Thursday, August 11, 2016

MAJAMBAZI YAMUUA KWA KUMPIGA RISASI MWANAMKE ALIKWENDA DUKANI KUWEKA MUDA WA HEWANII

Na John Gagarini, Kibaha

MKAZI wa Mtaa wa Karabaka-Misugusugu kata ya Misugusugu wilayani Kibaha mkoani Pwani Zawadi Halfan (25) ameuwawa kwa kupigwa risasi na majambazi wakati akisubiri kuunganishiwa kifurushi cha muda wa maongezi kwenye simu yake.

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa marehemu alikuwa amekaa kwenye benchi kwenye kibanda cha huduma za fedha kwa mtandao mali ya Gaitano Joseph (30).

Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 9 majira ya saa 2:30 usiku kwenye mtaa huo ambapo marehemu alikuwa akisubiri huduma hiyo kabla ya mauti kumkuta.

“Marehemu hakuwa mlengwa bali walikuwa wamemlenga Yohana Koseja (24) ambaye ni mfanyakazi wa Mchungaji Raphael John ambaye ni mmiliki wa duka la M-Pesa ambapo majambazi hao baada ya kufika walimwamuru Yohana asimame baada ya kufunga duka hilo lakini alikimbia na kukaidi agizo la majambazi hayo ambayo yalikuwa matatu,” alisema Mushongi.

“Kutokana na Yohana kukimbia majambazi hayo yalianza kufyatua risasi ndipo moja ilimpata marehemu sehemu ya mgongoni upande wa mgongoni na kufariki papo hapo ambapo  walikuwa wakifyatua risasi hizo kwa Yohana wakimhisi kuwa alikimbia na fedha bada ya kufunga duka,” alisema Mushongi.

Alisema baada ya majambazi hao kutoka kwenye tukio la kwanza walivamia duka lingine la M-Pesa lililopo pamoja na duka la madawa ya binadamu linalomilikiwa na Renovatus Katabalo (29) mfanyabiashara na mkazi wa Kongowe ambapo duka lake lipo eneo hilohilo la Karabaka na kupora kiasi cha shilingi 300,000.

“Chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali na msako unaendelea mkoa mzima ili kuwakamata watuhumiwa ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili za mauaji ambapo eneo la tukio maganda ya risasi aina ya SMG/SAR,” alisema Mushongi.  

Mwisho.


No comments:

Post a Comment