Monday, August 8, 2016

MWILI WAKUTWA VICHAKANI UKIWA UMEPIGWA RISASI KIDEVUNI


Na John Gagarini, Kibaha

MWILI wa mtu mmoja ambaye jina lake ambalo halikuweza kufahamika mara moja mwenye umri kati ya miaka (33) na (38) umeokotwa huku ukiwa umepigwa risasi chini ya kidevu na kutokea utosini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa mtaa wa Lulanzi kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani Thobias Shilole alisema kuwa marehemu aliuwawa na watu wasiofahamika.

Shilole alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 7 majira ya saa 3 asubuhi kwenye korongo lililopo kwenye shamba linalomilikiwa na Saeed Yeslam Saeed ambapo watoto waliokuwa wakichunga mbuzi ndiyo waliogundua mwili huo na kutoa taarifa kwa wazazi wao ambao walitoa taarifa kwa balozi wao na ndiye aliyemjulisha juu ya tukio hilo.

“Mwili huo ulikuwa na jeraha la risasi chini ya kidevu na kufumua kichwa na mtu huyo anahusishwa na tukio lililofanyika siku kama tatu zilizopita kwa kumpiga risasi kwenye makalio na kumpora fedha mtu aliyetambulika kwa jina la Beno Nyoni (36) mkazi wa Picha ya Ndege ambaye alikuwa akijenga nyumba yake eneo la mtaa wa Lulanzi,” alisema Shilole.

Shilole alisema kuwa watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi baada ya kumshambulia walikimbia na kusababisha majeruhi huyo kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi lakini ilishindikana na kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi ambako hadi sasa anatibiwa baada ya kutolewa risasi iliyokuwa mwilini.

“Tunaiomba serikali kumlazimisha mmiliki kulifanyia usafi kwani pori kubwa ambalo limekuwa likitumiwa na wahalifu kwa ajili ya kujificha na kufanya wizi kisha kujificha huko kwani hata mwaka jana tulikuta mtu akiwa amejinyonga hivyo sehemu hiyo usalama wake ni mdogo hasa ikizingatiwa eneo hilo liko umbali wa kilometa 2 toka barabara kuu ya Morogoro,” alisema Shilole.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa baada ya kuangaliwa marehemu alikutwa na jeraha kidevuni na kichwani huku mwili wake ukianza kuharibika.

Msuhongi alisema kuwa pembeni yake kulikutwa kofia ya kuficha sura ganda la risasi aina ya SMG/SAR na nyaraka mbalimbali ambazo ni ramani za nyumba mbili, stakabadhi za kibali cha ujenzi, hati ya hukumu ya shauri la mgogoro wa ardhi.

Alisema vitu vingine vilivyokutwa ni kadi za biashara, kadi za benki za posta, NBC, Posta na CRDB, kadi ya kupigia kura na leseni ya udereva vyote vikiwa na majina ya Nyoni ambaye ni mfanyabiashara wa Picha ya Ndege.

“Vitu hivyo ni vya Majeruhi huyo aliyofanyiwa tukio hilo la unyanganyi wa kutumia silaha na kupora mali na walifika kwenye kwenye hilo kwa lengo la kugawana mali hizo lakini inaonyesha walihitilafiana ndipo walipompiga marehemu risasi na kumuua kisha walimpekekua kwani mifuko ya suruale yake ilkuwa iko nje na hakukutwa na kitambulisho chochote na mwili umehifadhiwa hospitali ya Tumbi,” alisema Mushongi.

Naye diwani wa kata hiyo Robert Machumbe alisema kuwa shamba hilo lilikofanyika tukio hilo lina pori kubwa sana hivyo ni vema Halmashauri likafanya utaratibu kama mmiliki kashindwa litolewe kwa mtaa ili kuweza kujengwa huduma za jamii kama shule, zahanati na huduma nyingine kwani kwa sasa limekuwa hatari kwa wananchi.

Mwisho.       


  



  




No comments:

Post a Comment