Sunday, January 4, 2015

WALILIA WODI YA WAZAZI

Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wa Kijiji cha Kwaruhombo kwenye Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametoa kilio cha kujengewa wodi ya wazazi kwenye kituo cha afya cha Kwaruhombo ili wanawake wajawazito wasijifungue kwenye wodi za kawaida.
Akizungumza kijijini hapo wakati wa ziara ya maendeleo ya mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, Hadija Stambuli alisema kuwa akinamama wamekuwa wakijifungulia kwenye wodi hivyo kutokuwa na usiri.
Stambuli alisema kuwa hiyo imekuwa changamoto kubwa kwa akinamama wanapokwenda kujifungua wamekuwa wanashindwa kusitiriwa wakati wa uzazi.
“Tunakuomba Mbunge wetu utusaidie wakinamama ili tunapokwenda kujifungua kwani hakuna usiri hivyo tungepata jengo maalumu kwa ajili ya kujifungungulia ingekuwa vizuri,” alisema Stambuli
Akijibu malalamiko hayo mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa kujifungua ni jambo jema na linahitaji usiri.
Ridhiwani alisema kuwa kwa kushirikiana na halmashauri ili kuhakikisha kunakuwa na jengo kwa ajili ya kinamama kujifungulia.
“Tutakaa na uongozi wa Halmashauri ili kuhakikisha kunakuwa na jengo maalumu kwa ajili ya kujifungulia ili kuwaondolea fadhaa akinamama wakati wakijifungua,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisikitishwa na matumizi mabaya ya mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa wanaopata rufaa na kuutaka uongozi wa kituo hicho kuhakikisha kinadhibiti matumizi hayo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment