Na John Gagarini, Kibaha
KATA ya Pangani wilayani Kibaha inatarajia
kubadilisha ofisi za Mtaa wa Kidimu kuwa Zahanati ili kukabiliana na changamoto
ya mtaa huo kutokuwa na zahanati hivyo kufanya huduma za matibabu kupatikana
kwa ugumu.
Akizungumza na waandishi wa habari diwani wa kata
hiyo Agustino Mdachi alisema kuwa gharama za kufuata matibabu kwa wakazi wa
mtaa huo ni kubwa na kuwafanya wagonjwa kuwahatarini pale wanapokuwa wamepatwa
au kuzidiwa na ugonjwa.
Mdachi alisema kuwa tegemeo kubwa ni hospitali ya
wilaya ya Kibaha ya Mkoani ambayo iko umbali wa kilometa 18 na ile ya jirani ya
Mpiji Magohe ambayo iko kata ya Mbezi wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam
ambapo usafiri wa pikipiki ni shilingi 5,000.
“Mgonjwa anapotaka kwenda Mkoani humbidi kuwa na
shilingi 50,000 hasa nyakati za usiku na mchana ni 40,000 au 30,000 gharama
hizi kwa ajili ya kwenda kupata matibabu ni kubwa sana na kwa mwananchi wa
kawaida kumudu ni ngumu sana,” alisema Mdachi.
Alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo
wameamua kuibadili ofisi hiyo na kuwa zahanati ya mtaa ambapo wananchi watapa
huduma karibu.
“Kwa sasa tuko kwenye mchakato kwa kuwaomba
Halmashauri ya Mji kuturuhusu na kuleta wataalamu wa afya ili waangalie namna
ya kulifanya jengo hilo kuwa zahanati na tunaamini ombi letu litakubaliwa,”
alisema Mdachi.
Aidha alisema kuwa kutokana na ukubwa wa jengo hilo
la serikali ya mtaa kuwa vyumba vingi wanaamini kuwa litafaa kwa ajili ya
kuanzia huduma za kiafya wakati wanafanya mipango ya kujenga sehemu nyingine.
“Kwa kuwa ya kata ina ofisi nyingi tunaweza kutoa
chuma kimoja kwa ajili ya ofisi ya mtaa ili kufanikisha zoezi hilo ambalo
litawafanya wananchi wa mtaa na kata hiyo kupata huduma za afya karibu,”
alisema Mdachi.
Aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada za
serikali kwa kujitolea katika masuala mbalimbali ya maenedeleo ikiwa ni pamoja
na kufanikisha zoezi hilo la ujenzi wa zahanati hiyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment