Na John Gagarini, Kibaha
JAMII mkoani Pwani imetakiwa kusimamia malezi ya watoto wadogo na kuacha kuwafanyia vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikiwaletea athari kubwa katika makuzi yao.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mratibu wa mtandoa wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Watoto wadogo Tanzania (TECDEN) mkoa wa Pwani Feliciana Mmasi wakati wa mafunzo ya Sera ya Haki ya Mtoto Tanzania kwa walimu na walezi wa vituo vya watoto wadogo wilayani Kibaha.
Mmasi alisema kuwa baadhi ya watoto mkoani Pwani wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na ndugu wa karibu hata baadhi ya wazazi hasa wale wa kike.
“Kumekuwa na vitendo vingi vya ukatili ambavyo watoto wadogo wamekuwa wakifanyiwa huku baadhia ya jamii ikiviangalia na kuvifumbia macho hivyo kuendeleza unyanyasaji kwa watoto wadogo,” alisema Mmasi.
Aidha alisema kuwa baadhi ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto wadogo ni pamoja na ubakaji, vipigo, kuuwawa, kunyimwa chakula na vitendo ambavyo ni kinyume cha haki za binadamu.
“Utafiti uliofanyanyika mwaka 2010 kuhusu hali ya ukatili nchini umeonyesha kuwa watoto 6 kati ya 10 wamefanyiwa vitendo vya ukatili katika mikono ya ndugu na jamaa wa karibu huku mtoto mmoja kati ya wawili wamefanyiwa vitendo vya ukatili na walimu,” alisema Mmasi.
Kwa upande wake ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Joannes Bigirwamungu alisema kuwa wamekuwa wakiunda timu kwenye ngazi mbalimbali kwa ajili ya kupokea taarifa za vitendo vya ukatili na kuripoti kwenye vyombo vya sheria.
Bigirwamungu aliitaka jamii kutoa taarifa za baadhi ya watu wanaofanya vitendo vya ukatili kwa watoto ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika wa matukio hayo ambayo yanawanyima haki watoto.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment