Na John Gagarini, Wami
MAMLAKA ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) imekanusha uvumi kuwa mashine za
uzalishaji wa maji zimeuzwa nchini Kenya hali ambayo imesababisha maji kukatika
mwezi mzima.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake Meneja wa
mamlaka hiyo Injinia Christer Mchomba alisema kuwa uvumi huo si wa kweli kwani
mashine zote zipo na zinatumika kama kawaida.
Injinia Mchomba
alisema kuwa uvumi huo umekuja kutokana na maji kutokutoka kwa sababu ya
mashine hizo kuvuta uchafu ambao umesababisha kuziba na kushindwa kupitisha
maji.
“Tatizo la maji
kushindwa kutoka hakutokani na mashine kuuzwa bali ni kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha kwenye mkoa wa Morogoro ambapo ndiyo chanzo cha mto Wami
na kusababisha uchafu kuwa mwingi na mashine kuziba na kuharibika hivyo maji
kushindwa kutoka,” alisema Injinia Mchomba.
Alisema kuwa tatizo ni
tekeo ambapo kwa sasa linawekwa ambalo likikamilika litasaidia kuchuja uchafu
tofauti na ilivyokuwa mwanzo kwani maji zamani yalikuwa masafi na yalikuwa
hayana uchafu.
“Uchafu huo unatokana
na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na watu wanaojihusisha na uchimbaji
wa madini, kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji na uchafuzi wa mazingira
hivyo kusababisha uchafu mwingi kuja na maji,” alisema Injinia Mchomba.
Alisema kuwa ukarabati
wa mashine hizo unaendelea ambapo umefikia asilimia 85 na baada ya miezi miwili
au mitatu tatizo la ukosefu wa maji Chalinze litakuwa ni historia
“Tuna mitambo 30 na
mingine mipya hata hatujaifungua iweje watu waseme kuwa imeuzwa wakitaka ukweli
waje hapa ili waione kuliko kusema tu bila ya kujua ukweli na waache kuvumisha
vitu ambavyo havina ukweli,” alisema Injinia Mchomba.
Aidha alisema kuwa kwa
sasa kuna mradi unaotekelezwa ambao utavifikia vitongoji vyote vya Jimbo la
Chalinze ambapo awamu ya tatu utatumia bilioni 60 hadi kukamilika.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Ubena
MBUNGE wa Jimbo la
Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amelipongeza Jeshi la
Magereza mkoani Pwani kwa ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya Sekondari ya Bwawani
kwa gharama nafuu.
Aliyasema hayo wakati
akizindua madarasa hayo kwa ajili ya wanafunzi wa kutwa wa shule hiyo ambayo
inamilikiwa na Jeshi hilo la Magereza eno la Ubena.
Ridhiwani alisema kuwa
Jeshi hilo limeonyesha uzalendo wa hali ya juu na kutumia vizuri rasilimali
fedha kwa kujenga madarasa hayo yenye mawili thamani ya shilingi milioni 31.8.
“Haya ndiyo mambo
tunayoyataka kwa kufanya ujenzi wa vitu vya umma kwa matumizi mazuri ya fedha
na ujenzi bora hivyo taasisi nyingine za serikali zinapaswa kuzingatia ujenzi
kama huu,” alisema Ridhiwani.
Alisema baadhi ya
taasisi za umma zimekuwa zikifanya ujenzi wa kawaida kwa gharama kubwa huku
ukiwa haujazingatia ubora wa ujenzi wa majengo ambayo hutumiwa kwa muda mrefu.
Aidha alizitaka
halmashauri kuwatumia wataalamu wa Magereza katika ujenzi wa majengo mbalimbali
ambapo ujenzi wao unazingatia ubora matumizi bora ya rasilimali fedha.
Awali akimkaribisha
mbunge huyo mkuu wa Magereza mkoa wa Morogoro Kato Lugainunula ambaye alimwakilisha mkuu wa
Magereza nchini John Minja, alisema kuwa lengo la Magereza ni kuihudumia jamii
katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu.
Lugainunula alisema
kuwa awali shule hiyo ilitumika kutoa elimu ya sekondari kwa watumishi wa
Magereza ambao walikuwa hawajapata elimu ya sekondari lakini waliondoa
utaratibu huo na kutoa elimu kwa wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali.
Naye kaimu mkuu wa
shule hiyo ya Bwawani Emanuel Lwinga alisema kuwa madarasa hayo ni kwa ajili ya
wanafunzi wa kutwa ujenzi wake ulitumia muda wa miezi mitano hadi kukamilika
kwake.
Lwainga alisema kuwa
kila darasa lina uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 40 na 45 ambapo shule hiyo
ina jumla ya wanafunzi 396 wakiwemo wale wa kidato cha tano na shule hiyo ni
moja ya shule zinazofanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne kimkoa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment