Wednesday, January 14, 2015

MRADI WAMI CHALINZE KUNUFAISHA 271,000

Na John Gagarini, Chalinze

MRADI wa Maji wa Wami Chalinze awamu ya tatu  mara utakapokamilika unaratajia kuwafikia wananchi 271,000 wa Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.

 Aidha mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 60 unatarajia kuanza mwezi Machi mwaka huu utapunguza tatizo la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Chalinze ambao wanahudumiwa na mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) Mhandisi Christer Mchomba alisema katika awamu hiyo itaongeza mitandao ya maji kwenye vitongoji 210 kutoka kwenye vijiji 47 ambavyo vilifikiwa kwenye utekelezaji wa awamu ya pili iliyoanza mwaka 2008.

 “Katika awamu ya tatu ya mradi huu yatajengwa pia matenki ya kuhifadhia maji kwenye vijiji 20 vya awamu ya kwanza kikiwamo kijiji cha Bwiringu, Msata, Lugoba, Msoga, Mandela na vingine ambavyo havikujengewa matenki,” alisema Mhandisi Mchomba.

Mhandisi Mchomba alisema kwa sasa awamu ya pili ,wizara inakamilisha ujenzi wa nyongeza ya chujio la maji ambalo litaongeza wingi wa maji yanayosafishwa na kuzalishwa.

Alisema kuwa watajenga tanki kubwa eneo la Mazizi lenye uwezo wa kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 200,000 pamoja na vituo vya maji kwenye vijiji na vitongoji vyote kwenye Jimbo hilo.

“Kwa sasa wanazalisha maji kwa asilimia 85 tu kutokana na mashine kushindwa kufanya kazi kikamilifu ambapo kwa siku ni mita za ujazo 2,000 badala ya 5,000 kwa siku,” alisema Mhandisi Mchomba.  

Kwa upande wake ofisa maabara wa mradi huo Riziki Kacheche alisema  kuwa maji ghafi yanapokuwa machafu zaidi tope huziba na kuzuia maji kuchukuliwa katika kiwango kinachotakiwa kwenda kusafishwa na hivyo kusabababisha uwezo wa kuzalisha maji na kuyasafisha kuwa mdogo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment