Sunday, February 22, 2015

RIDHIWANI ATOA MSAADA WA CHAKULA KWA WAHANGA WA MVUA

 Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, Idd Swala kushoto akimkabidhi moja ya wahanga wa mvua ambazo ziliharibu nyumba za wakazi wa Chalinze hivi karibuni.  

 Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Idd Swala kushoto akimkabidhi vyakula moja ya wananchi ambao walipata janga la mvua ambayo iliharibu nyumba za wakazi wa Chalinze.

Na John Gagarini, Chalinze
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani amewasaidia chakula watu 131 ambao nyumba zao ziliharibika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha hivi karibu.
Mvua hizo zilinyesha Februari 16 kwenye Kijiji cha Msoga na Februari 19 mwaka huu na kusababisha watu 11 kujeruhiwa huku nyumba zaidi ya 100 zikibomoka hali iliyosababisha wengine kuhifadhiwa na majirani zao.
Akitoa vyakula hivyo kwa niaba ya Mbunge huyo wa Jimbo la Chalinze, katibu wake Iddi Swala alisema kuwa vitu hivyo ni kuwawezesha wananchi hao angalau waweze kujipatia mlo huku mipango mingine ya kuwasaidia ikiendelea.
“Mbunge ameamua kujitolea vyakula hivyo ambavyo ni mchele kilogramu tano, maharage kilogramu tano,  unga wa sembe kilogramu tano na sukari kilogramu mmoja ili kuwasidia katika kipindi hichi kigumu hivyo ameona awasaidie,” alisema Swala.
Swala alisema kuwa anawaomba watu wengine nao waweze kuwasaidia wahanga hao kwa hali na mali ili waweze kupata huduma zingine za kiutu.
Naye mmoja ya waathirika hao Ramadhan Madewa ambaye mbali ya nyumba yake kubomoka pia alijeruhiwa usoni alisema kuwa anashukuru msaada huo kwani utawasaidia wakati wakiendelea kuangalia namna gani watakavyojipanga kurjesha makazi yao katika hali ya kawaida.
Kwa upande wake diwani wa Bwiringu Nasa Karama alimshukuru Mbunge huyo kwa kujitolea kuwapatia chakula waathirika wa mvua hizo ambazo kwenye kata yake jumla ya nyumba 84 ziliharibiwa na mvua hizo.
Naye mtendaji wa kata ya Msoga Hassan Mtamani alisema kuwa msaada huo utawasaidia waathirika wa janga hilo kwa kipindi hichi ambacho wanaendelea kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea.
Mwisho.



    

No comments:

Post a Comment