisi kupunguza majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa kwa ajili ya kulinda maisha ya wananchi wa Tanzania na mali zao.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mkurugenzi wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania Dk Agnes Kijazi wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wahariri wa vyombo vya habari na wadau wa sekta mbalimbali kuhusu utabiri wa mvua za msimu wa Machi na Mei 2015.
Dk Kijazi alisema kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa muda mrefu sasa imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha kuwa inaboresha huduma zake kwa kuongeza wigo wa kuwafikishia wananchi taarifa na tahadhari za hali ya hewa kwa wakati na hivyo kutumika pamoja na mambo mengine kuweka mikakati ya kupunguza athari za majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa ili kulinda maisha ya watu na mali zao.
“Tunaomba wahariri kwa kushirikiana na mamlaka kuweza kutoa taarifa sahihi juu ya hali ya hewa kwa wananchi ili waweze kuweza kujua jinsi gani ya kukabiliana na majanga yakiwemo ya mvua au madhara mengine yanayotokana na hali ya hewa,” alisema Dk Kijazi.
Dk Kijazi alisema kuwa kwa sasa Mamlaka iko katika maandalizi ya kutoa utabiri wa msimu wa mvua za masika (Machi-Mei) utabiri ambao wanatatarajia kuutoa tarehe tatu mwezi wa tatu mwaka huu.
”Ushauri wa kisekta ni muhimu sana katika kuhakikisha kuwa utabiri utakaotolewa utasaidia kupanga mipango mbalimbali ya sekta husika na kupunguza athari ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa,” alisema Dk Kijazi.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha hilo linafanikiwa hutegemea kwa kiasi kikubwa huduma na taarifa sahihi za hali ya hewa zinazotolewa kwa wakati muafaka.
Mkurugenzi huyo wa mamlaka ya hali ya hewa nchini alisema taarifa za hali ya hewa hutumika katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika kufanikisha shughuli za sekta mbalimbali kama vile Usafiri wa anga na kwenye maji, Nishati, Afya, Utalii, Misitu, Mazingira, Mifugo, Uvuvi, Usimamizi wa mipango miji, Umwagiliaji, Utalii, Kilimo na usalama wa chakula, Mipango ya shughuli za kijamii na kiuchumi, pamoja na huduma nyinginezo nyingi.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment