Na Wellu Mtaki,Dodoma.
Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Dodoma Dr. Dickson Chilongani amewataka wahumini wa kanisa hilo kuwekeza nguvu kazi kwa wanawake kwani ukiwekeza kwa mwanamke unakuwa umenufaika.
Kauli hiyo ameitoa Leo Tarehe 31 March 2024 Katika kanisa la Dayosisi Central Tanganyika Dodoma wakati akilihubiria kanisa kuhusu habari za yesu kristo Mleta Mageuzi pamoja na kueleza habari za kuwekeza Mwanamke kuharakisha Maendeleo.
Amesema kuwa lazima mkubali kwamba ukiwekeza kwa mwanamke mwisho wa yote inalipa ila kwa wanaume inaweza isikulipe na ifikiapo wakati unawaitaji wanaweza usiwaone kwenye itaji lako.
"Wekeza kwa wanawake: Harakisha maendeleo.” Kwa kauli mbiu hii wanawake walitaka watambuliwe na waaminiwe zaidi kuwa wanaweza. Na hapa tena siku ya pasaka tunawaona wanawake wakiwa mstari wa mbele. Saa 12 Alfajiri wakati wanaume bado wanachapa usingizi, Mariamu Magdalene, Mariamu mamaye Yakobo na Salome wanakwenda kaburini na manukato ya thamani ili kuupaka mwili wa Yesu. Wanafanya hivi kwavile Yesu aliposulubiwa, sabato ilikuwa inakaribia na kwahiyo mazishi yalikuwa ni ya haraka haraka, hawakuwa na muda wa kuuandaa mwili wake kwa maziko" Amesema Chilongani.
"Kwahiyo saa 9 mchana Yesu anapokata roho, wanaoshuhudia kifo chake ni wanawake. Inapofika jioni, Yesu anapozikwa, wanaoshuhudia kaburi na mazishi yake ni wanawake. Wanaume wameingia mitini" amesema Chilongani
Aidha amehisihi jamii kuwe na usawa ambao utasaidia kumuwesesha mwanamke kujiamini Katika kujikomboa kimaisha kwani kumekuwa na mageuzi makubwa sana kwa wanawake na hii ndio inahashiria wanawake wanaweza kuongoza .
"Haya ni mageuzi makubwa sana, kwavile wakati huu wa Yesu Israeli ilikuwa ni nchi yenye mfumo dume na ukilitimba uliokithiri kwelikweli dhidi ya wanawake. Mwanamke alikuwa si kitu. Ndio sababu hata katika Yohana 6 tunasoma kwamba Yesu alilisha watu 5000 kwa samaki 2 na mikate 5. Lakini waliohesabiwa walikuwa ni wanaume peke yao, wanawake hawakuhesabiwa. Ni kana kwamba walikuwa si binadamu. " Amesema Chilongani
Pia amesisitiza wahumini wa kanisa hilo watambue kuwa mwanamke ni mtekekezaji mzuri wa majukumu na hanahakikisha anafanya kazi kwa weledi bali wapo watu ambao awana imani naye na hao ndio wanapelekea kushusha uchumi wa mwanamke kiujumla.
"Na hata katika mahakama za Israeli ushahidi wa mwanamke kisheria ulikuwa haukubaliki. Lakini bado Yesu anawafanya wanawake kuwa mashahidi wa kufufuka kwake na anawatuma wawaambie wanafunzi wake waende Galilaya watamkuta" amesema Chilongani.
Aidha amewataka wahumini wamtangulize Mungu Katika maitaji ya maombi Yao na waachane na tabia ya kupanga aina ya maitaji wanayoyataka kwa Mungu Bali wamwache Mungu atatenda mwenyewe.
"Ni lazima tujifunze kumtanguliza Yesu Kristo na siyo kumtangulia. Askofu Mkuu mstaafu marehemu John Ramadhani aliwahi kusema: “Wakristo wengi badala ya kumtanguliza Roho Mtakatifu wanamtangulia”. Mtu badala ya kumwomba Mungu ampe mke mwema, anampa Mungu masharti kwamba anataka mke mweupe tena mwenye mwanya. Huko ni kumtangulia Mungu. Badala ya kuomba gari, anaomba Scania, wakati hata baiskeli yenyewe hana. Huko ni kumtangulia Mungu. Kumtanguliza Mungu ni kumwomba mke au gari na kuacha mapenzi yake mema yatimizwe" amesema Chilongani
Pia hamewahimiza wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi Katika ngazi ya kanisa na serikali kwa ujumla na kuzingatia usawa wa kijinsia.
"Somo linatutaka tuwaamini wanawake na tuthamini mchango wao katika kanisa na jamii. Katika kanisa mwaka huu Dayosisi yetu ina mkutano mkuu (sinodi), na tumeanza chaguzi mbalimbali katika ngazi zote. Ningeomba sana kuwe na usawa. Zisiwepo nafasi za wanaume peke yao na za wanawake peke yao" amesema Chilongani
"Katika taifa, chaguzi pia zimeanza kufanyika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Ni vyema kuwe na usawa, tuwaamini wanawake. Kubwa zaidi, kumekuweko na baadhi ya wanaume wanaomzodoa Rais Samia kana kwamba hawezi lolote kwasababu tu ni mwanamke. Ni kana kwamba hawaoni kazi ambazo Rais wetu amezifanya katika kipindi chake hiki kifupi cha uongozi. Watu wa jinsi hii ni wabinafsi na hawatufai katika jamii" amesema Chilongani
Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu ni kanisa la Kiuaskofu katika Dayosisi ya Central Tanganyika. Dayosisi ya Central Tanganyika ilianzishwa mwaka 1927. Ilikatwa kutoka Dayosisi ya Mombasa. Kabla ya hapo Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na DRC Congoeneo lote hili lilikuwa chini ya umisheni wa CMS Afrika na kujulikana kama Dayosisi ya Eastern Equatorial Africa na Askofu wa kwanza alikuwa James Hannington (1884 – 1885). Huyu alikuwa shahidi wa kwanza baada ya kuuwawa na Kabaka Mwanga katika eneo la Busuga nchini Uganda 29/10/1885.