Na John Gagarini, Kibaha
MADARASA matatu na ofisi ya Mwalimu Mkuu shule ya
Msingi Kongowe wilayani Kibaha mkoani Pwani zimeungua na moto ambao ulitokea
juzi usiku na kusababisha hasara kubwa.
Akizungumza na Patapata mwenyekiti wa mtaa wa
Kongowe Maimuna Jamhuri alisema kuwa moto huo ulitokea Agosti 28 majira ya saa
nne usiku ambapo chanzo chake bado hakijafahamika mara moja.
Jamhuri alisema kuwa moto huo ulianzia kwenye ofisi
hiyo ambayo ni ya mwalimu mkuu na kuenea kwenye madarasa pamoja na chumba cha
kuhifadhia vitabu ambavyo navyo vimeteketea kwa moto huo ambao ulikuwa mkali.
“Moto huo ulizimwa na wananchi ambao walijitokeza
kwa wingi ambapo gari la zimamoto lilifika kwa kuchelewa kutokana na kuwa kwenye
harakati za kuzima moto sehemu nyingine”, alisema Jamhuri.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kongowe Iddi
Kanyalu alisema kuwa baada ya kutokea moto huo viongozi kadhaa walifika akiwemo
mkurugenzi, Mwenyekiti na Injinia wa Halmashauri kwa ajili ya kuangalia athari
za moto huo.
Kanyalu alisema kuwa kutokana na makisio ya
harakaharaka zinahitajika zaidi ya milioni 50 kwa ajili ya kujenga upya
madarasa hayo na ofisi kwani madarasa hayo yameharibika sana na hayafai kwa
matumizi wala kufanyiwa ukarabati.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo leo kamati ya
maenedeleo ya kata ina kaa kuangalia namna ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo
limewakumba wanafunzi 200 waliokuwa wanatumia madarasa hayo.
Naye mtendaji wa kata hiyo ya Kongowe Said Kayangu
alisema kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Beatus Lingumbuka alitapa athari kidogo
kichwani na mikononi kwani alikuwa kwenye harakati za kujaribu kuokoa baadhi ya
vitu wenye ofisi yake.
Kayangu alisema kuwa kutokana na jitihada za
wananchi wameweza kuokoa madawati kwenye madarasa hayo ambayo yalikuwa hatarini
kuungua lakini hata hivyo waliweza kuyatoa na hakuna dawati hata moja
lililoungua
Mwisho.
No comments:
Post a Comment