Na John
Gagarini, Kibaha
FAMILIA nane
zenye watu zaidi ya 20 kwenye mtaa wa Mharakani kata ya Picha ya Ndege wilayani
Kibaha mkoani Pwani zimenusurika kufa baada ya moto kutokea wakati wamelala.
Wakizungumza
na mwandishi habari hizi wahanga wa tukio hilo la moto huo ambao ulitokea
Agosti 7 usiku kuamkia Agosti 8 majira ya saa 6;30 usiku walisema kuwa watu
waliokuwa jirani na nyumba yao ndiyo waliowafahamisha juu ya moto huo ambao
unasadikiwa ulianzia kwenye moja ya maduka yaliyo kwenye nyumba hiyo.
Emanuel Mhina
alisema kuwa wao walikuwa wamelala na ilipofika majira ya saa saba kasoro
waliamshwa na watu na walipoamka walikutana na moto mkubwa ambao hawakujua
ulianza saa ngapi ndipo walipoanza kujiokoa.
“Tunamshukuru
mungu tumenusurika licha ya mali zetu zote kuteketea kwa moto ambao ulianzia kwenye
moja ya maduka ambayo yameungana na nyumba hii ambayo tulikuwa tunaishi,”
alisema Mhina.
Naye Said
Juma alisema kuwa moto huo umewapa hasara kubwa kwani amepoteza vitu karibu
vyote na kufanikiwa kuokoa vichache hali ambayo inamfanya aanze upya maisha.
Kwa upande
wake mwenyekiti wa mtaa huo Yahaya Abdala alisema kuwa wananchi, Zimamoto
pamoja Jeshi la polisi walifanikisha kuzimwa moto huo ambao ulisababisha vitu
vote kuteketea lakini hakuna mtu aliyedhuriwa na moto huo zaidi.
Naye diwani
wa kata ya Picha ya Ndege Robert Machumbe alisema kuwa wahanga hao hawakuweza
kuokoa kitu kwani vitu vyote viliteketea kwa moto huo uliokuwa mkali.
Machumbe alisema
kuwa baada ya tukio hilo walichangisha kwa majirani na kupata kiasi cha
shilingi 80,000 ambazo ziligawanywa kwa wahanaga hao angalau wapate fedha kwa
ajili ya chakula na wahanga hao wamehamia kwa ndugu jamaa na marafiki zao
wakiangalia namna ya kutafuta nyumba nyingine.
Katika hatua
nyingine mtoto mwenye umri kati ya miaka minne na nusu amenusurika kufa baada
ya mama yake kumwacha kwenye nyumba huku akiwa amemfungia ndani na yeye kwenda
kusikojulikana ambapo kati ya majirani waliounguliwa nyumba ambaye ni
mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alijitosa na kumwokoa mtoto
huyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment