Na John Gagarini, Rufiji
IMEELEZWA kuwa kuwepo kwa migogoro ya ya wakulima
na wafugaji katika Halmashauri ya Rufiji mkoani Pwani kunatokana na
baadhi ya wafugaji kuvunja sheria na taratibu zilizowekwa na kwenda
kulisha mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa maalumu kwa ajili ya shughuli
mbali mbali za kilimo.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Jimbo la Rufiji
Mkoani humo Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza na viongozi wa Halmashauri
Mpya ya Rufiji ambapo ameahidi kulivalia njuga suala la migogoro ya ardhi
inayotokana na jamii ya wafugaji na wakulima ambao wamekuwa wakigombania maeneo
ya mashamba na kusababisha kutokea kwa mapigano ambayo wakati mwingine
yanapelekea uvunjifu wa amani.
Mchengerwa alisema kuwa hawezi kuwavumilia wale
wote ambao wataonekana wanakwenda kinyume cha sheria za nchi, na kuhakikisha
kila mfugaji na mkulima anatengewa maeneo yao rasmi kwa ajili ya kufanyia
shughuli zake ili kuepukana na migogoro na mapigano ambayo yamekuwa
yakijitokeza kutokana na kugombania ardhi.
“Nitaweka mikakati kabambe ambayo itaweza
kuwawasaidia wananchi wakiwemo wafugaji na wakulima kwa kushirikina na viongozi
wa halmashauri katika kuwatenge maeneo yao maalumu ambayo yataweza kusaidia
kuepukana na migogoro hiyo ya ardhi,” alisema Mchengerwa.
Alisema kuwa anatambua kuwepo kwa changamoto kubwa
na migogoro kati ya wakulima na wafugaji, lakini dhamira yake kubwa
anataka kuona wanachi wake wa jimbo la rufiji wanakaa kwa amani bila ya kuwepo
kwa mapigano yoyote na kuhakikisha kwamba sula la amani na utulivu linakuwepo.
“Natambua wananchi wengi wa Jimbo la Rufiji wanategemea
sana shughuli za kilimo hivyo kwa sasa wameshaweka utaratibu wa kutenga maeneo
ya wafugaji ili wasiweze kuingia katika mashamba ya wakulima na kupelekea
vurugu za mara kwa mara kitu amabcho sio kizuri na kinarudisha nyuma maendeleo,”
alisema Mchengerwa.
Naye Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rufiji Saidina Malenda mara baada ya kushinda katika uchaguzi huo alisema
atahakikisha anasharikina bega kwa bega na viongozi wenzake kwa lengo la
kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi wa Rufiji.
Malenda alisema kuwa anawashukuru madiwani wenzake
kwa kuweza kumchagua kuwaongoza na kubainisha kwamba atafanya kazi bidii zote
na kwa kushirikina katika mambo mbali mbali ya kimaendeleo bila ya kuwa
na ubaguzi wa aina yoyote wa itikadi ya vyama ili kuweza
kuwatumikia wananchi katika huduma mbali mbali wanazozihitaji.
Katika uchaguzi huo wa halmashauri mpya ya Wilaya
ya Rufiji,uliofanyika utete nafasi ya Mwenyekiti ilikwenda kwa Saidani Malenda
ambaye alipata kura 11 kati ya kura 19 zilizopigwa, ambapo nafasi ya Makamu
mwenyekiti ilikwenda kwa Hawa Mtopa ambaye aliyepata kura 10 katika ya
kura 19 zilizopigwa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment