Na John Gagarini, Chalinze
MWENYEKITI wa Halmashauri ya mji wa Chalinze
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Said Zikatimu ameutaka uongozi wa Kitongoji Cha
Msanga kata ya Talawanda uhakikisha inamkamata mtu ambaye anatishia kuwabaka
wanafunzi wa shule ya Msingi Msanga.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Talawanda
wakati wa ziara yake kuangalia shughuli za maendeleo kwenye kata ya Talawanda
alisema kuwa mtu huyo hapaswi kuachwa kwani anahatarisha afya za wanafunzi hao.
Zikatimu alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wakike wa
shule hiyo tayari wameshatoa taarifa dhidi ya mtu huyo ambaye huwa anawakimbiza
kwa nia ya kuwafanyia kitendo hicho na endapo hatakamatwa anaweza kutekeleza
azma yake hiyo mbaya.
“Mtu huyo inasemekena yuko Kijijini hapa amekuwa
akificha sura yake ili asifahamike amekuwa akijificha kwenye vichaka na kuwakimbiza
wanafunzi kwa nia ya kutaka kuwabaka hivyo lazima viongozi muweke mtego ili
mumkamate mtu huyo ambaye ni hatari,” alisema Zikatimu.
Alisema kuwa serikali haiwezi kukaa kimya kwa mtu
wa namna hiyo ambaye ni hatari kwa wanafunzi na kuwafanya watoto wa kike
wasisome kwa amani hivyo lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kumdhibiti
mapema.
“Lazima mfanye mpango wa kumkamata mtu huyo pia
mnaweza kupiga kura ili kumbainisha mtu huyo ambaye baadhi ya watu wanamfahamu
na wengine hawamfahamu ambapo kwa kutumia kura anaweza kufahamika kwa urahisi,”
alisema Zikatimu.
Aidha alisema kuwa kamati za ulinzi na usalama ya
Kijiji na Kitongoji zinapaswa kulishughulikia suala hilo na wananchi
kutolifumbia macho kwani mtu huyo anaweza kufanya kweli endapo hatua
hazitachukuliwa mapema.
No comments:
Post a Comment