Na John Gagarini, Bagamoyo
WAZAZI wa watoto wa wafugaji
kwenye Kijiji cha wafugaji cha Chamakweza kata ya Pera wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani wametakiwa kuwapeleka shule watoto wao wakike waliofaulu kwenda
kidato cha kwanza mwaka huu kwenye shule mbalimbali wilayani humo.
Hayo yalisemwa na mjumbe wa kamati ya wafugaji ya kata ya
Pera, Yohana Kipojo, wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya awali
ya Ekishomi inayomilikiwa na kanisa la Gosheni Inland lililopo kwenye kitongoji
cha Chamakweza.
Kipojo alisema kuwa lengo la kuwahimiza wazazi hao kuwapeleka
shule watoto wao wakike waliofaulu ni kuhakikisha wanapata elimu ya juu na
kuachana na tabia ya kuwaoza huku wale wakiume wakipatiwa elimu.
“Tunatoa hadi Machi 30 endapo mfugaji yoyote kama hajampeleka
shule mtoto wake wakike aliyefaulu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake
hivyo lazima wahakikishe wanawapeleka ili wapate elimu,” alisema Kipojo.
Aidha alisema kuwa elimu ni haki kwa watoto wote na si watoto
wa jinsia moja ambapo baadhi ya wazazi hawawapeleki watoto wakike shule na
kuwapelendelea wakiume jambo ambalo linalosababisha watoto wakike kukosa elimu.
Kwa upande wake mlezi wa shule hiyo Rehema Ishengoma alisema
kuwa kuwaoza watoto wadogo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu
ambayo iko kikatiba.
Ishengoma amesema kuwa wanafunzi wakike wanaoozwa kwenye umri
mdogo wanapata mateso makubwa hasa wakati wa kujifungua kwani miili yao bado
haijawa na uwezo wa kujifungua na endapo mtoto wakike atapata elimu atajua haki
zake na kuweza kuyatawala maisha yake.
Naye Mchungaji wa Kanisa hilo Jackson Bukelebe alisema kuwa
lengo la kujenga shule hiyo ya awali ni kuwasogezea shule karibu watoto
wawafugaji kwani shule zilizopo ziko mbali nao.
Mch Bukelebe alsema kuwa eneo hilo halina shule jambo ambalo
linawafanya wanafunzi ambao ni wadogo kuwa na wakati mgumu kwenda shule ambapo
kitongoji hicho hakuna shule.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment