Na Mwandishi Wetu, Makambako
WAFANYABIASHARA wa pembejeo Soko Kuu la Mji wa Makambako, mkoani Njombe, wamemshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuweka ruzuku ya mbolea iliyorahisisha shughuli za kilimo na upatikanaji mazao ya kutosha kwa wakulima mkoani humo.
Wizara ya Kilimo mwaka 2023/24, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), inaendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea nchini kutoa ruzuku kwa wakulima hadi mwaka 2025/26 ili kuongeza matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 hadi kilo 50 kwa hekta, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa mazao.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Pembejeo za Kilimo mkoani Njombe, Abdusalim Mangoma alitoa pongezi hizo kwa niaba ya wenzake wakati akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara Tanzania (JWT), katika ofisi za jumuiya hiyo zilizopo Mji Mdogo wa Makambako.
Vìongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wake Hamis Luvembe, wanafanya ziara ya kutembelea wafanyabishara wa mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na kusajili wanachama wake.
Sanga alisema hatua ya serikali kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima imeonesha matokeo chanya kwenye uzalishaji mazao katika mkoa huo.
"Wakulima sasa wananunua mbolea kwa utaratibu maalum, tofauti na awali hawakuwa wanaunua mbolea kwa sababu bei zilikuwa siyo rafiki kwao hivyo kushindwa kupata mazao ya kutosha," alisema.
Naye Katibu wa wafanyabiashara hao, Mhema Wakala, alisema mfumo wa usajili wakulima umesaidia kutambulika maeneo walipo na mashamba yao.
"Hii imetusaidia wasambazaji wa mbolea kuwatambua wakulima na kuwafikia kwa urahisi hadi waliopo vijijini," alisema Wakala.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Njombe na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Sifael Msigala, alisema wafanyabiashara wa mikoa hiyo wanatekeleza majukumu yao kikamilifu kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa serikali ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katibu wa JWT, Abdallah Salim, aliwasihi wafanyabishara kutekeleza vyema majukumu yao kwa kufuata taratibu na kanuni za serikali kwa sababu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anasikiliza na kuzifanyia kazi kero zinazowakabili.
"Endeleeni kufanyabiashara huku mkitembea kifua mbele kwa sababu Rais Dkt. Samia tunaendelea kumfikishia kero zenu na kuzifanyia ufumbuzi, lengo ni wafanyabishara kuwa na ustawi kwenye taifa latu," alisema.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa JWT, Ismail Masoud, alisema Rais Dkt. Samia ni kiongozi wa mfano kwa sababu amegusa moja kwa moja matatizo ya wafanyabiashara nchini.
Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akizungumza Agosti 8, 2023 kwenye kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane, jijini Mbeya, alisema eneo la uzalishaji kabla ya ruzuku ya mbolea lilikuwa ekari 10,440,000 mwaka 2021/2022 hadi kufikia hekta 11,137,874.
Aidha, matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka hekta 363,599 mwaka 2021/22 hadi tani 580,529 5085,590 mwaka 2022/23
Uzalishaji wa chakula umeongezeka kutoka tani. 17,148,290 mwaka 2021/22 hadi tani 20,42,014 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la tani 3,000,000.
Aidha, mbolea zitakazohusika kwenye ruzuku ni mbolea za kupandia na kukuzia ambapo DAP kwaajili ya kupandia na Urea kwaajili ya kukuzia ambazo ni takribani asilimia 50 ya matumizi ya mbolea nchini.
Mbolea za kupandia na kukuzia za aina zingine zinahusika kwenye ruzuku kulingana na mahitaji ya soko.