Monday, February 25, 2013

MWANAFUNZI AFANYIWA UNYAMA



Na John Gagarini, Kibaha
MWANAFUNZI wa shule ya sekondari ya Pangani Kata ya Pangani ambaye alikuwa aingie kidato cha pili mwaka huu mwenye umri wa miaka (16) ameshindwa kwenda shule baada ya kutekwa na vijana watatu kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo alipata mimba na vijana hao waliitoa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha huku akibubujikwa na machozi alisema kuwa vijana hao ambao ni wakulima kati yao wawili ni ndugu walimteka kwa kutumia visu walivyokuwanavyo.
Aliwataja vijana hao ambao anawatuhumu kumfanyia kitendo hicho kuwa ni Jonas Edward, Isaka Joseph na Faida Joseph ambao ni ndugu walimteka Novemba 3 mwaka jana baada ya kumdanganya kuwa anatakiwa kwenda kuchukua mzigo wa ndugu yake.
“Baada ya kwenda kufuata mzigo huo niliwakuta wakiwa na visu vitatu ambapo kila mmoja alikuwa na kisu na kunipeleka kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi kusema kuwa hapo ndipo nitakapokuwa naishi na endapo nitajaribu kutoka basi wataniua,” alisema mwanafunzi huyo.
Alisema kuwa kwa kipindi chote hicho walikuwa wakifunga mlango kwa nje kwa kutumia kufuli kwa nje hali ambayo ilimfanya ashindwe kutoka pia ikizingatiwa kuwa nyumba hiyo iko mbali na nyumba zingine na kuwa katika kichaka.
“Faida ambaye ndiye aliyenifanya kama mke wake alinipa mimba lakini baada ya kuona hivyo walinilazimisha kuitoa kwa kutumia majani ya chai ambayo yalichemshwa na maji na kuniamuru ninywe na kusababisha mimba kutoka ambapo nilitokwa na damu nyingi na kupata maumivu makali,” alisema mwanafunzi huyo.
Aidha alisema kuwa walimtengenezea kajumba kadogo kwa kupanga matofali na miti kisha yeye kuingia humo mfano wa kaburi ambapo alikuwa akijisaidia kwenye mifuko ya plastiki na chupa kwa ajili ya haja ndogo na kuoga ni humo ndani.
“Kwa upande wa chakula walikuwa wakipika usiku tu kwani walikuwa wakifika majira ya saa sita au saba usiku wanapika tunakula ila asubuhi na mchana nilikuwa sili chakula hata mavazi yangu waliyachoama moto nikawa navaa nguo ya moja ya vijana hao,” aliongeza.
Aliongeza kuwa siku moja vijana hao walisahau kufunga mlango na ndipo alipotoka na kuomba msaada kwa mtu ambaye alimpeleka hadi nyumbani kwa walezi wake ambao ni babu na bibi yake ambao ndiyo waliokuwa wakiishi naye kwa muda wote.
Kwa upande wake babu wa mwanafunzi huyo Daud Zakayo alisema kuwa mwanafunzi huyo alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na walifanya jitihada kumtafuta ambapo walitoa taarifa polisi na kwa ndugu lakini bila ya mafanikio.
Zakayo alisema kuwa baada ya mjukuu wao kupatikana walitoa taarifa polisi ambapo vijana hao walikamatwa kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo. Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa bado hajapata taarifa.
Mwisho.  

RAGE ACHANGIA TAWI LA SIMBA KIBAHA



Na John Gagarini, Kibaha
MWENYEKITI wa Klabu ya Simba Ismail Aden Rage ameendesha harambee kuchangia tawi la Simba Kwa Mfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya shughuli mbalimbali ambapo alifanikisha kupatikana kwa kiasi cha shilingi 420,000.
Harambee hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki Kwa Mathias wilayani Kibaha kwenye ukumbi wa Back Yard ambapo mbali ya kuendesha harambee walijadili mambo mbali mbali ya kuisaidia klabu hiyo kufanikiwa kwenye mashindano mbalimbali.
Rage alitoa kiasi cha shilingi 100,000 ikiwa ishara ya kuanzisha harambee hiyo na kufuatiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa NEC kutokea wilayani Kibaha Rugemalila Rutatina ambaye alitoa kiasi cha shilingi 100,000.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka yeye aliahidi kutoa kutoa kiasi cha shilingi 100,000 na wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo nao walichangia fedha na kufikia kiasi hicho.
“Fedha hizi zilizochangwa zinapaswa kutumika kwa ajili ya malengo yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti pamoja na mambo mbalimbali ya tawi,” alisema Rage.
Aliwataka wadau wa Simba kujitokeza kuisaidia timu yao ili kuhakikisha inafanikiwa kutetea ubingwa wake wa ligi kuu ya Voda Com ambao kwa sasa inaonekana kama imeuweka rehani baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mwisho.

MBUNGE AREJEA KAZINI BAAADA YA KUUGUA KWA MIEZI SABA

HATIMAYE Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo Said Bwanamdogo ameanza kazi baada ya kurejea toka nchini India  alipokuwa akipatiwa matibabu tangu alipougua miezi saba iliyopita wakati wa kikao cha Bunge mjini Dodoma Julai mwaka jana ameanza kazi kwa kuahidi kutekeleza ahadi zote zilizobaki alizoahidi.

  alitoa ahadi ya kutoa kiasi cha shilingi milioni nne kwa ajili ya kumalizia nyumba ya Mwalimu kwenye shule ya msingi Java na mifuko 50 ya saruji katika shule ya msingi Kwamakuru,Manda Mazingara ,Kata ya Mkange ili kukarabati madarasa matano ambayo yamebomoka.

Bwanamdogo alisema mbali ya mchango huo pia atatoa 200,000 za kununulia nyavu,400,000 ya umeme wa jua katika shule ya msingi Saadan, mabati 70 katika ujenzi wa soko la Saadan na mifuko 50 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya serikali ya kijiji cha Mkange.

Alisema ahadi hizo ni za awamu ya pili baada ya kukamilisha ahadi mbalimbali alizozitoa kipindi cha uchaguzi na kuzikamilisha kupitia fedha za mfuko wa jimbo fedha , wafadhili na binafsi.

"Lengo la kutoa vitu hivyo pamoja na fedha ni kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutatua kero za wananchi zinatumika ipasavyo ili kuondoa kero ambazo zinaweza kutatuliwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi katika chaguzi mbalimbali," alisema Bwanamdogo

Aliwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM na serikali wajenge ushirikiano katika kufanya maamuzi na majukumu mbalimbali ili kuleta maendeleo hatimaye kukuza uchumi wa jimbo hilo.

"Msiwe na tabia ya kusemana ndani ya jamii na badala yake watumie vikao halali vya chama katika kuwekana sawa kama endapo kuna kiongozi anamapungufu ili kuleta heshima ya chama," alisema Bwanamdogo.

Mbunge huyo wa jimbo la Chalinze hicho ni kikao chake cha kwanza kuzungumza tangu arejee nchini India kwa matibabu mara baada ya kuugua kwa takriban miezi Saba kuaznia July 2012 alipoanza kuugua ghafla kwenye bunge lililofanyika mwezi huo.


Picha zikimuonyesha Mbunge Said Bwanamdogo akizungumza juzi katika kikao cha kwanza cha Halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mkange Tarafa ya Miono picha na John Gagarini.
4 attachments — Download all attachments   View all images   Share all images  
E89A9800.JPGE89A9800.JPG
1645K   View   Share   Download  
E89A9785.JPGE89A9785.JPG
1792K   View   Share   Download  
E89A9779.JPGE89A9779.JPG
1581K   View   Share   Download  
E89A9774.JPGE89A9774.JPG
1431K   View   Share   Download  




Friday, February 22, 2013


Na Mwandishi Wetu, Kibaha
ASKARI wa Jeshi la Polisi kituo kidogo Cha Kwa Mathiasi Wilyani Kibaha mkoani Pwani Pc Ramadhan amelazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kujeruhiwa na wananchi waliovamia kituo hicho kutaka kuwatoa watu waliowatuhumu kuwa wameiba simu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 21 mwaka huu majira ya saa 1 usiku baada ya wananchi hao kutaka kuwatoa watu waliodai kuwa wameiba simu na kutaka kuwaua.
Kamanda Matei alisema kuwa chanzo cha tukio hilo kilianza kwenye uwanja wa mpira wa miguu baina ya timu za Palasupalasu na Kigogo ya Jijini Dar es Salaam, ambapo mchezo huo uliokuwa ukichezwa kwenye uwanja wa Mwendapole kulivunjika kutokana na vurugu zilizojitokeza.
“Baada ya mchezo huo kuvunjika washabiki wa timu hizo walianza kushambuliana na ndipo watu waliotuhumiwa ambao ni Michael Mathias (30) na Hashim Noah (19) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mwanagati Jijini Dar es Salaam kukimbia kwa kutumia pikipiki na walipoona wmezidiwa waliiacha pikipiki kisha kuingia kwenye msikiti wa Tanita,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema kuwa baada ya kuingia ndani ya msikiti huo wananchi hao waliuzunguka msikiti huo kisha kutaka kuwatoa watu hao ili wawaue ndipo polisi walipofika na kuwatawanya wananchi hao lakini waligoma na kuanza kuwarushia mawe polisi ndipo polisi walipopiga risasi kuwatawanya wananchi hao.
“Katika vurugu hizo Maria Stamford alipigwa risasi ya ziwa na Idd Shukuru alipigwa mguu wa kulia kisha waliwachukuwa watu hao na pikipiki yao ndipo wanannchi hao walikwenda hadi kwenye kituo hicho wakidhani kuwa watu hao wako pale kwani waliiona ile pikipiki nje ya kituo hicho,” alisema KamandaMatei.
Aliendelea kusema kuwa walikivamia kituo hicho na kumpiga askari huyo ambaye alikuwa amevaa sare na askari mwingine Bonventura kisha kuvunja mlango na kuwaangalia watu wale lakini hawakuwakuta na kuharibu vitu mbalimbali.
“Uchunguzi ulibaini kuwa watu wale hawakuwa wezi bali walikuwa ni mashabiki wa timu mojawapo ambao walizushiwa kuwa wezi jambo ambalo si la kweli majeruhi wanaendelea vyema na matibabu na kwa sasa tayari wameunda tume ndogo kufuatilia tukio hilo na hakuna mtu aliyekamtwa kuhusiana na tukio hilo,” alisema Kamanda Matei .
Mwisho. 
  

Thursday, February 21, 2013

MISITU


Na John Gagarini, Kibaha

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki wametakiwa kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu ya upandaji miti kuliko kuvuna ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ambayo yanapelekea uoto wa asili kutoweka.

Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Katibu Tawala mkoa wa Pwani Bi Betha Swai wakati akifungua mkutano wa wataalamu wa sekta ya misitu kuweka mikakati mbalimbali juu ya kuboresha misitu kwenye mkoa huo.

Bi Swai alisema kuwa ukatiji wa miti ni mkubwa tofauti na miti inayopandwa jambo ambalo litaipelekea nchi kukumbwa na majanga yanayotokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukame, mmomonyoko wa ardhi na ukosefu wa vyanzo vya maji.

“Ni vema mkatoa elimu kwa wananchi kwa kiwango kikubwa ili wananchi wakawa na uelewa juu ya uharibifu wa mazingira na umuhimu wa kutunza misitu kwani wengi wao hawaoni umuhimu wake licha ya kuwa wanatumia zao la miti katika kujipatia kipato,” alisema Bi Swai.

Aidha alisema kuwa halmashauri na serikali nazo zijikite kwenye utoaji elimu hiyo na si kutaka tu ushuru huku misitu ikiendelea kuteketea huku mikakati ya kupanda miti ikiwa si mizuri.

“Tuachane na kusema kuwa tumegawa miti sehemu Fulani kwa ajili ya kupanda kwa sasa tuwe na mkakati wa kupanda baadhi ya maeneo mfano kwenye mabonde au sehemu ambako kumefanyika uharibifu mkubwa ili tuonyeshe na si kusema kwa maneno tu,” alisema Bi Swai.

Kwa upande wake Bakari Mohamed alisema kuwa  lengo la kuanzishwa wakala hao amabo ni wapya ni kwa ajili ya kuondoa urasimu na mfumo wa kiutendaji katika utekelezaji wa majukumu ya misitu ili kuleta ufanisi.

Bw Mohamed alisema kuwa moja ya kazi za wakala ni kuihamasisha jamii kuanzisha misitu yao na kuilinda ile iliyopo pia kuwa na vikundi vya uzalishaji nyuki kwa kutumia rasilimali ya misitu.

Mwisho.      




Monday, February 18, 2013

Na John Gagarini, Kibaha
DIWANI wa kata ya Maili Moja Bw Andrew Lugano amesikitishwa na mamalaka ya maji safi na majitaka (DAWASCO) kushindwa kuwahudumia wananchi hali inayosababisha kukosa maji kwa zaidi ya mwezi sasa.
Akizungumza mara baad aya kufanya ziara kwenye kata hiyo kuangalia maeneo ambayo yamekuwa yakikosa maji kwa muda mrefu, huku akiwa ameambatana na meneja wa DAWASCO Bw Robert Mugabe alisema kuwa hakuna sababu ya wananchi kukosa maji kwa muda wote huo na uongozi upo.
Bw Lugano alisema kuwa amekuwa akipata kero hiyo ya maji toka kwa wananchi na jitihada zake za kufuatilia zimekuwa zikigonga mwamba hali iliyomlazimu kumtoa meneja huyo ofisini kwake Jumamosi na kumwonyesha jinsi gani wananchi wanavyotaabika kwa kukosa maji.
“Siwezi kukubali kuona wananchi wakihangaika kutafuta maji huku chanzo cha maji kikiwa jirani hivyo lazima kampuni hiyo ijali wananchi ili waondokane na kero hiyo,” alisema Bw Lugano.
Moja ya wakazi wa kata hiyo ambaye anakaa mtaa wa Mzimuni Bw Mohamed Atiki alisema kuwa wamekuwa wakipata tabu kubwa ya kupata maji hali inayowasababisha kununua maji kwa bei ya shilingi 500 kwa dumu la lita 20.
“Tumekuwa tukihangaika kwa kipindi kirefu licha ya kutoa taarifa ya ukosefu wa maji kwenye kampuni hii ya maji hivyo lazima wabadili utendaji kazi wao,” alisema Bw Atiki.
Kwa upande wake meneja wa DAWASCO Kibaha Bw Robert Mugabe alisema kuwa tatizo kubwa lililosababisha wananchi kukosa maji ni kutokana na ujenzi wa barabara katika kata hiyo.
“Mabomba mengi yamekatwa kutokana na ujenzi wa barabara lakini hata hivyo tayari tumewasiliana na mkandarasi ili kuangalia namana ya kuweza kurekebisha hali hiyo,” alisema Bw Mugabe.
Bw Mugabe alisema kuwa tayari wameshafanya tathmini ya uharibifu uliofanyika na wakati wowote wataanza kufunga mabomba yaliyokatwa ili wananchi hao waendelee kupata maji kama kawaida.
Mwisho.
Diwani wa kata ya Maili Moja Kibaha kushoto Andrew Lugano akizungumza na meneja wa DAWASCO Kibaha kulia Robert Mugabe, kuhusiana na kata hiyo kuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa maji (Picha na John Gagarini)


Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MWANAFUNZI wa darasa la kwanza wa  shule ya Msingi Mbaya, Geuza Patrick (12) amekufa kwa kujinyonga kwa kamba ya katani.
Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa Polisi mkoani Pwani Gregory Mushi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 13 mwaka huu majira ya saa 12 jioni huko kitongoji cha Msufini tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
Kamanda Mushi alisema kuwa mwanafunzi huyo alijinyonga kwenye Mti wa Mwembe nyumbani kwao.
Alisema kuwa chanzo cha kujinyonga bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
Aidha alisema mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
SHULE ya Sekondari ya Bundikani ya Kata ya Maili Moja wilayani Kibaha imeanza kuchukua hatua kali kwa wanafunzi wanaovaa suruali za kubana maarufu kama modo kwa kuzichana.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwalimu mkuu wa shule hiyo Flora Chibululu alisema kuwa juzi walichana suruali za wanafunzi watatu kutokana na kwenda shuleni na suruali hizo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa na tabia ya kuzirekebisha  kwa kuzibana suruali hizo licha ya kuwa zinashonwa kawaida na kukiuka taratibu za shule.
“Suruali hizo za shule hushonwa vizuri lakini wao huzipeleka kwa fundi na kuzibana sawa na miili yao maarufu kama modo, tulishawapiga marufuku kuzibadili nguo hizo lakini wanakaidi hali iliyotufanya tuchukue hatua hiyo ili kuleta nidhamu shuleni,” alisema Chibululu.
Chibululu alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikiuka taratibu za shuleni na kuiga tabia ambazo zinashusha taaluma hivyo shule itakabiliana na vitendo kinyume cha taratibu za shule.
Aidha alisema wataendelea kuzichana suruali hizo kwa mwanafunzi atakaye vaa kinyume cha sheria za shule kwani huo ni utovu wa nidhamu na lazima wanafunzi wafuate taratibu za shule.
Mwisho.  
Na Mwanidshi Wetu, Kibaha
WAFANYABIASHARA kwenye kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kupima afya zao kwa mujibu wa sheria ili waweze kuhudumia wateja wao wakiwa na afya njema vinginevyo watapelekwa mahakamani kwa kukiuka kanuni za afya.
Hayo yalisemwa na ofisa afya wa kata hiyo Ally Shah, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha na kusema kuwa watakaokataa kupima afya zao watapelekwa mahakamani.
Shah alisema kuwa hivi karibuni baadhi ya wafanyabiashara waligoma kwenda kupima afya zao wakidai kuwa kiwango cha kupima ni shilingi 5,000 ambayo ilipangwa na halmashauri wakidai kuwa ni kubwa.
“Wafanyabiashara wanatakiwa kupima afya ili kutoa huduma wakiwa na afya njema ili kuepuka maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama vile kifua kikuu na magonjwa ambayo yanaambukiza kwa haraka,” alisema Shah.
Alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa na hofu ya kupima afya kuwa wataonekana na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI jambo ambalo alisema kuwa upimaji huo hauhusiani na kupima vipimo vya ugonjwa huo.
“Wasihofie kupima afya kwani magonjwa yanayopimwa hayahusiani na ugonjwa wa UKIMWI na kama mtu anataka kupima ugonjwa huo ni hiyari yake mwenyewe na si kwa lazima kama sheria inavyoelekeza,” alisema Shah.
Aidha alisema kuwa magonjwa yanayopimwa ni pamoja na magonjwa ya zinaa, kifua kikuu na haja kubwa hivyo wafanyabiashara wapime afya zao kwani ni kwa faida yao na wateja wanaowahudumia.
Katika hatua nyingine alisema kwa sasa wanaendelea na kuboresha usafi wa mazingira ambapo vimeundwa vikundi mbalimbali vya usafi kwa ajili ya kuhakikisha mazingira ya Mji wa Kibaha ambapo sheria ndogondogo ya halmashauri inawatoza kiasi cha shilingi 50,000 kwa mtu atakayechafua mazingira.
Mwisho.