Tuesday, August 30, 2016

WAILILIA HALMASHAURI KUWAJENGEA SOKO BAADA YA SOKO KUTAKIWA KUVUNJWA

Na John Gagarini, Kibaha
USHIRIKA wa Wafanyabiashara wa Soko la mkoa la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wameiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwapatia eneo lingine la kufanyia biashara baada ya eneo wanalofanyia shughuli zao ambalo liko chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa kuvunjwa baada ya miezi mitatu kuanzia mwezi Agosti.

Akizungumza mara baada ya mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika mjini Kibaha mwenyekiti wa ushirika huo Ally Gonzi alisema kuwa hadi sasa hawajui hatma yao mara zoezi hilo litakapofanyika.

Gonzi tunaiomba Halmashauri kutujengea soko au kama hawataweza kujenga ndani ya muda huo wa miezi mitatu ni vema wakaiomba wakala hao kutuongezea muda wa kuwa hapa hadi pale tutakapokuwa tumejengewa soko jipya.

“Tunamwomba Rais John Magufuli kutuangalia kwani hapa tuko zaidi ya miaka 30 na hadi sasa Halmashauri bado haijatujengea soko ambalo waliahidi kutujengea kutokana na eneo hilo kutokuwa la halmashauri,” alisema Gonzi.

Alisema kuwa kwa kipindi kirefu Halmashauri hiyo imekuwa ikiahidi kuwajengea soko la kisasa kwenye kitovu cha mji lakini hadi wanapewa barua za kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo na Tanroads hadi sasa hawajajengewa soko.

“Tunachoona kwa sasa kwa kuwa soko bado halijajengwa ni vema wakatuongezea muda hata wa miaka miwili kwani Halmashauri ilisema itakuwa imejenga soko ndani ya miezi 18 hivyo kwa kipindi hicho ni bora tungebaki hapa kwanza lakini vinginevyo hatujui tutakwenda wapi,” alisema Gonzi.

Aidha alisema kuwa mbali ya wao kutokuwa na mahali pa kufanyia biashara pia Halmashauri itakosa mapato kwnai soko hilo ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato pia wao walikuwa wakitegemea hapo kwa ajili ya kujipoatia kipato chao na familia zao.


Mwisho. 

No comments:

Post a Comment