Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesema kuwa
mkoa utaweka mazingira mazuri kwa wanamichezo ili waweze kufanya vema kwenye
michuano mbalimbali ya ndani na ile ya Kitaifa ili kuendeleza vipaji.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akipokea kombe la ushindi
wa tatu kwa timu ya mpira wa Pete ya Ruvu JKT Mlandizi wilayani Kibaha ambayo
ilishika nafasi hiyo kwenye mashindano ya Taifa yaliyofanyika mwaka jana.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa ofisi yake itahakikisha kuwa michezo
ndani ya mkoa inasonga mbele kwa ili kuleta mafanikio kwenye sekta hiyo ambayo
imekuwa ikiuletea sifa kubwa mkoa wa Pwani ambapo timu za soka za Ruvu Stars na
Ruvu Shooting zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara zinatokea kwenye mkoa
huo.
“Fedha ni changamoto kubwa kwenye sekta ya michezo lakini
tutajitahidi kwa hali na mali kw akushirikiana na wadau wa michezo kuhakikisha
timu zilizondani ya mkoa wetu zinafanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ya
kimkoa na kitaifa ili kuendeleza sifa nzuri ya michezo iliyopo kwa sasa,”
alisema Mhandisi Ndikilo.
Aidha alisema kuwa
licha ya mkoa kuwa na changamoto kubw aya ukosefu wa fedha lakini mkoa umekuwa
ukipiga hatua kubwa na kuufanya kuweza kutamba kwenye nyanja mbalimbali ikiwa
ni pamoja na timu ya mpira wa soka la wanawake kushika nafasi ya pili kwenye
mashindano ya Taifa yaliyomaliziki hivi karibuni .
Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la michezo la mkoa
ambaye ni katibu Tawala wa mkoa huo Mgeni Baruhani alisema kuwa kwa bahati
mbaya hakuna fedha zinazotengwa kwa ajili ya michezo lakini ofisi ya mkoa
imekuwa ikisaidia michezo kwa kuzichangia timu na vilabu vya mkoa ili vishiriki
kwenye michuano mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha mpira wa Pete mkoani
Pwani Fatuma Mgeni alisema kuwa timu hiyo kwa sasa iko kwenye maandalizi ya
mashindano ya Afrika Mashariki itakayofanyika Zanzibar kuanzia mwezi Machi
mwaka huu na kuwaomba wadau kujitokeza kuisaidi ili iweze kufanya vizuri kwenye
michuano hiyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment