Monday, February 23, 2015

SIMBA ISITAFUTE MCHAWI TATIZO NI

Na John Gagarini, Kibaha
TIMU ya soka ya Simba imetakiwa isimtafute mchawi kutokana na matokeo mabaya inayoyapata uwanjani kwani hali hiyo inatoka na usajili ambao haukuwa mzuri kwa kutosajili wachezaji wenye uzoefu.
Wachezaji wengi waliosajiliwa ni wale ambao wanahitaji uzoefu wa muda mrefu kabla ya kutegemewa na timu ya Simba ambayo ni timu kubwa hapa nchini.
Akizungumza na gazeti hili msemaji wa Tawi la Simba wilayani Kibaha mkoani Pwani lililopo Kwa Mfipa maarufu kama “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa wachezaji waliyopo wengi ni chipukizi ambao walipaswa kuwa na wachezaji wenye uzoefu.
“Timu ni nzuri lakini wachezaji wengi ni chipukizi na hawana uzoefu wa michezo mikubwa kama hii ya ligi kuu ambayo ni ngumu na inahitaji uzoefu mkubwa ambapo wachezaji hawa wanashindwa kumudu dakika 90 za mchezo,” alisema Lardhi.
Lardhi alisema kuwa hakuna haja ya kumtafuta mchawi na kutuhumiana kuwa kuna kundi fulani linahujumu timu hiyo si kweli kwani hali halisi inaonekana kuwa wachezaji wa Simba wengi hawawezi kumudu mikimikiki ya ligi.
“Hakuna cha Simba Ukawa wala nini bali timu yetu inashindwa kuhimili vishindo ni dhahiri kuwa kamati ya Usajili msimu huu imesajili timu ya Vijana wadogo wengi ambao walitakiwa kusaidiana na wachezaji wenye uzoefu,” alisema Lardhi.
Aidha alisema kwa upande wa kocha hawezi kulaumiwa kwani uwezo wake ni mzuri na timu aliikuta hata hivyo amejitahidi kuhakikisha timu inacheza vizuri tatizo ni kukosa wachezaji wazoefu.
Alibainisha kuwa huu ni msimu wan ne timu ya Simba haiku vizuri wanaifanya kama timu ya majaribio ligi kuu ni ngumu na inahitaji wachezaji wenye uzoefu mkubwa hivyo viongozi wasitoe lawama zozote.
Mwisho.  
Na John Gagarini, Kibaha

TIMU ya soka ya Kiluvya United ya Mkoani Pwani imefanikiwa kupanda daraja la kwanza baada ya kutoka sare ya goli 1- 1 na timu ya Mshikamano ya Jijini Dar es Salaam kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Ruvu JKT Mlandizi wilayani Kibaha.

Kiluvya United imefanikiwa kupanda licha ya kuwa bado ina michezo miwili mkononi kwenye mashindano ya ligi daraja la Pili  Taifa ilianza mbio zake za kuwania kupanda daraja tangu mwaka jana.

Katika mchezo wa huo ulioifanya timu hiyo kupanda hadi daraja la Kwanza kutoka la pili ulishuhudiwa na mashabiki wengi toka timu hizo mbili ulikuwa na ushindani mkubwa na kufanya kuwa na mvuto uliowafanya mashabiki kupata burudani ya nguvu.


Mashabiki wa United walifurahia matokeo hayo ambayo yameipandisha timu hiyo ya mkoa wa Pwani ambayo imepania msimu ujao kupanda ligi kuu ya Voda Com ili kuungana na timu za Ruvu Shooting na Ruvu Stars.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo kwisha kocha mkuu wa United Yahaya Issa alisema kuwa kwa kwa sasa kikosi chake kina jumla ya pointi 20 na kwamba kimebakiza michezo miwili, Mshikamo ikiwa na pointi 13 ikifuatiwa na Abajalo ikiwa na pointi 12 zote za Jijini Dar es Salaam.

‘Ndugu waandishi kwanza kabisa napenda kumshukuru mungu kwa timu yangu kupanda daraja la kwanza na hii yote nikutokana na juhudi za wachezaji na uongozi mzima wa United pamoja na mwamko wa mashabiki wa Pwani ndiyo waliofanikisha kupanda daraja,” alisema Issa.

Issa alisema kuwa kwa sasa wao ndiyo vinara kwa pointi 20 na bado wana michezo miwili dhidi ya Abajalo na Cosmo hivyo hakuna timu yoyote ambayo itaweza kufikia pointi zao hata kama wakishinda michezo yote.

Naye Mkrugenzi wa timu hiyo ya United Edward Mgogo “Eddo Master” alisema kwamba ndoto yao kubwa ni kuhakikisha timu hiyo inafika mbali ili kuweza kushiriki katika ligi kuu ya Tanzaania Bara.

Aidha alitoa wito kwa wadau mbali mbali na mashabiki wa Mkoa wa Pwani kuiunga mkono timu yao ili kuweza kutimiza azama yao ya kuweza kufika mabli na hatimaye katika siku zijazo iweze kushiriki hata michuano mbali mbali ya Kimataifa.

Kikosi hicho ambacho kwa sasa kimeacha gumzo ya hali ya juu kutokana na wachezaji wake kuonyesha kandanda la aina yake siku ya jumamosi kinatarajia kushuka dimbani kumenyana na timu ya Abajalo katika nyasi za uwanja wa Karume Jijiji Dar es Salaam ikiwa kama kumalizia michezo yake miwili ya mzunguko wa mwisho.

  Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani limepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 12 ikiwa ni pamoja na wateja wake kujiwekea nguzo kinyemela na kujiunganishia nyaya za umeme zenye urefu wa mita 2000.

Shirika hilo liliweza kubaini kuwa kuna baadhi ya wateja wake ambao wameamua kujiunganishia umeme kwa kujiwekea nguzo pamoja na nyaya za umeme zenye urefu huo kinyume cha utaratibu.

Hayo yalisemwa na ofisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Pwani Henry Byarugaba na kusema kuwa tukio hilo la kuhujumu miundombinu hiyo  limetokea katika eneo la  Matumbi Wilayani Bagamoyo.

“Shirika iliweza kubaini kuna baadhi ya wateja wake ambao wameamua kujiwekea nguzo kinyemela pamoja na nyaya za umeme zenye urefu wa mita 2000 bila ya TANESCO ambao ndiyo waunganishaji wa umeme kufahamu jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” alisema Byarugaba.

Byarugaba alisema kuwa Shirika limepata hasara kuwaba kutokana na kuwakuta wateja wawili kujiunganishia nguzo saba bila ya TANESCO kufahamu kwani mbali ya hujuma hiyo pia ni hatari sana maana miundombinu hiyo inahujumiwa na watu wachache hivyo hawataweza kuvumilia hali hiyo.

“Baada ya kukuta nguzo hizo zimewekwa hatua ambazo tulizichukua ni kuziondoa nguzo zote saba kwani hazikuwa zimezingatia taratibu katika uwekaji wa miundombinu hiyo hivyo hazikuwa halali kuwepo katika eneo hilo,” alisema Byarugaba.

Aidha alisema kuwa kubainika kuwepo kwa nguzo hizo ni kutokana na juhudi za makusudi ambazo zinafanywa na wafanyakazi wa Shirika hasa nyakati za usiku na mchana ili kuweza kuangalia miundombinu yake na kuwabaini wateja ambao wamekuwa wakivunja sheria kwa kujiunganishia  nguzo wenyewe.

“Hivi kweli jamani mtu anafanya maamuzi ya kuamua kuhujumu miundombinu yetu bila ya woga wowote ule hii ni hatari sana na ndio maana sisi jukumu letu ni kuhakikisha miundombinu yetu inakuwa katika hali ya usalama, na siyo wateja wetu kujichukulia maamuzi wao wenyewe bila ya kuwaona wahusika kutoka,”alisema Byarugaba.

Ofisa usalama huyo wa TANESCO alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa hali hiyo wameshapeleka taarifa polisi ili kuweza kuwasaka watuhumiwa wote ambao wamehusika katika tukio hilo la kujiunganishia nguzo na nyaya kiholela ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Alibainisha kuwa kwa sasa bado wanendelea kufanya uchunguzi wa  kina ili waweze kuwafahamu ni watu gani ambao wamehusika katika zoezi hilo la kuwawekea wateja hao nguzo na nyaya bila ya uongozi  wa Shirika kufahamu lolote juu ya tukio hilo.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment